Na Bint Ally Ahmed

Islamic Education Panel ni jopo  la wataalamu lililoundwa rasmi mwaka 2006, lengo kuu likiwa ni kusimamia na kuratibu ufundishaji wa Elimu ya Dini ya Kiislamu katika mfumo wa elimu nchini. Na hiyo ni kuanzia Shule  za Awali hadi Vyuo Vikuu.

Akieleza historia fupi ya Islamic Education Panel, Mwenyekiti wa jopo hilo Sheikh Mohamed Kassim amesema kuwa, awali Wizara ya Elimu Tanzania Bara, iliweka wazi  kuwa haitashughulikia taaluma ya dini, bali imewaachia wana dini wenyewe  kuchukua jukumu hilo. Na kwamba kazi pekee ya Wizara itakuwa ya kutahini masomo ya Dini kupitia Baraza la Mitihani Tanzania, baada ya kuombwa kufanya hivyo na wanadini.

Awali kabla ya kuundwa kwa Jopo hili, Taasisi ya Islamic Propagation Centre (IPC) iliandaa mihutasari ya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa shule za Msingi, Sekondari (‘O’ level na ‘A’ level) na kuanza kuandika vitabu vya kiada kwa lengo la kutoa taaluma ya elimu ya Dini ya Kiislamu kuendana na mfumo wa elimu nchini.

Kazi ya uandishi wa vitabu vya kiada vya kidato cha I-IV ilianza kwa kuandika Juzuu 24 za Elimu ya Kiislamu kwa Posta (EKP) zilizolandana na muhtasari wa Elimu ya Dini ya Kiislamu (‘O’ level) kisha zikafuatiwa na uandishi wa vitabu 8 vya ‘Islamic Studies’ vilizolandana na muhtasari wa Islamic Knowledge, ‘A’ level.

Ilipofika mwaka 1996 iligundulika kuwa pamoja na mitihani ya Elimu ya Dini ya Kiislamu (‘O’ level) kufanywa na wanafunzi Waislamu wa Tanzania Bara na Visiwani, palikuwa na muhtasari tofauti tofauti (wa BAKWATA, IPC na Wizara ya Elimu Zanzibar). Hapo ndio ikaonekana haja ya kukaa pampoja na kuja na muhutasari mmoja. Kwa hiyo, kwa kushirikiana na Mratibu wa Masomo haya ya Dini katika Baraza la Mitihani Tanzania, paliundwa jopo (Panel) la dharura la kuandaa muhtasari mmoja kwa ‘O’ level, ‘A’ level na Diploma. Jopo hili lililokutana Chuo cha Kiislamu Zanzibar likiwa na wajumbe wawakilishi wafuatao:

Mwarabu Said Mponda-Baraza la Mitihani Tanzania, Mohammed R. Kassim-IPC, Masoud A. Masiku-IPC, Mtengwa B. Mtengwa-IPC (na Munadhamat Da’awah), Khatib I. Mavura-BAKWATA na Iddi Khatib-BAKWATA. Wengine walikuwa Hilal O. Mohammed-Wizara ya Elimu Zanzibar, Mwalimu Basha-Wizara ya Elimu Zanzibar, Abdurazaq Othman-Chuo cha Kiislamu Zanzibar, Fadhili Pandu- Chuo cha Kiislamu Zanzibar, Abdalla Hadhar-Chuo cha Kiislamu Zanzibar na Abdalla Habibu Ally Kombo- Chuo cha Kiislamu Zanzibar. 

Jopo hili baada ya warsha ya takriban siku tatu ndani ya mwezi wa Ramadhani 1996, lilifanikiwa kwa uwezo wa Allah (sw) kukamilisha muhtasari wa pamoja wa Elimu ya Dini ya Kiislamu (‘O’ level) na kuidhinisha mihutasari ya Islamic Knowledge ya ‘A’ level na Diploma iliyoandaliwa na IPC, itumike baada ya kuhaririwa na kutolewa chini ya Islamic Education Panel.

Ilipofika mwezi Machi 1996 Jopo lilikaa tena kwa wiki tatu katika Chuo cha  Ualimu Morogoro kuandaa miswada ya vitabu vya kiada kulingana na muhutasari wa Elimu ya Dini ya Kiislamu kidato cho I-IV. Jukumu la kuhariri na kuchapisha vitabu hivi ilikabidhiwa IPC. Pia jukumu la kuandaa miswada ya vitabu vya ‘A’ Level na Diploma na  kuvichapisha iliachiwa IPC. na kazi  ya Jopo lile la dharura ikaishia pale.

Sheikh Mohamed Ramadhani Kassim alieleza kuwa, pamoja na jitihada hizo, IPC iliona kuwa, kwa kuwa suala la Elimu nchini ni suala linalohusu jamii yote ya Waislamu, hapana budi kuwa na jopo la kudumu la wataalamu wa Kiislamu wenye weledi na watendaji watakaowakilisha Tanzania Bara na Visiwani.

Katika kutekeleza wazo hili, Novemba 12, 2006, IPC iliitisha kikao rasmi kwa ajili ya kuunda Jopo la Kudumu la Islamic Education Panel, litakalo simamia kikamilifu Elimu ya Dini ya Kiislamu katika mfumo wa elimu nchini.

Wajumbe wa jopo waliochaguliwa walikuwa: Mwenyekiti Mohamed R. Kassim-Ubungo, Mwalimu Shafii Hussein (Katibu)-Ubungo, Prof. Hamza M. Njozi (Mjumbe)-Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (wakati huo), Mwalimu Said O. Nsigarila (Mjumbe)-Kirinjiko Islamic Centre, Dk. Ahmed Mohamed Ame (Mjumbe)-Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwalimu Masoud A. Masiku (Mjumbe)-Ubungo Islamic School, Mwalimu Othman Kalulu (Mjumbe)-Elimu ya Kiislamu kwa Posta (EKP), Mwalimu Bakari Kombo (Mjumbe)-Chuo cha Kiislamu Zanzibar, Mwalimu Suleimani Hemed (Mjumbe)-Chuo cha Kiislamu Zanzibar, Mwalimu Ally Nassor Hamad (Mjumbe)-Ukaguzi Mitaala Zanzibar, Mwalimu Haji Mwevura Haji (Mujumbe)-Chuo Kikuu Zanzibar.

Majukumu ya Islamic Education Panel yalianishwa kama ifuatavyo:

 1. Kusimamia na kuratibu ufundishaji wa Elimu ya Dini ya Kislaamu na Lugha ya Kiarabu katika mfumo wa elimu nchini kuanzia ngazi za shule za awali hadi vyuo vikuu.
 2. Kuanzisha, kusimamia ma kuratibu madrasa za watoto kwa kufuata mtaala.
 3. Kusimamia na kuratibu darsa za watu  wazima na Elimu ya Kiislamu  kwa posta (EKP).
 4. Kusimamia na kuratibu malezi ya vijana mitaani na mashuleni.
 5. Kukuza mitaala na kuandika mihutasari ya Elimu ya Dini ya Kiislamu na Lugha ya Kiarabu sanjari na kuandika vitabu vya kiada na ziada kwa ajili ya ngazi mbali mbali za elimu nchini.
 6. Kuendesha kitaifa mtihani wa Elimu ya Dini ya Kiislamu wa kuhitimu elimu ya msingi nchini kwa kibali cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
 7. Kufuatilia na kuzuia upotoshwaji wa mafundisho ya dini ya Kiislamu kwa muktadha wa  Quraan na Sunnah.

Mwaka 2007 Kikao cha Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, kiliitambua rasmi Islamic Education Panel na majukumu yake pamoja na kulifanya jopo hili la wataalam liwe chini ya Jumuia na Taasisi za Kiislamu (T), ili liwe sauti ya Waislamu wote na taasisi zote za Kiislamu juu ya suala la usimamizi na uratibu wa ufundishaji wa somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu katika mfumo wa elimu Tanzania Bara na Visiwani.

Kikao cha Jumuia na Taasisi za Kiislamu (T) chini ya Mwenyekiti wake Amir Mussa Yusufu Kundecha, kilipitisha Azimio la kuiongezea nguvu Islamic Education Panel kwa kuongeza wajumbe na kuitambulisha rasmi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Wajumbe wa Islamic Education Panel waliorasimishwa  Wizarani mwaka 2007 ni hawa wafuatao:

Mohamed R. Kassim, Shafii Hussein, Prof. Hamza Njozi, Dk. Mohammed A. Ame, Bakar Kombo, Dk. Haji Mwevura, Said O. Nsigarila na Suleiman Hemed. Wengine ni Mohammed Ali Mohammed, Ali Nassor Hamad, Dk. Hamdun Suleyman, Khatib Mavura, Abubakar Musa, Mwinyikombo Ayub, Masoud A. Masiku, Suleiman Lenga, Ally S. Kilima, Mohammed Issa, Mohammed Said, Musa Kundecha na Imran Kimaro.

Sheikh Kassim alibainisha kwamba katika kuchagua wajumbe wa Jopo hili, sifa zifuatazo zilizingatiwa:

 1. Mjumbe awe na ujuzi wa kutosha juu ya somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu/ Islamic Knowledge au Lugha ya Kiarabu.
 2. Awe amesomea Ualimu katika ngazi ya stashahada au Zaidi.
 3. Awe na uzoefu wa kufundisha somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu/ Islamic Knowledge kwa muda usiopungua miaka mitano au kuandika vitabu vya somo hili kwa ajili ya kufundishia shuleni.
 4. Awe ni mchapa kazi mwenye moyo wa kujituma na kijitolea.

Islamic Education Panel katika kutekeleza majukmu yake,  imefanya kazi nyingi ikiwemo kutengeneza na kusimamia mihutasari ya somo  la Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa shule za Awali, Msingi, Sekondari    (“O” na  “A” level)  Ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada.

Lakini pia Panel imeandaa vitabu vya kiada vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa kidato cha I-IV. Aidha imeandaa vitabu vya kiada vya shule za msingi, Darasa la I-VII na vitabu vya kiada vya (‘A’ Level (Volume 1-3).

Pia imeandaa moduli ya mbinu za kufundishia Elimu ya Dini ya Kiislamu Ualimu ngazi ya Stashahada. Kuandika vitabu vya kiada na ziada vya Lugha ya Kiarabu.

Kuendelea kufuatilia na kukagua ufundishaji wa mafunzo ya Dini ya Kiislamu katika shule na vyuo, halikadhalika kuandika na kutafsiri vitabu vya Maarifa ya Uislamu kwa ngazi zote za elimu.

Baada ya juhudi kubwa iliyofanywa na viongozi wa IEP, Wizara ya Elimu alitoa kibali  June 2011 cha kuruhusu mtihani wa Darasa la Saba kufanyika kitaifa.

Sheikh Kassim anabainisha kwamba mpaka sasa Alhamdulillah, kuna mafanikio kiasi kwani usomaji wa somo la Dini ya Kiislamu umekuwa mkubwa na mwamko umeongezeka sana. Hivi sasa hadi vijijini somo hilo linafundishwa na kufanyiwa mtihani wa taifa.

Aidha, Islamic Education Panel katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,  imeweka Waratibu wa Elimu wa Mikoa na Maamiri wa Kanda ili kusaidiana katika kusimamia utekelezaji wa majukumu haya.

Changamoto  kubwa inayoikabili Islamic Education Panel  katika kutekeleza majukumu  ni ukosefu wa rasilimali watu na rasilimali fedha.

Tangu mwanzo ilitarajiwa uwezeshaji na utekelezaji wa majukumu haya utokane na Waislamu wenyewe kupitia Jumuiya na Taasisi zao halikadhalika watu binafsi. Ni kutokana na ukweli na mtazamo huo, Mwenyekiti anatoa wito kwa Waislamu binafsi, Jumuiya na Taasisi za Kiislamu kutoa michango na sadaka zao ili kuwezesha Islamic Education Panel kutekeleza majukumu yake.