Masiku kumi ya Dhul-Hijja

 

Na Bakari Mwakangwale

WAISLAMU wote ulimwenguni wapo katika mwezi wa Mfungo Tatu, yaani Dhul-Hijja.

Huu ni mwezi wa pili kati ya miezi minne mitukufu, wa mwanzo ni Dul-Qa’da (Mfungo Pili) ukifuatiwa na Dhul-Hijja wa tatu ni Muharram, na wa nne ni Rajab.

Na katika miezi yote hiyo minne, Dhul-Hijja ndio mtukufu zaidi, na siku kumi za mwanzo ndizo tukufu zaidi kuliko siku nyengine ndani ya mwezi huo huo wa Dhul-Hijja.

Kwani Mwenyezi Mungu amezitilia kiapo siku hizo 10 kwa kupitia Qur an (Suratul Fajr, 89:1-2). Allah Mtukufu anasema Wal-Fajir, Naapa kwa Alfajiri. Walayaalin ashri-Na kwa masiku Kumi.

Bila shaka kinachoapiwa hapa ni masiku kumi ya Mfungo Tatu (Dhulhija).

Amesema Ibnu Kathir, Ibnu Abaas, Ibnu Zubayr na Mujaahid kuwa, makusudio ya hii ni masiku kumi ya Dhulhija na bila shaka Allah anapokiapia kitu chochote kile, tujuwe huwa kuna utukufu na fadhila na mazingiatio ndani yake.

Kwa hivyo, Aya iko wazi kabisa kuwa Allah (s.w) ameziapiya siku hizo kumi kwa utukufu wake na ubora wake na nafasi yake katika Uisalamu. Na tumeamrishwa kufanya matendo mema katika masiku haya ili tupate fadhila zake na thawabu na Ibada tofauti za kujikurubisha na Allah kwa mfano kufunga, kusali kutoa sadaqa, na kuleta aina ya dhikri kwa wingi.

Kinyume chake ni kuwa kufanya dhambi ndani ya miezi minne mitukufu ni maradufu ya dhambi ndani ya siku  nyengine nje ya miezi minne hiyo mitukufu.

Na katika Hadith iliyopokewa na  Ibn Abbas (r.a) ambae amesema,  Amesema Mtume (s w a), “Hakuna masiku matukufu yenye kupendwa matendo (kufanywa ibada ndani yake ) mbele ya Allah Kama masiku haya ...

Masahaba wakasema, hata kupigania jihaad, Mtume (s.a.w) akasema: hata kupigana Jihad ..isipokuwa mtu mmoja aliyetoka yeye mwenyewe na Mali yake Kisha asirudi na chochote kile.”

Sababu ya ubora na utukufu wa masiku haya, ni kukushanyika kwa pamoja ibada kuu ndani yake nazo ni Sala, Funga, Sadaka, na Hijja wala Hakuna kipindi hata kimoja ibada kama hizo kukushanyika hivyo, na ibada kubwa ambazo unaweza kuzifanya kipindi hichi ni kutekeleza Ibada ya Hijja na Umra.

Hii ni ibada bora na yenye fadhila kwa kuthibiti dalili kutoka kwa Mtume (s. a.w) amesema,  “kufanya Umra mpaka Umra nyengine basi ni kifutio baina yake na Hija baada ya Hija yenye kukubaliwa haina malipo zaid ya Pepo tu.