Jicho langu kwa Almarhum Sheikh Kilemile

Na Sheikh Mussa Kileo

MOJA katika murua mwema tuliofundishwa na Mtume wetu (S A W) ni kutaja wema wa maiti zetu, baada ya kutanguliza mkono wa taazia kwa wahusika wote wa msiba huu name nalazimika kuandika japo kwa uchache juu Sheikh Suleiman Kilimile, nikiwa mmoja wa wanafunzi wake, lakini pia uwepo wa usuhuba na muamala mwema  baina yetu.

Nilianza kumsikia Al-Marhum Sheikh Suleiman Kilemile, kupitia kipindi cha Dakika Tano cha Qur’an, tukufu cha Redio Tanzania katika miaka ya 1980. Kilikuwa ni kipindi kifupi mno  cha  dakika tano, wakati  wa saa kumi na moja alfajri.

Lakini ufupi wa kipindi hicho haikumzuiya Sheikh kwa uwezo mkubwa kuzitumia vyema dakika zile chache kufikisha ujumbe wenye ufafanuzi na kuele weka vyema  kwa hadhira yake.

Baada ya Sheikh kurudi masomoni Saudia (1978-1983) kutoka Chuo cha Ummu ul Quraa kilichopo Makkah, nami katika mwaka 1985, nikiwa mwana funzi ninayejifunza Uislamu, kwa kutaka kujiendeleza zaidi katika upande wa lugha ya kiarabu.

Ndipo niliamua kwenda kwa Almarhum Sheikh Kilemile, kuwa mwanafunzi wake katika fani ya swarfa na Alhamdullilah nilifaidika vya kutosha kwa elimu yake ambayo ni swadaka yake endelevu, Allah Taala aendelee kumlipa malipo makubwa.

Usuhuba wangu na Sheikh Kilemile uliimarika zaidi mwishoni mwa miaka ya 80’s (1987- 1989) pale Sheikh alipokuwa akiendesha darsa na khutba za kimwamko katika Msikiti wa Chihota, Tandika, Jijini Dar es Salaam, nami nikiwa mmoja wa wanafunzi wake katika darsa hizo na kuzidi kuchota katika kisima cha elimu yake.

Kwa kupitia darsa hizo kutokana na kipaji na elimu aliyokuwa nayo Sheikh Kilimile, aliweza kutuamsha makundi mengi ya vijana na wazee kwa kuwazindua juu ya dhulma zinazowakabili Waislamu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Waislamu kukosa  maamuzi.

Nakumbuka vyema namna Sheikh alivyoweza kufa fanua kwa ufasaha mkubwa kwamba Uislamu ndio kheri na ndio chaguo pekee la Allah (s.w) kwa wanaadamu.

Aidha, akafafanua namna Uislamu ulivyohimiza kusoma elimu nyengine akibainisha hayo kwa dalili mbali mbali za Qur’an na Sunna.

Sheikh Kilemile, katika darsa zile daima alitaka Waislamu tuwe tayari tuishi kwa mujibu wa Uislamu, kuutumikia na kujiandaa kumtumikia Allah (s.w) vilivyo na kuachana kabisa na kila kilicho kinyume na Uislamu.

Baaada ya Sheikh Kilemile, kutupika tukapikika katika darsa zake za kimuamko pale Chihota, naku mbuka baadhi ya vijana tukamfuata nyumbani kwake na kumueleza Sheikh, utayari wetu katika hali yoyote iwayo katika kuutumikia Uislamu, na kilichobaki tulimtaka Sheikh atueleze na atufundishe nini kinafuata.

Tulikuwa tunamueleza Sheikh,  kwamba vijana  tuko tayari kwa hali na mali kumtumikia Allah (s.w) na kufuata radhi zake na kuachana na  mifumo ya kibinadamu, nakumbuka tukawa tunamuuliza je Sheikh tufanye nini ? Al-Marhum Sheikh Kilemile, alikuwa daima akitutuliza kwa kutwambia tuendelee kuwa na subra huku tuendelee na jitihada za kujenga Shule ili vijana zaidi wa Kiislamu wazidi kupata  elimu.

Kabla ya safari yangu ya kwanza ya kimasomo (Oktoba,1989) nchini Sudan, sikuwacha mara kwa mara kumtembelea Sheikh nyumbani kwake tukijadili mambo mbali mbali hususan ya kuhuisha Umma wa Kiislamu.

Aidha, niliporudi safari yangu ya pili ya kimasomo Madina Islamic University (1992-1996) bado nilie ndelea kuwa karibu na Sheikh Kilemile, katika kadhia  mbali mbali  za kuunusuru Uislamu.

Hapana shaka, Sheikh wetu alitamani sana kuona siku Uislamu utakapotawala tena dunia na kuwakomboa wanaadamu toka katika viza vya ushirikina na utwaghuti kwa kuurejesha tena nuru na uadilifu wake, lakini qadhaa ya Mwenyezi Mungu imemfikia.

Kwa kukhitimisha, nikiri bayana kwamba Sheikh ameacha pengo kubwa kwa Umma wa Kiislamu, lakini pia amewacha alama na hazina adhimu katika upande wa kielimu na kuutumikia Uislamu.

 

 

 

 

 

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All