Msafiri pia amepewa tahfifu katika swala kwa kupewa ruhusa ya kukusanya swala mbili za faradhi na kuziswali kwa wakati mmoja kama tunavyojifunza kutokana na Hadithi zifuatazo:

Ibn Abbas (r.a) amehadithia kuwa Mtume wa Allah alikuwa akichanganya Dhuhur na Asr wakati akitoka safarini, pia alichanganya Magharibi na Isha. (Al-bukhari).

Mua’dhi bin Jabal (r.a) amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) alikuwa katika vita vya Tabuk. Jua lilipopinduka kidogo aliswali Dhuhuri pamoja na Asr. Kama alianza safari kabla ya jua kupinduka (kabla ya wakati wa dhuhur) aliakhirisha Dhuhur mpaka wakati wa Asr.

Hali kadhalika kwa swala ya Magharibi, jua lilipotua kabla hajaanza safari, aliswali Magharibi pamoja na Isha, na kama alianza kusafiri kabla ya jua kutua; aliakhirisha Magharibi mpaka wakati wa Isha na kuziswali pamoja. (Abu Daud, Tirmidh).

Kutokana na Hadithi hizi msafiri anaruhusiwa kuchanganya Adhuhuri na Asr kuziswali wakati mmoja, pia anaruhusiwa kuswali Magharibi na Isha

kwa wakati mmoja, ila swala ya Alfajiri haichanganyiki na swala yoyote na wakati wake ni ule ule wa kawaida.

Kuna aina mbili za mkusanyo na zote zinajuzu. Aina ya kwanza huitwa Jam-'u Taqdym. Katika aina hii unazikusanya swala mbili katika wakati wa swala ya mwanzo. Yaani kwa kuswali Adhuhuri na Asr pamoja katika wakati wa Adhuhuri kwa adhana moja na Iqama mbili. Hivyo hivyo utaswali Magharibi na Isha katika wakati wa Magharibi.

Aina ya pili huitwa Jam'u Ta-akhir. Katika aina hii unazikusanya swala mbili katika wakati wa swala inayofuatia. Yaani msafiri ataswali Adhuhuri na Asr pamoja katika wakati wa Al-'Asr kwa adhana moja na Iqama mbili. Hali kadhalika ataswali Magharibi na Isha kwa pamoja katika wakati wa Isha.

Namna ya kuswali swala za mkusanyo wa Adhuhuri na al-'Asr, ukishaadhini na kukimu utaanza kuswali rakaa mbili za Adhuhuri. Baada ya kutoa salaam utasimama na kukimu tena kisha utaswali rakaa mbili za Al-'Asr.

Kama unaswali Jam-'u Ta-akhir ya mkusanyo wa Magharibi na Isha, baada ya kuadhini na kukimu, utaanza kuswali rakaa tatu za Magharibi kama

kawaida. Baada ya kutoa salaam utasimama na kukimu tena na kisha utaswali rakaa mbili za Isha.

Kama tunavyojifunza katika Hadithi uamuzi wa kukusanya swala katika wakati wa swala ya mwanzo (Jam-'u Taqdym) au katika wakati wa swala inayofuatia (Jam'uta-Akhr) utategemeana na hali ya safari kama tunavyojifunza katika Hadithi ifuatayo:-

Abdullah ibn Abbas (r.a) amesema: “Mwenendo wa Mtume (s.a.w) ulikuwa kabla hajaanza safari akiona kuwa jua limepindukia (wakati wa Adhuhuri umeingia) alikuwa akiswali Adhuhuri na al-Asr na kisha huanza safari yake vinginevyo akiona, kuwa bado jua halijapinduka, basi huianza safari yake na mbele ya safari akiswali Adhuhuri na al-’Asr katika wakati wa Al ’Asr.

Hivyo hivyo akiona jua limeshazama alikuwa akiswali Magharibi na Isha wakati huo wa Magharibi kabla ya kuanza safari, na kama jua bado halijazama, basi huanza safari yake kisha huswali Magharibi na Isha wakati wa Isha. (Ahmad).

Nne, msafiri pia amefanyiwa wepesi wa kusimamisha swala, kwa kuruhusiwa kuswali huku anatembea au anaendelea na safari juu ya kipando au chombo anachosafiria. Ruhusa hii tunaipata katika aya zifuatazo:-Hifadhini swala na swala ya kati na kati. Na simameni kwa unyenyekevu katika kumuabudu Mwenyezi Mungu. Na kama mkiwa na khofu (basi swalini) na hali ya kuwa mnakwenda kwa miguu au mmepanda vipando. Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu (swalini) kama alivyokufunzeni yale mliyokuwa hamyajui”. (2:238-239).

Pia Hadithi ifuatayo inatufahamisha juu ya swala ya Mtume(s.a.w) juu ya kipando: Ibn Umar (r.a) ameeleza kuwa Mtume wa Allah alipokuwa safarini alikuwa akiswali Isha juu ya ngamia katika upande wowote ule atakapoelekea, akiswali kwa ishara wakati wa usiku ila kwa swala za faradhi na alikuwa akiswali witri juu ya ngamia anayetembea. (Albukhari, Muslim).

Ilivyo ni kwamba msafiri anaruhusiwa kuswali juu ya kipando huku anaendelea na safari. Namna ya kutekeleza swala hii ni kwamba, baada ya msafiri kutawadha au kutayammamu, ikiwa anasafiri kwa mguu au kwa mnyama na anaona hofu ya kuvamiwa na maadui au wanyama, atafunga swala akiwa ameelekea Qibla, kisha ataendelea na swala huku anatembea akiwa ameelekea kule anakokwenda. Ataswali kwa ishara tu.

Ikiwa msafiri anasafiri, kwa chombo kama vile gari, meli, ndege n.k, atatawadha au atatayammamu, kisha atakaa na kuelekea popote pale kiti chake kinavyomruhusu, kisha ataadhini na kukimu na kuswali kwa ishara kama vile kuinamisha kichwa na kuinua katika kuashiria visimamo, rukuu, itidali, sijda na vikao. Inapendekezwa kuwa mtu ainamishe kichwa zaidi kwa sijda kuliko vile anavyoinamisha katika kuashiria rukuu.

KUSIMAMISHA SWALA VITANI

Muislamu haruhusiwi kuswali swala ya faradhi nje ya wakati wake hata akiwa katika vita vya kupigania Dini ya Allah (s.w). Bali Allah (s.w) ametuhafifishia swala, tukiwa vitani na kutuelekeza tuswali ifuatavyo:

“Na unapokuwa pamoja nao (Waislamu katika vita) ukawaswalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe (waswali) na washike silaha zao. Na watakapomaliza sijda zao basi na wende nyuma yenu (kulinda); na lile kundi jingine ambalo halijaswali liswali pamoja nawe, nao washike hadhari yao na silaha zao (humo ndani ya

swala, maana) wale waliokufuru wanataka mghafilike na silaha zenu na vitu vyenu, ili wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mnaona ugonjwa, kuondoa silaha zenu, na mshike hadhari yenu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu itakayowadhalilisha”. (4:102).

Namna ya kusimamisha swala katika uwanja wa vita kutokana na maelekezo ya aya hii ni kwamba, askari wagawanyike katika makundi mawili ambayo yataswalishwa na Imamu mmoja na swala itafupishwa kama ilivyo katika swala ya safari.

Kundi moja litaanza kuswali na Imamu wakiwa na silaha zao na kundi jingine litabaki katika ulinzi. Imamu ataswali rakaa moja na hili kundi la kwanza na watakaponyanyuka kuswali rakaa ya pili, Imamu atabakia pale akiendelea kusoma Qur’an na kila mtu katika wale wanaomfuata, atamaliza upesi upesi rakaa ya pili na baada ya kutoa salaam watarudi nyuma upesi kuchukua nafasi za ulinzi.

Baada ya kundi la pili kupokelewa nafasi zao, watakwenda kujiunga na Imamu ambaye bado anaendelea na rakaa yake ya pili. Wote

watakapojiunga na swala, Imamu atamalizia swala yake ya rakaa mbili.

Baada ya Imamu kutoa salaam kila mmoja katika wale wanaomfuata atasimama na kumalizia rakaa yake ya pili.

Aya hii ya (4:102) inayotuelekeza namna ya kuswali tukiwa katika vita vya kupigania Dini ya Allah (s.w) inafuatiwa na aya inayotoa amri ya kusimamisha swala kwa nyakati zake kama tunavyojifunza:

Mwishapo kuswali, kuweni mnamkumbuka Mwenyezi Mungu - msimamapo na mkaapo na (mlalapo) ubavu. Na mtakapopata amani, basi simamisheni swala (kama kawaida). Kwa hakika swala kwa Waislamu ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu. (4:103).

Hebu fikiri: Kama askari wa Allah (s.w) aliyejitoa muhanga kwa mali yake, hali yake na nafsi yake kwa ajili ya kupigania dini ya Allah (s.w) hakuruhusiwa kuiacha swala au kuiswali nje ya wakati wake, je wewe uliyezama kwenye shughuli nyingine ndio utegemee kusamehewa kwa kupitisha wakati wa swala ukaswali wakati unapojiona kuwa huna shughuli!

Aya hii inatufahamisha kwa uwazi kuwa swala tano zimefaradhishwa kwetu pamoja na nyakati zake makhsusi.

Tukiondoa ruhusa tulizopewa kuziswali swala kidharura tunapokuwa vitani, na tukiondoa udhuru wa kusahau na kupitiwa na usingizi, hapana ruhusa yoyote iliyotolewa katika Qur’an au Hadithi inayokubalika kuswali kadha kama wengi wafanyavyo. Je, mtindo huu wa kuswali kadha tunauiga kwa nani? Je, huku sio kupuuza swala? Kama tunapuuza swala kwa nini tusitarajie kupata ghadhabu za Allah (s.w) badala ya kujidanganya na kujipa matumaini ya kupata malipo mema kutoka kwake kutokana na kadha zetu hizo. Ujira wa wapuuzaji wa swala unabainishwa katika Qur’an: “Basi, adhabu itawathibitikia wanao swali. Ambao wanapuuza swala zao. (107:4-5).