Na Bint Ally Ahmed

Ona Fahari kuvaa Hijab-Lemu

Ni utambulisho, hifadhi ya mwanamke

*Kongamano la ‘Pink Hijab’ lafana Dar

Kongamano la Hijab lililoandaliwa na Taasisi ya Pink Hijab na kufanyika katika ukumbi wa Hellenic Jijini Dar es Salaam, limefana kwa kuhudhuriwa na Waislamu zaidi ya 1000 kutoka kona zote za Jiji.

Akizungumza na waandishi wa habari, mgeni rasmi katika kongamano hilo kutoka Nigeria, Mariam Lemu, alisema amefurahishwa kuona Waislamu wa Tanzania wana mwamko mkubwa wa kupenda kujistiri kupitia vazi la hijab, na kubainisha kuwa vazi hilo linalinda heshima na utu wa mwanamke.

Bi Lemu alisema, Nigeria hususani eneo la Kaskazini ambako yeye anatoka, Waislamu wengi wana fursa ya kuvaa vazi hilo bila bughudha na wanajifaharisha nalo.

Lakini kwa upande wa Kusini bado kuna changamoto kadhaa ya uvaaji wa nguo hiyo za stara na sababu kubwa ikiwa ni idadi kubwa ya waumini wa Kikristo.

“Ninataka kutoa wito hapa kwa wanawake wenzangu, wasione haya hata kidogo kuvaa vazi la hijab, huu ni utambulisho wa mwanamke.”

“Ukijithamini nao watakuthamini, jifaharishe kwa sababu ni nguo ambayo ukiivaa inalinda heshma na utu wako.” Alisema Bi. Mariam.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki katika kongamano hilo kutoka Jumuiya ya Wanafunzi na Vijana wa Kiislamu Nchini (TAMSYA), Amirati Neema Mandalanga, alitoa wito kwa wazazi kuwazoesha watoto wao vazi la hijab ili waanze kulipenda wakiwa wadogo.

Alisema, juhudi zaidi zinahitajika kwa pande zote wakiwamo walimu, kuhakikisha wanafunzi wanavaa vazi hilo muhimu na kulifanya kuwa sehemu ya maisha yao.

Naye Bi. Mariam Mangula kutoka Jukwaa la Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi jijini Dar es Salaam (JUWADA), aliipongeza Taasisi ya Pink Hijab kwa kuendelea kuandaa makongamano kama hayo, kwani ni muhimu na yanawafanya wanawake kuendelea kujifunza na kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa vazi hilo.

Bi. Mangula alisema, si kawaida kuweza kuwakutanisha wanawake wengi kiasi kile, lakini kupitia Pinki Hijab wengi wamejitokeza na kupata fursa ya kuongeza ufahamu wao.

Katika Kongamano hilo pia walikuwepo wanawake wajasiliamali ambao waliweza kuelezea umuhimu wa kujiajiri.

Miongoni mwao ni taasisi ya Marashi ya Unguja, ambao walisema kongamano kama hilo ni fursa lakini pia ni uwanja wa kukumbushana juu ya umuhimu wa stara ya mwanamke.

Kwa upande wake mlezi wa watoto shuleni, Mzee Mikidadi Khalfani, aliwashauri wazazi kujenga tabia ya kujitathmini ni kwa kiwango gani wanachangia kuwajengea watoto wao wa kike tabia njema ikiwa ni pamoja na kujistiri.

Kongamano hilo lilienda sambamba na Siku ya Kuvaa Hijab Duniani, huku Taasisi ya Pink Hijab ikiteuliwa kuwa balozi wa siku hiyo hapa nchini.