Akizungumza katika mahojiano maalumu na ya televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon, Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Bashar al-Ja'afari, amesema ugaidi unatumiwa kama nyenzo na wale wanaoufadhili na kuuhami kifedha

Aidha Al-Jaafari ameukosoa vikali muungano wa kijeshi unaoongozwa na Marekani kwa kuwahamisha magaidi wa Daesh, huku ukiwa unadai kwamba unazishambulia ngome za kundi hilo la ukufurishaji.

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa, vyombo vya serikali ya Algeria vimewakamata mamia ya magaidi kwenye mpaka wake wa pamoja na Niger na baada ya kuwahoji ikabainika kuwa, magaidi hao wanatoka eneo la Aleppo katika ardhi ya Syria na kuongeza kuwa, inashangaza na inapasa kujua ni nani aliyewasafirisha magaidi hao kutoka Syria hadi kwenye mpaka wa pamoja wa Algeria na Niger.

Al-Jaafari alisisitiza kuwa, Marekani na Uturuki zinajua ni wapi alipo Abu Bakr al-Baghdadi.

Balozi huyo amelaani pia muamala uliofanywa hivi karibuni baina ya Marekani na genge la kigaidi la (ISIS), ambapo Washington ilipokea "makumi ya tani za dhahabu" na kwa upande wake ikawaruhusu magaidi wa kundi hilo kuondoka katika mkoa wa Dayr al-Zawr nchini Syria.

Bashar al-Jaafari alibainisha kuwa, Magharibi inafanya kila njia "kuurefusha mgogoro nchini Syria" na kwamba serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump, inataka kutumia "uwekezaji wa mtaji wa ugaidi" ili kufanikisha ajenda inayofuatilia katika eneo la Mashariki ya Kati. Parstoday.