Uchunguzi wabaini utumwa wa ngono Jeshi la Majini Marekani

Uchunguzi uliofanyika katika Jeshi la Majini la Marekani umebaini kundi moja la wanamaji wa nchi hiyo, limeanzisha biashara ya wanawake wanaotumiwa katika masuala ya ngono.

Tovuti ya Military Times imefichua kwamba, uchunguzi uliofanyika ndani ya Jeshi la Majini la Marekani umeonyesha kuwa, harakati za wanamaji hao wa Marekani za magendo ya wanawake wanaotumiwa katika biashara ya utumwa wa ngono, zilianza mwezi Juni mwaka 2017.

Harakati hizo zilianzishwa na askari wa Jeshi la Majini la Marekani huko Bahrain kwa kutuma ujumbe kwa mwanamke aliyekuwa akiishi Thailand na kwamba, mahusiano hayo ya kingono yalikwenda mbali zaidi na baadaye nyumba ya mwanamke huyo ilitumiwa na wanamaji wa Marekani kuwinda wasichana wanaotumiwa katika biashara haramu ya ngono.

Nyaraka zilizofichuliwa zinaonyesha kuwa mwanamke huyo Mthailand, alikubaliana na wanamaji wa kimarekani kusaka wasichana wengi zaidi watakaotumiwa katika biashara ya ngono katika “soko lenye mvuto” la Bahrain.

Military Times imeripoti kuwa uchunguzi huo umebaini kuwa wanajeshi wa kikosi cha majini cha Marekani baadaye waliajiri nyumba kadhaa nchini Bahrain kwa kutumia fedha za walipakodi, kwa ajili ya kuendeshea biashara ya ngono nchini Bahrain.

Katika miaka ya hivi karibuni kumefichuliwa ripoti nyingi zinazohusiana na ufuska na ufisadi wa kimaadili uliokita mzizi katika vikosi vya jeshi la Marekani.parstoday.