• 23,000 wamejeruhiwa

Jeshi la utawala dhalimu wa Israel limeua zaidi ya Wapalestina 254 na kuwajeruhi wengine wasiopungua 23,000 tangu yaanze ‘Maandamano Makubwa ya Haki ya Kurejea' ambayo yalianza kufanyika kila Ijumaa kuanzia Machi 30 mwaka 2018.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotangazwa Jumatatu wiki hii na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, tangu Machi 30 2018, Ukanda wa Gaza umeshuhudia ongezeko kubwa la Wapalestina wanaouawa katika maandamano kwenye eneo linalotenganisha utawala wa Israel na Ukanda wa Gaza.

OCHA imethibitisha kuwa, Jeshi la Israel limeua Wapalestina 254 katika Ukanda huo tangu Machi 30 hadi Desemba 31 mwaka 2018.

Ripoti hiyo imesema watu 180 miongoni mwao, wameuawa katika Maandamano Makubwa yanayojulikana kwa jina la ‘Haki ya Kurejea’ na matukio yanayohusiana na maandamano hayo.

Aidha taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema miongoni mwa Wapalestina hao waliouawa kwa risasi za jeshi la Israel, 44 walikuwa ni watoto na wanne ni wanawake.

Tangu tarehe 30 Machi mwaka huu hadi hivi sasa, Wapalestina 247 wameshauawa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel na zaidi ya 25,000 wameshajeruhiwa.

Nchi nyingi duniani pamoja na mashirika mbalimbali ya kimataifa, muda wote yamekuwa yakilaani jinai zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya Wapalestina.

Wimbi hilo la maandamano ya Wapalestina ni la kukumbuka jinai nyingine ya utawala wa Kizayuni ya kuteka ardhi nyingine za Wapalestina tarehe 30 Machi 1976.

Kwa muda mrefu sasa siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel zimekuwa ni kuwapora Wapalestina ardhi zao na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwa lengo la kuvuruga muundo wa kijiografia wa maeneo ya Palestina na kuyapa maeneo hayo sura ya Kizayuni. (IQNA).