Na Salmin Juma, Zanzibar

Wananchi wa Shehia ya Chaani Masingini wilaya ya Kaskazini “A” Unguja wamesema wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama baada ya kuanza ujenzi wa barabara iliyotoka Kwanyanya hadi Mkokotoni.

Wananchi hao wameamua kupaza sauti baada ya kufikiwa na mradi wa kukuza uwajibikaji Zanzibar- PAZA wenye lengo la kuwaamsha juu kufuatilia haki zao za msingi pamoja na kupelekea uwajibikaji kwa watendaji wa sekta tofauti.

Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari wananchi hao walisema ingawa kinachofanyika ni jambo zuri la kukuza mawasiliano, lakini ujenzi huo umepelekea baadhi ya miundo mbinu ya maji kukatwa hatimae huduma hiyo kukosekana katika baadhi ya maeneo.

Mmoja miongoni mwa wananchi wa shehia hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Mwajuma Ali Ussi alisema, ujenzi wa barabara hiyo umeharibu miundombinu ya maji wala hayapatikani na walipoulizia kwa kampuni inayotengeneza barabara walijibiwa kuwa, kampuni imeshalipa kwa Mamlaka ya Maji, ZAWA ili wananchi warejeshewe huduma ya maji kama kawaida.

“Mradi wa Kukuza uwajibikaji wa PAZA umetusaidia sana, maana hatukuweza kukaa kimya, tulifatilia ili tujue linaamulika vipi jambo hili”, alisema mama huyo.

Alisema, ZAWA walijibiwa kuwa , kama wanahitaji huduma ya maji watoe pesa ndipo waungiwe tena wakati awali huduma ilikuwepo kijijini kwao.

Zuwena Ngwali Mohamed ambae ni mjumbe wa Sheha wa Shehia ya Chaani Masingini aliungana na wananchi wenzake kwa kusema, huduma hiyo inapatikana katika maeneo mengine lakini kwa wakaazi wa Masingini ya Kati bado hawajapata huduma hiyo kutokana na ujenzi wa barabara unaendelea hivi sasa.

Naye Sheha wa Shehia ya Chaani Masingini Sheha Hamdu Hussein alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusu kadhia hiyo alithibitisha kwa kusema, huduma ya maji imekua shida kupatikana kwa baadhi ya wakaazi wa maeneo yaliyopitiwa na ujenzi wa barabara na ameshalifikisha katika mamlaka husika suala hilo.

“Tatizo hili kweli lipo , kuna miundombinu imeharibika na ninachojua kampuni imeshalipa umeme waliyoharibikiwa lakini kuhusu ZAWA sijui”, alisema Sheha huyo.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Zanzibar ZAWA Zahor Suleiman alisema, wanachokifahamu ni kuwa kila walio athirika na kukosekana kwa maji kufuatia ujenzi wa barabara hiyo wamesha warejeshea huduma, hivyo kama kuna waliyokua bado waende afisini kwao kuripoti na watawafikishia huduma hiyo.

“Maji tumeshayarudisha katika eneo husika lakini hatumpelekei mtu hadi nyumbani kwake, hivyo kama mtu anataka kuungia hivyo basi alipie Tsh 50,000.”

Wananchi wa Shehia hiyo wameamua kupaza sauti zao kufuatia mradi wa kukuza uwajibikaji Zanzibar (Promoting Accountability of Zanzibar – PAZA ) unaowafanya kujitambua pamoja na kupigia mbio haki zao.

Mradi huo umekuja kwa lengo la kukuza uwajibikaji katika majukumu hatimae kufikia mendeleao katika eneo husika na unaendeshwa na chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania –TAMWA upande wa Zanzibar , Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar – WAHAMAZA na NGENARECO – PEMBA chini ya mradi wa kuziwezesha asasi za kiraia Zanzibar, ZANSASP, ambapo mradio huo upo ukingoni kumalizika na unatarajiwa mwezi wa Pili mwaka 2019

 

Latest News

Most Read