Na Bakari Mwakangwale

WAISLAMU wametakiwa kufuta dhana kuwa Bakwata na Baraza Kuu ni “vyama” pinzani.

Wito huo umetolewa na Amir wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania,

Sheikh Mussa Kundecha akiongea na Waislamu waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Baraza hilo, uliofanyika Jumamosi ya wiki iliyopita katika Ukumbi wa City Garden, Jijini Dar es Salaam.

Amir Kundecha amesema, Mabaraza hayo makubwa ya Waislamu nchini sio pinzani, bali yaweza kuwa mabaraza shindani yenye lengo la kuupeleka mbele Uislamu na kuwaletea maendeleo Waislamu.

“Kwa dhana ya wengi ya kudhania kuwa Mabaraza yetu makubwa mawili, Bakwata na Baraza Kuu ni mabaraza pinzani hiyo ni dhana potofu.

Waislamu tuifute fikran hiyo, haya ni Mabaraza shindani ili kweza kuwapa huduma inayofaa Waislamu.” Amesema Amir Kundecha.

Amir Kundecha alisema ikumbukwe kwamba kama Waislamu hawataweza kufanya mashirikiano, upo uwezekano wa kukosa kunufaika na keki za kitaifa, kwani akasema kwa Wakristo linapokuja suala la kitaifa hawaangalii Taasisi na Jumuia zao, bali huwa kitu kimoja na kufanikisha jambo lao.

Alisema, wakati wa uongozi wa Mufti Shaaban Simba wa Bakwata, palikuwa na ushirikiano wa kutosha baina ya viongozi, na kwa Mufti aliyepo sasa (Sheikh Abubakar Zubeir) ushirikiano umekuwa mkubwa zaidi.

Alisema, ushirikiano huo umepelekea kufanya ziara (safari) za nchi za nje kama wawakilishi wa Waislamu kutoka Tanzania na huko walitambuliwa kama ujumbe wa Waislamu kutoka Tanzania na si ujumbe wa Bwakata na Baraza Kuu.

“Namimi nikuombeni, huko katika shughuli zenu za Kiislamu msiwe wapinzani ila muwe washindani kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Waislamu pawe na hali ya kushirikiana ikibidi kuunganisha nguvu kwa kila jambo linalohusu Waislamu ili lililokusudiwa lifanikiwe pasiwe na hali ya kukwamishana kwa mtazamo wa mabaraza yenu.” Amesema Amir Kundecha.

Akifafanua Amir Kundecha, alisema wanachama wa Baraza Kuu sio Muislamu mmoja mmoja bali ni Jumuiya na Taasisi za Kiislamu na kwa Bakwata wanachama wake ni kila Muislamu aliyetamka Shahada.

Hivyo akasema, kwa mseto huo haoni kama hapo kuna upinzani na kwamba kuimarisha mashirikiano baina ya Waislamu kupitia mabaraza hayo ni jambo muhimu ambalo litaweza kuharakisha maendeleo ya Waislamu na nchi kwa ujumla.

Aidha, Amir Kundecha alisema ipo haja sasa kwa Waislamu kubadilisha mfumo katika kuratibu na kuyaendea mambo yao kwani inawezekana mfumo uliopo sasa unawakwamisha.

Alisema, kama kiongozi wa Baraza Kuu, anakiri kuwa yapo mapungufu kadhaa ya kiutendaji hivyo wapo tayari kupokea maoni na ushauri kutoka kwa kila Muislamu ili kuliwezesha Baraza kuwa katika muundo mzuri wa kuwatumikia Waislamu kwa ufanisi zaidi.

“Ni jambo jema kuwa na njia mbadala itakayoweza kuturatibu katika muundo wa kukidhi haja zetu, kwani pamoja na uwepo wa Bakwata na Baraza Kuu, ni muhimu mabaraza hayo kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Waislamu kwa kasi zaidi.” Amesema Amir Kundecha.

Awali akifungua Mkutano huo ambao ni wa kumi na tano tokea kuundwa kwa Baraza hilo mwaka 1992, Amir Kundecha, alihoji ni wakati gani Waislamu wanaweza kuwa na msimamo wa pamoja na kuweka tofauti zao pembeni.

Katika hotuba yake hiyo ya ufunguzi Amir Kundecha, alisema hoja ya kuwa na mashirikiano baina ya Waislamu haina mjadada kwani ndio maamrisho ya Allah (sw) na Mitume wake, juu ya kushikamana kwa pamoja.