Na Bint Ally Ahmed

Nyasaka Sekondari yapiga hatua kidato cha nne 2020

 

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kiislamu Nyasaka Islamic secondary School iliyoko Jijini Mwanza, Mwalimu Said Rajab Mangi, ametoa wito kwa wazazi  wa Kiislamu kuwapeleka watoto wao katika shule hiyo na kamwe hawatojutia uamuzi wao huo.

Mwalimu Mangi alisema hayo wakati akiongea na mwandishi kwa njia ya simu kutoka Jijini Mwanza, ambapo amewaomba wazazi kumpa dhamana ya malezi na kutoa elimu bora kwa watoto wao shuleni hapo.

 Alisema wazazi wanatakiwa kufanya uchaguzi sahihi wa wapi wanawapeleka watoto wao hasa katika kipindi hiki cha kutafuta shule za kidato cha kwanza na kidato cha tano, ili wasikosee katika chaguzi na hatimaye wakapoteza dira na ndoto za watoto wao za kutokufikia malengo.

Mwalimu Mangi amesema kuwa anachukua dhamana ya shule yake kuwapa elimu sahihi wanafunzi watakao jiunga na shule, na kuwaanda kuwa Makhalifa wa Mwenyezi Mungu ili kupata kizazi kitakachokuwa na viongozi walio na khofu ya Mungu katika kuitumikia dini na jamii kwa ujumla.

Shule ya Kiislamu ya Sekondari ya Nyasaka iliyopo jijini Mwanza imepiga hatua katika kuyaendea mafanikio ya wanafunzi waliofanya matihani wa kidato cha nne 2020, ikilinganisha na miaka mitano iliyopita.

Mwaka jana wanafunzi 14 wamepata daraja la kwanza huku daraja la pili wakiwa 40.

Kulingana na matokeo yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa hivi karibuni, idadi ya wanafunzi waliopata daraja la tatu ni 49 ambapo waliopata daraja la nne wakiwa 32.

Aidha idadi ya wanafunzi wa kidato cha nne shuleni hapo mwaka 2020 ilikuwa wanafunzi 209 wakati mwaka 2019 walikuwa wanafunzi 187.

Urari wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne katika shule hiyo tangu mwaka 2018 unaonyesha kuwa wanafunzi waliopata daraja la kwanza (DIV-I) mwaka huo walikuwa 9, DIV II walikuwa wanafunzi 59, DIV III walikuwa wanafunzi 86 na DIV IV 44. Mwaka huo hakukuwa na DIV O ambapo jumla ya wanafunzi ilikuwa 198.

Mwaka 2019 DIV I walikuwa wanafunzi 8, DIV II wanafunzi 36, DIV III wanafunzi 57, DIV IV wanafunzi 48. Hakukuwa na DIV 0 ambapo jumla ya wanafunzi ilikuwa 149.

Mwaka 2020 DIV I wamepata wanafunzi 14, DIV II wanafunzi 40 , DIV III wanafunzi 49, DIV IV wanafunzi 32, huku kukiwa hakuna mwanafunzi aliyepata DIV 0 na jumla ya wanafunzi ilikuwa 135.