Na Shaaban Rajab

Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu alietukamilishia dini yetu na akatubariki sisi na kutuchagulia Uislamu kuwa ndiyo dini yetu.

Swala na salamu zimshukie mjumbe wake, aliyewalingania watu wamtii Mola wao na akawahadharisha dhidi ya kufanya maasi. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awabariki ahli zake, Maswahaba zake na wote waliofuata na wanaofuata nyayo zake hadi siku ya malipo.

Waislamu Oktoba 28 kuamikia 29 sawa na Rabiul Awal 11, 1442 wanaadhimisha Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa mbora wa viumbe Mtume Muhammad (SAW).

Wananchi wa maeneo mbalimbali duniani na hapa nchini wamepamba mitaa yao kwa maua, bendera na taa katika maadhimisho ya kuzaliwa Mtume wa na mbora wa viumbe Muhammad (SAW).

Ushiriki wa Waislamu katika sherehe ya maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume (SAW) unaweza kuwa moja ya eneo la kudhihirisha umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.

 

Kwa mujibu wa nukuu za Maulama wengi wa Kiislamu, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake Mtume, yaani Amina binti Wahab, alifariki dunia wakati mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita.

Inafahamika na wengi kwamba kumekuwepo na mivutano baina ya Waislamu juu ya kuwepo sherehe za Mazazi ya Mtume (SAW).

Lakini kwa kuzingatia umuhimu wa umoja, mshikamani na upendo baina ya Waislamu katika dini, si jambo jema hasa katika kipindi hiki ambacho kuna harakati kubwa ya wenye chuki na Uislamu ulimwenguni kuwafarakanisha Waislamu, kutumia maulid kuwa moja ya vigezo vya Waislamu kuhasimiana na kuchukiana baina yao.

Katika ulimwengu wa leo chuki dhidi ya Uislamu, au kwa jila la kiingereza Islamophobia, ni jambo linalopewa uzito na kuenezwa kwa namna maalumu katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Waislamu wenyewe wanaweza kuingia katika kmikumbo huo kwa kuhamismiana wao kwa wao kupitia Maulid.

Umoja wa Waislamu ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho kuna kila aina ya fitina na machafuko.

Ni muhimu maulid yakatumika kuonyesha umoja katika kuepusha chuki dhidi ya Uislamu. Wale wanaopenda kusherehekea mazazi ya Mtume, wafanye hivyo kwa kumfuata kwa vitendo yale aliyokuja nayo. Na wale wasiopenda, wasiwabughudhi wala kuwasimanga wale wanaopenda. Kwa kudhihirisha ustahimilivu huo baina ya Waislamu, propaganda chafu zinazoenezwa kwa madhumuni ya kuwadhihirishia walimwengu sura isiyokuwa sahihi kwamba Waislamu ni watu wasiokuwa kitu kimoja watakwama na kutahayari kwa kutofikia malengo yao.

Kwa kuzingatia propaganda hizo chafu, Umma wa Kiislamu unapasa kuimarisha umoja na mshikamano wake hata kwenye suala la Maulid, ili kuzima njama hizo za maadui.

Kwa mnasaba huu wa maadhimisho kwa lengo la kuenzi uzawa na maulidi ya Mtume Mtukufu, tunatoa mkono wa pongezi kwa Waislamu wote duniani ambao katika maadhimisho haya, wataashiria umuhimu wa kuwepo Umoja kati ya makundi yote ya Kiislamu na kuimarisha umoja na udugu miongoni mwao.

Neema ya uwepo na ujumbe wa Mtume (SAW) ilisababisha kuongoka mwanadamu na kufuata njia sahihi ya uokovu na bila shaka, ujumbe huo wa amani, uadilifu, heshima, maadili bora na kuwatetea wanyonge ni nguzo muhimu za mafundisho ya Kiislamu ya mtukufu huyo (saw), jambo ambalo bila shaka mwanadamu wa leo analihitajia zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Mtume (saw) alikuwa na angali ni 'Rehema kwa Walimwengu' na mbeba ujumbe wa amani na urafiki kwa wanadamu, madhehebu na dini zote za mbinguni.

Qur'ani Tukufu ambacho ni kitabu kinachobeba ujumbe wa uokovu kwa wanadamu wote inasema katika Aya ya 19 ya Surat Aal Imran: Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu. Kwa maana kuwa Uislamu ndio dini ya hakika na ukweli ambayo inaridhiwa na Mwenyezi Mungu.

Vile vile kwenye kitabu hiki kitakatifu kuna aya nyingi sana ambazo zinasisitiza kwamba Uislamu ni dini ya rehema na huruma na iliyo na maarifa muhimu na ya kina yanayomuokoa mwanadamu, na kumtaja Mtume kuwa mwokozi na mwongozaji wa jamii ya wanadamu.

Kwa msingi huo Mtume amearifishwa kuwa ruwaza na kiongozi mwema na mwenye huruma na upendo si kwa Waislamu pekee bali kwa wanadamu wote duniani. Kwa msingi huo Waislamu wanapasa kufuata mfano wa Mtume (saw) katika maisha yao yote na kuhuisha ujumbe na mafundisho yake, kwa sababu yeye ndiye nembo ya Uislamu na aliyepewa na Mwenyezi Mungu jukumu la kuarifisha dini hii yenye upendo na rehema kubwa kwa wanadamu.

Historia inathibitisha ukweli huu kwamba tangu zama za Nabii Adam (as) hadi wakati huu, fitina za wafuasi wa shetani dhidi ya ujumbe wa Uislamu ulioletwa na Mtume Muhammad (saw) zitaendelea kuwepo. Ushahidi uliopo unaonyesha wazi kwamba fitina hizo ambazo zimeongezeka katika zama zetu hizi na ambazo zinaenezwa kwa njia tofauti na mikono ya shetani kupitia wafuasi wake ambao tangu enzi za kale wamekuwa na chuki kubwa dhidi ya Uislamu wa Mtume Muhammad (saw), zinaenezwa kwa njia ambayo si rahisi kuitambua na kila siku zinaendelea kudhihiri kwa namna tofauti na mpya.

Leo chuki dhidi ya Uislamu zimefikia kilele cha propaganda za vyombo vya habari vya nchi za Magharibi n ahata kuwatumia Waislamu wenyewe kupitia madhehebu yao, ili kujaribu kuwaonyesha walimwengu kinyume na ukweli, kwamba Uislamu na Waislamu ni sawa na utumiaji mabavu na ugaidi. Kuanzishwa kwa makundi ya kigaidi na kuongezeka vitendo vya mauaji ya kutisha katika nchi za Kiislamu, kumezidisha woga na chuki dhidi ya Uislamu, vitendo ambavyo vinaenezwa na maadui kwa ajili ya kuwafanya watu wauogope Uislamu na Waislamu.

Fitna za Wamagharibi zimeeneza chuki na kuufanya Uislamu uogopwe duniani, ili kuzuia kuenea Uislamu halisi uliwemnguni. Ni wazi kuwa jinai zinazofanywa kwa jina la Uislamu zimeanzishwa kwa makusudi ili kudhamini maslahi ya Wamagharibi na wakoloni mamboleo, ambao katika kipindi chote cha historia wamekuwa na chuki na uadui mkubwa dhidi ya dini hii ya mbinguni.

Kwa kueneza fitina na chuki dhidi ya Uislamu halisi ulioletwa na Mtume Muhammad (saw), maadui hao daima wamekuwa wakifanya juhudi za kuwatenganisha na hatimaye kuwadhoofisha Waislamu na nchi za Kiislamu. Zinafanya hivyo ili zipate njia ya kuweza kuibua ghasia na hofu miongoni mwa nchi za Kiislamu, kuzigawa na hatimaye kuzidhibiti na kupora maliasili zao. Kwa masikitiko makubwa, baadhi ya nchi vibaraka za Kiislamu si tu kwamba zinayafadhili kwa hali na mali makundi hayo yanayoendelea kuharibu jina zuri la Uislamu, bali zenyewe zimeingia kwenye medani ya kutekeleza jinai za kutisha dhidi ya Umma wa Kiislamu kama tunavyoshuhudia jinai hizo zikitekelezwa wazi dhidi ya Waislamu masikini wa Yemen, Afghanistan, Libya, Syria, Iraq nk.

Aidha wimbi hilo la chuki dhidi ya Uislamu mbali na kusababisha dhana mbaya dhidi ya Waislamu, limehatarisha maisha ya Waislamu wengi wanaoishi katika nchi za Magharibi, na hasa wanawake wa Kiislamu wanaolengwa moja kwa moja kutokana na mavazi maalumu ya sitara wanayovaa.

Kwa msingi huo Waislamu wanalazimika kuishi na kufanya kazi zao kwa wasiwasi, jambo ambalo bila shaka huzidisha mashinikizo ya kiuchumi na matatizo mengine mengi katika familia za Kiislamu zinazoishi katika nchi hizo.

Kwa hiyo ni muhimu katika kusherehekea Mazazi ya Mtume (SAW) ni muhimu kudhihirisha umoja wetu badala ya utengano na kuhitiliafiana. Tuikiendela kuhitilafiana na kuchuikiana wenyewe kwa sababu ya Maulidi, bila shaka wimbi la chuki baina ya Waislamu na dhidi ya Uislamu halitachagua anayekubali Maulid au anayepinga, sote tunadhurika.

Maulidi yawe ni fursa kwa ajili ya Waislamu kuimarisha umoja na mshikamano wao kwa lengo la kukabiliana na na chuki kubwa dhidi yao na dini yao na wakati huohuo, kutoa fursa ya kuuarifisha Uislamu sahihi mbele ya walimwengu.

Umoja na mshikamano bila shaka ndio njia pekee ya kukabiliana na fitina pamoja na mifarakano inayoibuliwa na maadui wa Uislamu na Waislamu wanapasa kutembea kwa uangalifu na mwamko mkubwa katika njia hiyo. Kwa kutilia maanani mazingira nyeti ya hivi sasa, Waislamu wanatakiwa kuimarisha umoja wao kwa kushikamana na mambo ya pamoja na kujiepusha na yale yanayowatenganisha, ili kuweza kuzima njama za maadui dhidi yao. Ni wazi kuwa iwapo Waislamu wataimarisha umoja na mshikamano huu miongoni mwao, bila shaka adui hatakuwa tena na fursa ya kueneza chuki, fitina na mifarakano miongoni mwao.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 46 ya Suratul Anfal: Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.

Kwa hakika mifarakano na migawanyiko kati ya Waislamu huwadhoofisha kwa ndani na kuwakosesha heshima kwa nje na katika jamii. Hivyo Waislamu wanapasa kuwa watiifu na kuimarisha umoja miongoni mwao na iwapo kutatokea jambo lolote linalokwenda kinyume na matakwa yao, wanapasa kufanya juhudi za kulitatua na likiwa nje ya uwezo wao wasubiri ili Mwenyezi Mungu awanusuru kama alivyoahidi mwenyewe katika kitabu chake kitakatifu.

Ingawa Waislamu wanafuata madhehebu mbali mbali, lakini nukta ambazo wanaafikiana ni za kimsingi na ni nyingi kuliko zile ambazo wanahitilafiana.

Mwenyezi Mungu anaarifisha umoja kuwa sifa muhimu zaidi ya Waislamu kwa kusema katika Aya ya 92 ya Surat al-Anbiyaa: Kwa hakika huu Umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu. Kwa hivyo niabuduni Mimi. Ili kuimarisha umoja katika Umma wa Kiislamu, Mtume Mtukufu (saw) aliwaunganisha Waislamu wa Ansar na Muhajirin chini ya bendera ya umoja na udugu wa Kiislamu. Umoja huo daima ulikuwa ukiwakurubisha zaidi Waislamu hao na kuimarisha nguzo zao za kidini na kiimani na kuratibu miamala yao ya kijamii. Kupitia miongozo na mafundisho ya Mtume Mtukufu (saw) Waislamu hao waliweza kudhihirisha kwa njia ya kuvutia mno ushirikiano na udugu wao wa Kiislamu, udugu ambao unapaswa kutawala katika jamii ya Kiislamu na ya mwanadamu kwa ujumla.

Sherehe za Mazazi ya Mtume ziwe ni nembo ya umoja na mshikamano wa Waislamu wote, ni fursa kwa Waislamu kuweza kuondoa tofauti zao ndogondogo na kushikamana kikamilifu na Qur'ani Tukufu pamoja na mafundisho ya Nabii wa Rehema, Muhammad al-Mustafa (saw) ili kuweza kufikia umoja na mshikamano wa jamii ya Kiislamu.

Tunautakiwa umma mzima wa Kiislamu amani, usalama, utulivu, heshima, nguvu na afya njema. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuuondolea Umma huu fitina, mifarakano na shari ya matakfiri ambao wameuletea umma huu unaompenda Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kwa nyoyo zao zote.

Tunamwomba aweze kuufanya Umma huu kuwa Umma bora zaidi kuliko umma nyingine zote, kama alivyoahidi mwenyewe katika Qur'ani Tukufu, na kuufanya uweze kuwashinda maadui wake.

 

 

Latest News

Most Read