Na Shaban Rajab

Mwalimu Khatibu Mavura amefariki. Kwa hakika si wengi wanamjua Khatibu Mavura, lakini huyu ni katika watu muhimu katika jamii ya Waislamu Tanzania.

Mavura amemaliza maisha yake yote katika kuutumikia Uislamu toka akiwa katika Jumuiya ya Kiislamu ya Ustawi wa Waislamu Afrika Mashariki-East Africa Muslim Welfare Society (EAMWS) na kisha Bakwata. Amefariki dunia majira ya saa 2:00 asubuhi siku ya Jumatatu Desemba 31 na kuzikwa katika makaburi ya Ukonga jijini Dar es Salaa Januari 1 mwaka huu.

Sheikh Mavura ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Elimu katika Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) hadi alipostaafu mwaka 2017, amefariki dunia nyumbani kwake Ukonga jijini Dar es Salaam baada ya kuugua kwa muda mfupi.

“Siku ya Jumatatu Desemba 31 mwaka jana 2018 aliamka na kuswali na baadae akapata kikombe chake cha uji kama ilivyo kawaida yake, baadae akiwa kapumzika kibarazani akisubiri kwenda kufundisha darsa lake pale nyumbani la Kiarabu, mara akasema anajisikia vibaya, pumzi zimebana na moyo unaenda mbio, akajilaza katika madrasa  yake, hapo ndio ikawa safari yake imewadia”. Alieleza Bw. Abdulbasat Mavura ambaye ni mwanae mkubwa.

Akielezea historia yake kwa ufupi, Bw. Abdulbasat alisema baba yake alizaliwa Masumbeni, Ugweno Wilayani Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro mwaka 1936. Baadae alipata elimu yake ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la nne katika shule ya msingi Masumbeni akiwa na umri wa miaka 11.

Alifaulu na kujiunga na masomo ya darasa la tano hadi darasa la nane katika shule ya Kati (Middle School) Shighatini Seminari iliyokuwa kati ya Ugweno na Usangi na kuhitimu mwaka 1957.

Aidha, kipindi hicho alisoma katika Chuo cha Ufundi Mbale kilichopo Kifula, Ugweno. Baadae alikwenda Zanzibar kwa masomo zaidi ambapo alijunga na chuo cha Ualimu  ambapo alipata mafunzo ya dini ya Kiislamu na Ufundi.

Ilikuwa mwaka 1964 ambapo Mwalimu Khatib Mavura alihitimu katika chuo cha Kiislamu Muslim Academy Zanzibar na baadae akajijunga na Chuo cha Baytul Ras kwa masomo zaidi. Baadae alikumbana na kikwazo, nacho si kingine bali ni vuguvugu la Mapinduzi ya Zanzibar, ambalo lilimlazimu kurejea Dar es Salaam.

Hata hivyo, Ofisa wa Wizara ya Elimu Zanzibar, Ramadhani Mshui, alimtunuku Cheti cha Ualimu, kilichomruhusu kufundisha dini ya Kiislamu katika shule za sekondari.

Baada ya kurejea masomoni Zanzibar, Mwalimu Mavura alikwenda Kigoma kuungana na mkewe ambaye alipelekwa huko kufanya kazi kama Afisa katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii. Sheikh Mavura pamoja na kuungana na mkewe Kigoma, lakini kusudio lake kubwa lilikuwa ni kutafuta uwezekano wa uhamisho kwa mkewe na kumrejesha Dar es Salaam, ambako alipanga kuendelea zaidi na masomo.

Akiwa katika harakati za kumhamishia mkewe Dar es Salaam kikazi, alilipeleka suala hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati huo akiitwa Rajab Semvua (Mapwiyanga), ambaye naye alijadiliana na mwenzake wa Mkoa wa Kigoma aliyekuwa akiitwa Abdunur Suleiman.

Baadae Semvua aliandika barua kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii wakati huo akiwa ni Bw. David Cleopa Msuya, akimuomba kumhamisha mke wa Mavura na wakati huo huo kuomba ajira kwa Bw. Mavura mwenyewe katika Wizara yake.

Bw. Suleiman alifafanua kwamba kwa kuzingatia kwamba Bw. Mavura ni mjuzi wa huduma za kijamii na kidini, basi anaweza kupatiwa nafasi kulingana na taaluma yake.

Hatimaye mkewe alipata uhamisho, lakini Bw. Mavura hakupata ajira Wizarani hapo. Kuanzia hapo Bw. Mavura alijikita katika kutoa elimu ya dini na alianza kufundisha dini katika shule za sekondari.  Bw. Abdunur Suleyman alimuagiza Mavura kwa Mzee Omar Muhaji ambaye alimsaidia kujiunga na taasisi ya East Africa Muslim Welfare Society (EAMWS) kama mkufunzi katika shule ya sekondari ya Dar es Salaam, lakini Ofisi yake kuu ikiwa katika Shule ya Msingi Jamiatul Islamiyya, Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam.

Mwalimu Mavura alitumia muda wake mwingi hapo kwenda kufundisha elimu ya dini ya Kiislamu katika shule mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Mwaka 1968 EAMWS ilitangazwa na serikali kuwa sio jumuia halali badala yake ikaundwa BAKWATA kuchukua nafasi yake na kurithi mali zote za Jumuia hiyo, na hapo Mwalimu Mavura akaingia ndani ya BAKWATA.

Kwa mara ya kwanza Mwalimu Mavura alikutana na Sheikh Malik mwaka 1966 na moja ya jukumu lake miongoni mwa majukumu aliyokuwa nayo, ni kuzungukia shule za sekondari za jiji la Dar es Salaam na vyuo kukusanya taarifa juu ya ratiba za mafunzo ya dini ya Kiislamu.

Akiwa shule ya sekondari Tambaza wakati  akizungumza na Mkuu wa Shule, aligundua mzee mmoja mwenye asili ya Kihindi alikuwa akimtizama kwa makini. Alipomalizana na Mkuu wa Shule, mara yule Mzee alikuja karibu yake na kumsindikiza Mwalimu Mavura. Alijitambulisha kuwa yeye anaitwa Mohammed Hussein Malik na anafundisha somo la hesabu shuleni hapo na anatokea Pakistan.

Wakati akimsindikiza Mwalimu Mavura, alimuomba kwa kusema kuwa kama anaweza kuungana naye katika kazi ile ya kufuatilia masomo ya dini katika shule za sekondari jijini. Mwalimu Mavura mara moja alimjibu bila kusita kuwa anaweza kufanya hivyo, ila kwa sharti moja tu, nalo ni ofisi yake ifahamu ushiriki wake.

Sekretarieti ya BAKWATA iliyokuwa ikiongozwa na Sheikh Mohammed Ally ilikubali ombi la mwalimu Malik bila kusita. Sheikh Mohammed Hussein Malik kabla ya kuja Tanzania mwaka 1964, alikuwa akifundisha visiwa vya Mauritius. Kituo chake cha kwanza baada ya kuja Tanzania kilikuwa ni Shule ya sekondari  Morogoro iliyokuwa ikimilikiwa na Aga Khan (sasa ni shule ya serikali).

Baada ya muda, aliletwa jijini  Dar es Salaam kufundisha somo la hesabu katika shule ya sekondari ya Aga Khan ambayo sasa ni shule ya sekondari Tambaza ambayo nayo ilikuwa ikimilikiwa na Jumuia ya Aga Khan kabla ya shule kuanza kutaifishwa. Alikuwa akiishi katika jumba za ghorofa za Aga Khan jirani na shule ya sekondari ya Mzizima.

Kutokana na fursa hiyo iliyoanzia kwa Sheikh Mavura, Sheikh Malik aliweza kutoa mihadhara mbalimbali wakati anafundisha Tambaza. Aliweza kuzuru shule nyingine za sekondari na vyuo na Misikiti. Pia alitoa mihadhara ya kitaaluma nyumbani kwa Sheikh Said Musa mtaa wa Swahili Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Mavura aliwahi kueleza kuwa mhadhara wa kwanza kutolewa na Sheikh Malik na kufanywa katika uwanja vya wazi  ulikuwa ule uliofanyika katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe (Sasa ni Chuo Kikuu cha Ualimu Chang’ombe-DUCE).

Mhadhara huu ulifanyika kupitia ombi la wanafunzi wa chuo hicho kumfuata mwalimu Mavura na kuhitaji mhadhara huo. Viongozi wa wanafunzi wa chuo hicho wakati huo walikuwa ni Hashim Semkuya, Rashid Mallya, Saad Fundi na Juma Rashid. Kauli mbiu ya Mhadhara huo wa kwanza  ilikuwa “Ufunuo wa Dini na Sayansi”.

Mhadhara huo ulikuwa wazi kwa watu wa dini zote ambapo baadae wanafunzi waliokuwa na majadiliano, walisitisha mjadala wao na kutoa nafasi kumsikiliza Sheikh Malik na ulikuwa na vipindi vya kuuliza maswali na kujibiwa. Tangu wakati huo, Sheikh Malik alipanga kuanzisha program nzima ya Da’awa na kufikia ngazi zote katika jamii ya Waislamu.

Sheikh Malik alikuwa akimudu vyema lugha za Kiarabu, Urdu, Kiingereza, Fursi na Kiswahili kwa uchache, na alijitahidi sana kuhakikisha kwamba kunakuwa na mawasiliano yanayomhakikishia kuwa ujumbe wake unawafikia walengwa.

Ukiacha kuendesha mihadhara ya ndani na ya wazi na kufundisha hesabu, Jukumu lake la kwanza katika kuujenga Uislamu lilikuwa ni kutoa mafunzo kwa makundi ya vijana nje na ndani ya shule hasa pale ambako Kiingereza kinaeleweka vyema.

Miongoni mwa vijana maarufu walioivishwa na Sheikh Malik walikuwa ni Khatib Mavura, Burhani Mtengwa, Hamza Soko, Yusuf Ngirini, Saad Fundi, Hashim Semkuya, Musa Mdidi, Swaleh Shaqsy, Mohammed Kassim, Ahmed Ulotu, Hassan Mshinda, Ally Kilima na wengine wengi.

Mchango wa Mwalimu Malik ulidhaminiwa kwa kiasi kikubwa na Sheikh Muhammad Ally Al Buhry (Wakati huo akiwa Katibu Mkuu wa BAKWATA) na Jumuia maarufu ya vijana wa Kiislamu iliyojulikana kama WARSHA YA WAANDISHI WA KIISLAMU iliundwa.

WARSHA waliandika vitabu na makabrasha kwa lugha ya Kiswahili yaliyotokana na mihadhara ya mwalimu Malik. Kitabu cha kwanza kilitafsiriwa kutoka katika kijitabu “Islamiat” kilichoandikwa na Sheikh Malik.

WARSHA ilikuja kuwa maarufu sana na ilienea kama moto wa nyika na hili liliwashangaza wengi. Ni kutokana na athari hizi za Sheikh Malik na makundi ya vijana wake, baadae kulileta vuguvugu kubwa la kuanzishwa shule za sekondari za Kiislamu nchini ambazo baadhi yake sasa ni vyuo.

Kulianzishwa program za mafunzo ya ziada (tuition) ili kuwasaidia wanafunzi wa shule za sekondari za Kiislamu ili kupata matokeo bora katika mitihani yao ya mwisho na kuweza kuleta changamoto katika ngazi za juu za masomo na ajira.

Hizi zilikuwa jitihada zilizohitimisha mbinu za kufifisha maendeleo ya Waislamu. Wasomi wengi wa Kiislamu sasa wanafaidi kwa njia moja au nyingine matunda ya jitihada hizi.

Kama tulivyoeleza hapo awali, Sheikh Malik maeneo yake ya utekelezaji yalikuwa ni katika shule, vyuo na Misikitini. Alikuwa akitoa mihadhara katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Dar es Salaam, Chuo cha Ualimu Chang’ombe Dar es Salaam na katika shule za sekondari kama Minaki, Kibaha, Pugu, Ruvu, Tambaza, Azania, Forodhani, Kisutu na Jangawani. Miongoni mwa Misikiti aliyokuwa akitoa Darsa ni Sunni, Madina, Kipata, Bungoni, Majumba Sita, Shadhilliy, Kimamba, Mwembe Chai, Magomeni Makuti na Mtambani. Katika darsa za Msikitini, siku zote alisaidiwa na wanafunzi wake, mmoja wapo alikuwa akimsaidia kutafsiri lugha kutoka Kiingereza kwenda katika Kiswahili.

Hata hivyo kazi kubwa ya tafsiri ya mihadhara yake ilifanywa kwa kina na mwalimu Mavura, Mtengwa, Mdidi, Shaqsy, Yasin Kachechele au Kilima na sehemu kubwa ya mada kuu katika Misikiti ilikuwa ni tafsiri na ufasiri wa thematic kutoka katika Quran.

Sheikh Malik alitambua kuwa kulihitajika nyenzo za kusambaza harakati. Ndipo hapo alihitaji kundi jingine la kusukuma mbele harakati. Hapo akafadhili Masjid QUBA wakati anakaribia kuondoka nchini baada ya kudaiwa na serikali kuwa ni mhamiaji haramu .

Mwalimu Mavura alikuwa karibu sana na Sheikh Malik. Ndipo alipomshauri kwamba ratiba yake imebana sana, kwanini siku ya Jumapili asipumzike? Alimjibu Mavura, “Khatib, kama unapumzika hapa duniani, utakwenda kufanya nini katika kaburini?”

Alianza kutoa Makala zake katika kipindi maarufu cha wiki enzi hizo katika Redio Tanzania-External Service. Kipindi kiliitwa “The Islamic Quarter” kilichorushwa kila Ijumaa kuanzia saa 2:45 hadi saa 9:00 usiku.

Sheikh Malik aliondoka nchini mwaka 1982 baada ya kutakiwa na serikali  kuondoka ndani ya saa 24.

Tangu hapo, Mwalimu Khatib Mavura aliendelea na harakati zake za kupigania maendeleo ya Waislamu akiwa ndani ya BAKWATA, akisimamia Idara ya Dini na elimu kwa ujumla hadi alipostaafu kazi rasmi mwaka juzi.

Sheikh Khatib Mavura amefariki lakini kamwe hatasaulika kwa mchango wake uliowezesha kutambulika Prof. Maliki, ambaye alikuja kuleta chachu na vuguvugu la kuamka umma wa Kiislamu nchini hususan katika elimu.

Mwalimu Mavura alitumia muda wake mwingi kufundisha elimu ya dini ya Kiislamu katika shule mbalimbali za jiji la Dar es Salaam.

Mwaka 1982 alikwenda kusoma diploma huko Sudan na kurejea mwaka 1985 na kuwa Mkuu wa Kitengo cha Idara ya Dini BAKWATA.

Miongoni mwa wanafunzi wake ni pamoja na Prof. Juma Mikidadi, ambaye pamoja na wenzake wengine alimfundisha akiwa shule ya sekondari ya Azania.

Akiongea na An nuur, Sheikh Hamisi Mataka, amesema Almarhum Sheikh Mavura ni mmoja kati ya wanaharakati wa Kiislamu walioingia katika utendaji wa Bakwata baada ya kuvunjwa kwa iliyokuwa Jumuiya ya Waislamu ya Afrika Mashariki (EAMWS).

Amesema, tokea kipindi hicho amekuwa akiitumikia Idara ya Elimu mpaka alipostaafu, miaka miwili iliyopita.

Mwalimu Mavura amefariki akiwa na umri wa miaka 82 na ameacha wajane watatu na watoto 17.

 

Inaalillaah wainaa illaihir Raaj’uun