NOVEMBA ya tarehe 23, 2020, yaani Jumatatu ijayo, wanafunzi wanaosoma elimu ya sekondari kidato cha nne 2020 nchini, watakuwa wanafanya mitihani yao ya mwisho ya kuhitimu.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA),jumla ya wanafunzi 490,103 wanategemewa kufanya mitihani hiyo ambapo watahiniwa wa shule ni 448,164 na watahiniwa wa kujitegemea ni 41,939.

Tunachukua fursa hii kuwatakia kila la heri vijana wetu hao katika mitihani yao.

Tuseme tu kwamba wale ambao walizingatia mafunzo shuleni, wakajiandaa vizuri, waliwasikiliza walimu wao kwa umakini na kuwaelewa, waliotumia muda wao wa ziada kujisomea na kufanya mazoezi ya kuelewa kile walichofundishwa darasani, wakajengewa kujiamini, bila shaka kwa uwezo wake Manani watafaulu.

Lakini wale waliokwenda shule kutimiza wajibu, wakakosa nidhamu, watoro, wapenda starehe na wasiojali upotevu wa muda, walioendekeza ujana wa mambo kuiga bila kujali hatima yao itakuwaje, hao watakuwa na wakati mgumu sana katika mitihani hii.

Vijana wetu wanapaswa kutambua kuwa ufaulu wao una maana kubwa sana kwao, kwa wazazi wao na jamii kwa ujumla.

 

Elimu ndio ufunguo wa ufahamu, ujuzi, taaluma na maarifa. Elimu ni nyenzo muhimu ya kuyakabili maisha hapa duniani na hata kesho tutakaporejea kwa Mola wetu. Elimu ni hazina isiyopoteza thamani yake.

Tuwaase tu vijana wetu kwamba kipindi hiki wanapaswa kuwa makini zaidi kwa kila hatua ya jambo wanalolifanya, ili kuweza kufika siku ya mitihani na kuifanya salama.

Wazazi na walimu kwa upander wao kila mmoja kwa nafasi yake, wahakikishe wanaongeza umakini kwa vijana wao na kuwasimamia kwa karibu ili waweze kufanya mitihani wao vizuri na salama.

Kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake, wanafunzi hawa watafanya mitihani yao salama na wakiwa timamu na hatimaye kufaulu vizuri. Wakifanya vizuri sote tutafurahi na kupongezana.

Tunawatakiwa wanafunzi wote wa kidato cha nne mtihani mwema wa kumaliza elimu yao ya sekondari