Kipekee kabisa tunapenda kuwapongeza vijana wote waliofaulu katika mtihani wa kuhitimu kidato cha nne 2020.
Bila shaka kufaulu kwenu ni matokeo ya juhudi katika masomo yenu, nidhamu na kuzingatia kile mlichofundishwa na walimu wenu, huku mkizingatia mwenendo wa maadili mema wakati wote mliokuwa shuleni.
Aidha tunachukua nafasi hii kuwapongeza walimu wote wa shule zetu mliofanya kazi kubwa ya kutoa mafunzo sahihi kwa vijana hawa, kiasi kwamba yale mliowafunza wanafunzi waliyaelewa na yaliwakaa barabara katika akili zao na hatimaye leo wameweza kufaulu. Hongereni sana.
Tunafahamu kwamba wale wote waliofaulu, watapata nafasi za kuchaguiwa kujiunga na kidato cha tano kwa mwaka 2021. Hivyo kwa sasa wanapaswa kuwa katika maandalizi ya kujiunga na daraja hilo la elimu ya juu ya sekondari.
Lakini wengine watapata nafasi za kujiunga na vyuo vya fani mbalimbali, ili kupata ujuzi na utaalam utakaowawezesha kumudu harakati za maisha yao baada ya kumaliza masomo yao.
Kwa wale ambao hatafanikiwa kupata nafasi za kuendelea na elimu ya juu ya sekondari, wasikate tamaa, maana maisha ni kuhangaika. Wanaweza kupata maajaaliwa yao kwa kushiriki katika kozi za fani mbalimbali na wakafanikiwa kufikia ndoto zao na kumudu maisha yao na hata kufikia matarajio yao.
Tutoe tu ushauri kwa serikali kwamba, pamoja na kazi nzuri ya kujenga shule za Msingi na zile za sekondari za Kata, lakini pia kuna haja ya kuongeza shule za kidato cha tano na sita ili kukabiliana na ongezeko la ufaulu kwa vijana wetu kila mwaka.
Hatutaraji kuona wanafunzi wengi wanaofaulu wanakosa nafasi za kuendekelea na masomo yao ya sekondari “A” level, kwa kuwa tu shule hazitoshelezi kupokea idadi yao.
Tunayasema haya kwa kuwa hivi karibuni tu, tumeona ongezeko la wanaofaulu darasa la saba kiasi cha shule zetu za serikali zilizopo kushindwa kuwapokea wanafunzi wote wanaofaulu, kwa kuwa miundo mbinu haikuruhusu kuwapokea wote. Leo tunalazimika kujenga madarasa ya haraka haraka, huku watoto wakisubiri majumbani ili yakamilike na waweze kuanza kidato cha kwanza.
Tunadhani kwamba kwa kadiri kasi ya ufaulu inavyoongezeka, ni muhimu na serikali ikaweka mipango yake kulingana na kasi hiyo, kwa kujenga madarasa na kuweka miundo mbinu yake mapema, au kujenga shule mpya ili kuondoa adha ya kuwasubirisha mafunzo wanafunzi hawa waliofanya vizuri.
Serikali imefanya uamuzi mzuri wa kutoa elimu bure, kwa hiyo inahitajika juhudi na mikakati madhubuti katika kutimiza azma hii ya Mheshimiwa Rais Magufuli.
Tunawatakia kila la heri waliofaulu katika masomo yao ya elimu ya juu. Wasiobahatika kufaulu, nao wana nafasi kwa kila mmoja kufikia malengo yake kwa njia watakayojaaliwa na Allah (SW) muhimu iwe ni njia halali.
Wazazi wa watoto ambao hawakubahatika kuchaguliwa kuendelea na shule au vyuo, wasije kukataa tamaa juu ya hatma ya maisha watoto wao.
Bado wana nafasi ya kufaulu maisha yao kwa njia mbadala kwa uwezo wake Allah (SW). La muhimu ni juhudi na kutokata tamaa.