Upinzani aliokumbana nao na mwisho kulitazama Jahazi la Uokozi alilolichonga kwa amri ya Mola wake. Nafanya hivi kwa kufuata maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur'an kwamba visa hivi anavyotusimulia ni kwa ajili ya kuchukua mfano na mafunzo ndani yake na kutuongoza.
Nabii Nuh (AS) ni katika mitume wa mwanzo na alifanya kazi kubwa ya kuwalingania watu wake kutaka kuabudiwa kwa Mungu Mmoja. Kazi hii ilimchukuwa zaidi ya miaka 900 kwa ustahamilivu mkubwa. Hata hivyo, Nabii Nuh hakukubalika na watu wake walio wengi. Kama ilivyo desturi za Mitume kukataliwa na jamaa zao wa karibu, Nabii Nuh alikataliwa hata na mwanawe wa kumzaa.
Sio tu kumkataa, jamaa zake hawa walishtadi pia katika kumfanyia vitimbi na maudhi ya kila aina. Hata pale alipoamrishwa na Mola wake atengeneze jahazi, basi waliamuwa kuligeuza choo cha kuweka haja zao kubwa. Mungu akawatia adabu kwa kuwapa ugonjwa mbaya ambao dawa yake ikawa ni kinyesi kile kile walichotia katika jahazi la Nabii Nuh. Wakawa wanakwenda kukichukuwa na kujipaka hadi jahazi likawa safi kabisa.
Mambo yalipofurutu ada, Mwenyezi Mungu Mtukufu Akamuamrisha Nuh apande kwenye jahazi lile yeye na wafuasi wake waliomuamini kama njia ya kuwatoa kwenye vitimbi hivi na kuwaacha wale wafanya vitimbi wakumbwe na gharika itokayo kwa Mola wao. Miongoni mwa waliogharikishwa ni mtoto wake mwenyewe, ambaye alikataa kupanda jahazi pamoja na baba yake.
Maalim Seif wa nyoyo za watu
Maalim Seif si Mtume na kattu hatuwezi kumfananisha hata kidogo na kazi za Mitume wa Mwenyezi Mungu. Huyu ni mwanaadamu wa kawaida tu. Hapokei wahyi na wala hakuna miujiza kutoka kwake. Lakini, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, nimekianza kisa cha Nabii Nuh kwani ndani yake muna mazingatio muhimu kwa muktadha wa makala hii.
Maalim Seif Sharif Hamad amekuwa kwenye siasa kwa zaidi ya nusu ya umri wake sasa. Ni kiongozi wa pekee aliyedumu kwa muda mrefu anayekubalika na watu wa rika lake na kizazi hata cha wajukuu zake.
Siku fulani katika mwezi wa Disemba mwaka 1987, Maalim Seif alikula kiapo mbele ya maelfu ya wananchi waliokusanyika kwenye uwanja wa Tibirinzi, kisiwani Pemba, baada ya mapokezi makubwa ya kihistoria ambayo yalifanyika kwanza Unguja na baadaye Pemba muda mfupi kabla ya kufukuzwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Siku hiyo ambayo imebakia kwenye historia milele, kiongozi huyu aliwaahidi Wazanzibari kuwa angelikuwa nao akiwa ndani ya serikali au nje ya serikali, ndani ya chama au nje ya chama. Wakati huo chama kilimaanisha CCM tu. Kiapo hiki kilimfungamanisha Maalim Seif na umma wa Wazanzibari na mpaka leo hii huwezi kumtenganisha na umma huo kwa namna yoyote ile.
Kazi kubwa aliyoifanya Maalim Seif ya kuwatumikia Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla imemjengea heshima ya kipekee. Ni kiongozi pekee aliyezitembelea karibu wilaya zote Tanzania Bara na Zanzibar kuonana na wananchi na kulala nao vijijini katika hali ambayo si viongozi wengi tulionao wanaoweza kufanya hivyo.
Hali hii ya mahusiano kati ya Maalim Seif na wananchi ndio iliyopelekea watu kumpenda, kumthamini na kumuamini. Anaishi katika mioyo ya wananchi walio wengi. Hata maadui zake wa kisiasa hawawezi kuipitisha siku bila ya kumuwaza mtu huyu.
Kosa la Maalim Seif
Ni imani hii ya wananchi kwa Maalim Seif ndiyo imekuwa kosa lake kubwa mbele ya maadui zake, ambao kila uchao wanahangaika kufikiria namna ya kummaliza