Shirika la ndege la Ethiopia liko mbioni kufungua kesi dhidi ya magazeti ya Marekani yaliyoandika habari za uongo kuhusiana na ajali ya ndege ya shirika hilo iliyosababisha vifo vya watu 157 hivi karibuni.

Kiongozi wa shirika hilo Tewolde Gebremariam, amesema magazeti ya Washington Post na New York Times, yaliandika habari za uongo kwa ajili ya kuharibu mwonekano wa shirika na nchi kwa ujumla.

Gabremariam alisema maandilizi yote kwa ajili ya kufungua kesi dhidi ya magazeti hayo yapo tayari.

Gebremariam alisema habari za uwongo zilizoandikwa na magazeti hayo zilikuwa na lengo la kusahaulisha watu kwamba Boeing 737 Max 8 ilipata ajali nyingine kabla ile ya ndege ya Ethiopian Airline.

New York Times, iliandika kwamba rubani wa ndege ya shirika hilo iliyopata ajali mwenye uzoefu wa saa karibu 8,000, Yared Getachew, hakuwa amepitia mafunzo ya kurusha ndege aina ya Boeing 737 Max 8. 

Washington Post kwa upande wao waliandika kwamba miaka mingi kabla hata ya ajali, kulikuwa na malalamiko katika Idara ya Anga ya Marekani kuhusiana uwezo mdogo wa marubani wawili katika kufuata taratibu za kiusalama.Parstoday.