Na Bint Ally Ahmed

Wanawake mkoani Njombe wamehimizwa kuhusu vazi la stara, unyonyeshaji watoto na kushiriki uchumi.

Akiwasilisha mada ya stara, Bi. Mwanaisha Sudi alirejea aya kadhaa za Qur’an zinazoonyesha heshima ya mavazi kwa mwanadamu na stara kwa mwanamke kiimani na kijamii.

 

Kwa upande wa kiimani alisema kuwa stara ni ibada, hivyo akawakumbusha kina mama wajisitiri ili kutafuta radhi za Allah (S. W.T).

Akielezea stara kwa upande wa kijamii, aliainisha kwamba moja ya alama kuu ya kumtofautisha mtu mwenye akili timamu na isiyokuwa timamu ni mavazi, kisha ndiyo zinafuata kauli na matendo yake.

 

Aidha amesema kuwa mwanamke ndio mwalimu mkuu wa familia na jamii nzima, hivyo aliwahimiza kina mama kuwa walimu bora kwa familia zao.

 

Akinukuu aya katika suratul Ah zab, aya 59,

"Ewe Nabii waambie wake zako na mabinti zako na wake wa waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe.

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu.”

 

Naye Bi. Mwaituni Hussein, aliwasilisha mada ya unyonyeshaji huku akinukuu Qur'an tukufu Suratul Baqara aya 233 isemayo,"Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anaetaka kutimiza kunyonyesha ...".

 

Aliwakumbusha kina mama kuwa kunyonyesha siyo jambo la hiyari ya mtu bali ni amri kutoka kwa Allah (s.wt), hivyo basi atakayeacha kumnyonyesha mwanae bila sababu ya kisheria afahamu kuwa anamdhulumu mwanae na dhulma ni haramu.

 

Bi. Mwaituni aligusia faida zinazopatikana kwa mama na mtoto kwa kunyonyesha ikiwemo mama kuwa na siha njema na upendo kwa mwanae, na mtoto kukua kimwili na kiakili pamoja na kuwa na upendo kwa wazazi wake, ndugu zake, binadamu wenzake na viumbe kwa ujumla.

 

Kwa Upande wake Bi. Beshuu Kasim, wakati akiwasilisha mada ya ‘Uchumi’ alirejea Suratul Israa, aya ya 35 inayosema, "Na timizeni kipimo mpimapo, na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni wema kwenu na khatimaye ndiyo bora".

 

 

Alisema vipimo vikifanywa sawa kwa uadilifu, basi kila mtu atavutika kufanya biashara na wewe na hivyo uchumi wako kukuwa kwa kasi, kinyume na yule anayefanya ghushi. Lakini pia alisema huko kupima kwa usawa ni amri ya Allah hivyo ni ibada.

 

Aliwahimiza wanawake kujipamba na sifa ya uadilifu katika shughuli zao za kila siku.

 

Kabla ya hapo shughuli hiyo ilizinduliwa na Amirat wa TAMSYA, Njombe   ambaye ndiye aliekuwa mgeni rasmi, Ukht. Maryam Suleiman, mbaye aliwataka kina mama wa Kiislamu kulipenda na kulithamini vazi la Hijabu, kwani hiyo ni katika nembo za Uislamu na kwamba hijabu inamtofautisha na asiye Muislamu.

 

“Mwanamke ukivaa nguo ya stara heshima yako inaongezeka zaidi, kwanini sasa tusilipende vazi hili linalotupa heshima?” alihoji Ukht. Mariyam Suleiman.