Na Bakari Mwakangwale

Swala ya Jeneza kufanyika Mtambani

Mufti Zubeir ametoa kauli ya kulani mauwaji hayo Jumamosi ya wiki iliyopita ikiwa ni siku moja tu kupita tangu Waislamu hao wauwawe kwa kupigwa risasi wakiwa msikitini katika ibada ya Swala ya Ijumaa ya wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari BAKWATA, Tabu Kawambwa, Mufti Zuber, amelaani tukio hilo kwa niaba ya Waislamu wa Tanzania.

Amesema, mbali na tukio hilo la kusikitisha lakini pia Mufti Zubeir analaani vitendo vyote vya aina hiyo kufanyiwa wanadamu popote pale ulimwenguni kwani si katika vitendo vya kibinadamu bali ni vya kinyama.

Katika taarifa yake kupitia kwa Mkurugenzi wa Habari, Mufti Zubeir amesema amepokea kwa mstuko mkubwa tukio la kuuwawa Waislamu 49 katika Misikiti ya Al nour na Linwood (Al nour and Linwood Mosques).

“Ndugu zetu wameuawa wakiwa msikitini kwa ajili ya Swala ya Ijumaa, kwa niaba ya Waislamu wa Tanzania, ninalaani kitendo hicho na vitendo vyote vya aina hii kufanyiwa wanadamu popote pale ulimwenguni.”

“Ni matumaini yangu kwamba, wahusika wote watapatikana na kufikishwa katika mikono ya sheria ili sheria ifuate mkondo wake.” Amesema Mufti Zubeir.

Mufti Zubeir amesema, kwa ujumla Waislamu wa Tanzania, wanaungana na Waislamu wote ulimwenguni, kuwaombea dua waliouwawa na kuwaombea ndugu na jamaa wa marehemu hao Allah (s w) awape subra katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.

Aidha, Mufti Zubeir pia ametoa pole kwa Shirikisho la Waislamu nchini New Zealand (FIANZ) pamoja na Serikali ya New Zealand, kutokana na janga hilo kubwa lililowafika.

Kwa upande mwingine Mufti Zubeir, ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya New Zealand, kwa uhuru inaoutoa kwa Waislamu nchini humo na kuiomba kuhakikisha kuwa uhuru huo unalindwa pale unapotishiwa kwa matukio kama hayo ya kigaidi ili kuwawezesha Waislamu wa nchi hiyo kutekeleza ibada zao bila ya hofu wala wasiwasi.

Kwa upande mwingine Mufti Zubeir, amewataka Waislamu nchini kuwa watulivu na kuendelea kuthamini tunu ya amani na kuilinda kwa kila hali.

Wakati huo huo, mmoja wa wahanga aliyenusurika katika uvamizi huo amesema, amemsamehe aliyemuua mke wake, kupitia shambulio hilo la Kigaidi lililofanyika katika Mji wa Christchur, nchini New Zealand.

Baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa, vimemnukuu muhanga huyo Bw. Farid Ahmed (59) akisema mke wake Bi. Husna (44), pia ameuwawa katika shambulizi la Ijumaa ya Machi 15, 2019.

Bw. Ahmed amesema, marehemu Husna, kabla ya kupigwa risasi aliokoa wanawake na watoto wengi na baada ya kufanikiwa aliingia upande wa wanaume kwa nia ya kwenda kumuokoa yeye (Bw. Farid Ahmed) ambaye ni mlemavu wa miguu akitumia kiti cha walemavu.

“Mimi ni mlemavu tangu mwaka 1998, mke wangu alikuwa anakuja kuniokoa, alipofika mlangoni akapigwa risasi akaanguka, hata hivyo sikujua kama amekufa mpaka nilipoona picha yake miongoni mwa waliofariki katika tukio hilo.” Amesema Bw.Faridi, ambaye yeye na mkewe walihamia Newzealand mwaka 1990, wakitokea Bangladesh.

Amenukuliwa akisema kwamba, mfyatua risasi akiwa ndani ya Msikiti alikuwa anampiga Muislamu mmoja risasi mbili, tatu hata zaidi na ndiyo sababu wengine walipata mwanya wa kujiokoa.

“Mimi nilinusurika kwa kuwa yule mfyatua risari hakunilenga, mke wangu alikuwa anafanya bidii kubwa kuwaokoa watu alionyesha kujali kuokoa maisha ya watu na hakujali sana maisha yake ni ishara ya ubinadamu aliokuwa nao lakini sasa amefariki na sina namna zaidi ya kumsamehe muuaji. Amesema Bw. Farid.

Wakati huo huo, Waislamu Jijini Dar es Salaam, leo wanatarajia kuswali Swalat Jeneza ikifuatiwa na Dua maalum kwa ajili ya Waislamu waliouwawa Msikitini katika Mji wa Christchur nchini New Zealand.

Swala hiyo itaswaliwa katika Msikiti maarufu wa Mtambani uliopo Kinondoni Jijini Dar es Salaam, ikiwa imeandaliwa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu (T), ambapo uchambuzi na taarifa za kina juu ya tukio hilo zitatolewa.

Katika tukio hilo imeripotiwa kuwa takriban Waislamu 49, wameuwawa na wengine kujeruhiwa baada ya kuvamiwa na kumiminiwa risasi katika Misikiti miwili tofauti (Al nour na Linwood) wakiwa katika ibada ya Swala ya Ijumaa ya wiki iliyopita.

 “Waislamu mnaombwa kuhudhuria katika Swala na Dua hiyo, Muislamu ndugu yake Muislamu na wala Uislamu hauna mipaka.”  Amesema mmoja wa waandalizi wa Swala hiyo.