Saudia yasitisha ibada ya Hija mwaka huu kwa wageni

Ni kwa sababu ya corona

Serikali ya Saudi Arabia imetangaza rasmi kwamba, wageni kutoka nchi za nje hawataruhuusiwa kutekeleza ibada ya Hija mwaka huu kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Hija na Umra ya Saudi Arabia imesema kuwa, Hija ya mwaka huu itashirikisha idadi ndogo ya mahujaji wa ndani ya nchi na wageni wachache wanaoishi nchini humo, kutokana na kuendelea maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 ambao haujapatiwa chanjo wala dawa.

Mwezi Machi mwaka huu Saudi Arabia pia ilisimamisha ibada ya Umra kwa Waislamu kutokana na maambukizi ya virusi vya corona. Wakati huo Wizara ya Hija na Umra iliwataka Waislamu kote duniani kusubiri kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kujitayarisha kwa ajili ya ibada ya Hija.

Uamuzi wa Saudi Arabia wa kusimamisha ibada ya Hija mwaka huu umewavunja moyo mamilioni ya Waislamu kote duniani, ambao huwekeza kwa miaka mingi kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo na kutimiza moja ya ibada muhimu za Kiislamu.

Mwaka jana karibu Waislamu milioni mbili na nusu walitekeleza ibada ya Hija huko Saudi Arabia.

Zaidi ya watu laki moja na sitini na moja elfu wameambukizwa virusi vya corona nchini Saudi Arabia na 1,307 miongoni mwao wameaga dunia.parstoday.