Na Nizar K Visram, Dar es Salaam

TAREHE 27 na 28 Februari mwaka huu Rais Donald Trump wa Marekani alikutana kwa mara ya pili na mkuu wa Korea Kaskazini (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea – DPRK) Kim Jong-Un. Mkutano huu wa kilele ulifanyikia mji mkuu wa Vietnam, Hanoi.

Ni mkutano wao wa pili baada ya kukutana Singapore mwaka jana na lengo ni kuzungumza jinsi ya kumaliza mgogoro wa nchi zao ambao umekuwa ukiendelea tangu mwaka 1953 wakati Marekani na marafiki zake walipoishambulia Korea na kusababisha mamilioni ya roho kupotea na Korea kugawanyika. Vita hivyo bado havijamalizika rasmi, bali vimesitishwa. Hivyo kisheria Marekani na DPRK zimekuwa katika vita virefu katika historia ya dunia.

Wakuu hawa walitakiwa wazungumze kwa muda wa siku mbili, lakini mambo yalikwenda kombo na Rais Trump akatoka mkutanoni kabla ya muda wake. Siku ya kwanza walikula pamoja chakula cha jioni na wakapata nafasi ya kuzungumza kidogo. Baada ya hapo Trump akaandika katika ukurasa wake wa Tweeter kuwa alikuwa na “mkutano mzuri sana” na Kim na alitegemea kuendelea siku iliyofuata. Alhamisi asubuhi wakapata kifungua kinywa na kuendelea na mazungumzo. Ndipo ikadhihirika kuwa jahazi lilikuwa linakwenda mrama. Kwa mujibu wa ratiba walitakiwa wawe na mkutano mwengine wakati wakila chakula cha mchana. Hiyo haikufanyika.

Ni baada ya Kim kumwambia Trump kuwa Marekani inapaswa kupunguza vikwazo ilivyoweka dhidi ya DPRK iwapo kweli anataka maelewano. Baada ya hapo Trump na ujumbe wake ukaondoka mkutanoni. Trump akaandika katika Tweeter kuwa hakusimama na kutoka kwa hasira, bali walipeana mikono kama marafiki. Hata hivyo wachambuzi wanasema ni dhahiri kuwa wakuu hao wawili hawakuelewana. Wanasema ni dhahiri kuwa mkutano huu haukuwa umeandaliwa vizuri, kama ilivyokuwa kule Singapore.

Kwani katika diplomasia mkutano kama huu unahitaji maandalizi na majadiliano ya kina baina ya washauri na wasaidizi wao. Ni lazima makubaliano yafikiwe na hata risala ya pamoja itayarishwe kabla ya wakuu wa nchi kukutana na kutiliana saini.

Kabla ya kuelekea Hanoi rais Trump alidokeza kuwa iwapo DPRK itakuwa tayari kusitisha majaribio ya mabomu ya nyuklia, yeye atafurahi sana. Ni kwa sababu huo utakuwa mwanzo mzuri utakaoashiria maelewano Zaidi. Bahati mbaya mambo hayakwenda vizuri  baada ya hapo. Nini kilichojiri? Ni kwamba mawazo na maneno ya washauri waandamizi wa Trump yalikuwa tofauti.

Wa kwanza ni Waziri wake wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo. Mnamo Oktoba 2017 wakati mazungumzo ya Marekani na DPRK yalikuwa yakiendelea, Pompeo alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi (CIA). Akapewa kazi ya maandalizi ya mkutano wa Trump na Kim. Wakati huo akadokeza kuwa Kim Jong-un alikuwa katika orodha ya watu ambao CIA iliwalenga kuwaua.

Alisema, “Iwapo Kim Jong-un atakufa ghafla, msije mkaniuliza kwa sababu sitasema lolote. Nyote mnaelewa historia ya CIA na kazi tunayofanya.”

Baada ya mkutano wa Trump na Kim huko Singapore tarehe 12 hadi 14 Juni 2018, Pompeo akapewa kazi ya ufuatiliaji wa mazungumo yao. Pompeo akaenda DPRK mara kadha na kukutana na viongozi wa huko, akimwakilisha Trump. Kumbe mambo yalikuwa hayaendi vizuri. Hii ilidhihirika wakati viongozi wa DPRK waliposema Pompeo alikuwa akidai kwa jeuri na vitisho kuwa DPRK lazima iangamize silaha zake zote za nyuklia. Badala ya kutumia busara na diplomasia alikuwa akitumia “uhuni”, walisema wakuu wa DPRK.

Risala ya DPRK ya tarehe 8 Julai 2018 ilisema:

“Tuko tayari kufanya mazungumzo na Trump kwa nia njema. Lakini ujumbe wa Marekani (yaani Pompeo) umekuja na madai ya kihuni bila ya kusikiliza upande wetu. Hawakutaka hata kuzungumzia suala la kimsingi la amani na utulivu katika Rasi ya Korea (maeneo ya Korea Kusini na Kaskazini). Hawakuona umuhimu wake.”

Hivi ndivyo Pompeo alivyokuwa akiendesha mazungmzo na DPRK kwa niaba ya Trump.

Tukija katika mkutano wa Hanoi, tarehe 27 Februari pande zote mbili zilieleza nia yao ya kuendeleza mazungumzo. Trump alisema yeye hakuwa na haraka, kwani ni muhimu kwa pande zote mbili kufikia maridhiano. Trump alikubali kuwa DPRK ilikuwa haijafanya majaribio ya silaha za nyuklia au makombora tangu mwishoni mwa 2017. Alisema kwake hilo ni jambo la maana sana.

Si hayo tu, bali tangu Septemba 2018 DPRK ilifunga kituo cha nyuklia cha Yongbyon ambacho ni muhimu sana kwa DPRK. Pia walifunga kituo cha majaribio cha makombora kilichopo Tongchang-ri. Zaidi ya hayo DPRK ilisema iko tayari kuwaalika wataalamu wa kimataifa waje huhakiki na kutoa ushauri. Sharti la DPRK ni kuwa na Marekani nayo ichukue hatua ya kuondoa vikwazo vyake dhidi ya DPRK, angalao vile vikwazo vinavyowaumiza raia wa kawaida. Huu ndio ulikuwa msimamo wa DPRK kabla ya mkutano wa Hanoi. Lakini wakati wote huo mipango tofauti ilikuwa inasukwa jijini Washington baina ya CIA, Waziri Pompeo na Mshauri John Bolton.

Hawa walikuwepo wakati Trump na Kim walipokutana Hanoi, nao walikuwa washauri wakuu wa Trump. DPRK ikatoa msimamo wake lakini Marekani ikakataa kuondoa vikwazo. Mkutano ukamalizika kabla ya muda uliopangwa na hakukuwa na risala ya pamoja ambayo hutolewa kwa kawaida. Trump akawaambia wanahabari:

“Ilibidi nivunje kikao kwa sababu DPRK walitaka vikwazo vyote viondolewe nasi tukakataa. Wao walikuwa tayari kuachana na sehemu kubwa ya mpango wao wa silaha za nyuklia, nasi tukakataa kuondoa vikwazo vyote.”

Usemi huo wa Trump kuhusu vikwazo haukuwa sahihi. Si kweli kuwa DPRK walitaka vikwazo vyote viondolewe. Walikuwa wanazungumzia baadhi ya vikwazo na ombi lao lilikataliwa na ujumbe wa Marekani. Ndipo ujumbe wa DPRK nao ukaitisha mkutano wao na waandishi ili kuweka mambo sawa. Waziri wake wa Mambo ya Nje Ri Yon-ho akasema:

“Tulitaka Marekani iondoe vikwazo ambavyo vinaminya uchumi wa wananchi na maisha yao ya kila siku. Hatukuzungumzia vikwazo vyote. Tulizungumzia vikwazo vitano tu tulivyowekewa kati ya 2016 na 2017, miongoni mwa jumla ya vikwazo 11. Nasi tulikuwa tayari  kufunga daima kituo cha kuchakata urani na plutonium inayotumika katika uundaji wa silaha za nyuklia. Kituo hiki kiko katika eneo la Yogbyon, nasi tulikuwa tayari kufanya hivyo mbele ya wataalamu kutoka Marekani.”

Ri akaongeza kuwa DPRK ilikuwa tayari hata kuahidi kimaandishi kuwa itaacha kabisa majaribio ya silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu. Bahati mbaya Trump alipoteza fursa hii adimu ambayo huenda isijirudie tena. Hata hivyo DPRK haitabadili msimamo wake kama Trump atataka mkutano mwengine, alisema Ri.

Haya ndivyo yaliyojiri huko Vietnam. Vyombo vya habari vya kimataifa vilisambaza habari tofauti kabisa. Wao walisema mkutano wa Hanoi ulivunjika baada ya Trump kumtaka Kim abomoe kituo cha Yongbyon cha kuchakata uranium na plutonium. Naye Kim akamtaka Trump aondoe vikwazo vyote vya Marekani dhidi ya DPRK.

Kimsingi wanachotaka Marekani ni kuwa DPRK iteketeze silaha zake zote za nyuklia kwanza ndipo wafikirie kuondoa vikwazo. Kuna uhakika gani kuwa Marekani watatimiza hayo? Inawezekana baada ya hapo wakaanzisha madai mapya na agenda mpya ya kile wanachokiita demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, kama wanavyofanya katika nchi nyingi duniani. Labda watamtaka Kim aitishe uchaguzi wa vyama vingi, abinafsishe mashirika yake yote na aruhusu makampuni ya kibeberu yawekeze DPRK, kama wanavyofanya duniani.

Tayari DPRK imechukua hatua kadha, kama vile kusimamisha majaribio ya nyuklia na makombora. Wamebomoa kituo cha majaribio. Pia wamekubali kuwaruhusu wakaguzi wa kimataifa kuangalia kituo cha majaribio ya mitambo ya makombora. Licha ya yote haya, Marekani inadai eti DPRK inatishia usalama wa Marekani na marafiki zake. Inakataa hata kuregeza vikwazo ili wananchi angalau waweze kuagiza madawa na pembejeo kutoka nje. Matokeo ya vikwazo vya Marekani ni kuwa watoto zaidi ya 60,000 nchini DPRK wana utapiamlo.

Kwa vyovyote vile, kuna uwezekano wa Trump na Kim kukutana kwa mara ya tatu. Habari zinasema baada ya ndege yake kuondoka Hanoi, rais Trump alimpigia simu rais wa Korea kusini, Moon Jae-in na kumuomba asaidie kupanga mkutano wake na Kim.

(This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. 0658- 010 308)

 

        

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All