Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI), imetangaza kuwa Saudi Arabia ndiyo nchi inayoongoza kwa ununuaji silaha duniani.

Kituo cha habari cha Middle East Eye chenye makao yake mjini London, Uingereza kimeripoti kuwa takwimu za kila mwaka za taasisi ya SIPRI zinaonyesha kuwa, ununuaji silaha unaofanywa na Saudi Arabia umeongezeka kwa asilimia 192 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2014 hadi 2018.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nazo pia ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa ununuzi wa silaha duniani.

Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm imebainisha katika ripoti yake kuwa, Marekani na nchi za Ulaya zimeiuzia Saudia ndege za kivita, magari ya deraya pamoja na zana nyingine za kijeshi kwa ajili ya kutumia katika vita vilivyoanzishwa na utawala wa Riyadh dhidi ya Yemen.

Ripoti ya SIPRI imefafanua kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Saudi Arabia imenunua kutoka Marekani na Uingereza ndege 94 za kivita zilizosheheni makombora ya cruise pamoja na silaha nyingine zinazoongozwa kutokea mbali.

Na katika kipindi cha miaka mitano ijayo, inatazamiwa kununua ndege 98 za kivita, vifaru 83 pamoja na mifumo ya ulinzi ya makombora kutoka Marekani, magari 737 ya kijeshi kutoka Canada, manowari tano kutoka Uhispania na makombora ya balestiki ya masafa mafupi kutoka Ukraine.

Inaelezwa kuwa misaada na uungaji mkono wa kijeshi unaotolewa na nchi za Magharibi kwa mwaka wa nne sasa kwa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen, umekuwa ukisababisha mauaji na maafa makubwa kwa raia wasio na ulinzi wa nchi hiyo.Parstoday.