Na Bakari Mwakangwale

WAISLAMU wametakiwa kuwa na utaratibu wa kuwafunza watoto wao mwenendo na tabia za kuipenda dini yao ili kuwajenga kiimani na uchamungu.

Wito huo umetolewa na Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida, Alhaji Burhan Mlau, aliyekuwa mgeni rasmi  katika Kongamano la uvaaji wa Hijabu kwa watoto wa Shule za Msingi na Sekondari Mkoani Singida.

Waislamu Mkoani Singida, Julai 19, 2020, walifanya Kongamano kubwa lililowakutanisha wanafunzi wote wa Kiislaamu wa Shule za Msingi na Sekondari, lengo likiwa ni kuwaelimisha umuhimu wa uvaaji wa vazi la Hijabu ambalo ni vazi maalumu kwa ajili ya mtoto wa kike, kina mama na watu wazima kwa ujumla.

Alhaj Malu, amesema utaratibu huu wa kuwakusanya na kuwapa semina juu ya mwenendo wa maadili ya Dini yao, watoto hawa itawapelekea kuipenda dini yao, kuelewa haki zao kiimani na kuwa mahalifa wazuri hapo baadae.

“Nimefurahishwa sana na hatua hizi, hawa watoto wetu wakirithishwa tabia hizi Uislamu utaendelea kupata heshma kubwa na kuja kuwa na jamii iliyo salama.”

“Kwa kuwafundisha uvaaji wa Stara watoto hawa kwa umri huu ni jambo zuri na la kuendeleza katika mikoa yetu yote na inawezekana hasa tukianzia huku chini kwa watoto hawa, muhimu ni kuwa na ushirikiano wa kimalezi baina ya wazazi na walimu wao.” Amesema Alhaj Mlau.

Katika hafla hiyo, Alhaj Mlau, aliwapongeze wazazi, waalimu, walezi na wanaharakati wa masuala ya kidini kwa kuwa kitu kimoja na jambo ambalo kwa sasa ndiyo kiu ya BAKWATA, na ni ndoto za Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zubeir.

Katika Kongamano hilo, Wazazi na Waislamu kutoka Taasisi mbalimbali za kidini walihudhuria kongamano hilo na kupongeza semina hiyo kwa wanafanfunzi hao mambint wa Kiislamu.

“Tunawapongeza waandaaji wa kongamano la watoto wetu na hasa kuhusu Uvaaji wa Hijabu hili ni jambo zuri na lisiishie hapa, bali liende  mbali zaidi na liwepo mara kwa mara na hata wazazi wao wa kike nao ni lazima kuhimizwa katika haya ili waweze kuwa walimu na mfano kwa watoto wao.” Amesema mmoja wa washiriki wa Kongamano hilo kwa niaba ya wenzake.

Mkoa wa Singida, umetajwa kuwa kinara katika kuhimiza suala la malezi mema ya watoto na kuweka misingi mizuri, safi na yenye alama ya Uislamu kwa mujibu wa maagizo na mafundisho ya Mtume (s.a.w) na hiyo ndio dhana halisi ya usemi usemao ‘Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.’