Bi. Linde McAvoy, alisilimu na kuwa Muislamu wiki chache baada ya kujiunga na Chuo cha Georgia Career Institute Conyers (GCI) katika jimbo la Georgia nchini Marekani mwezi Disemba 2017.

Alichagua taaluma ya vipodozi na alianza kuhudhuria masomo akiwa amevaa vazi la staha la Hijabu na hapo masaibu yalianza kumuandama kufuatia vazi lake hilo la hijab.

McAvoy alikiandikia barua Chuo cha GCI, kupitia mawakili Waislamu, kulalamikia namna ambavyo anakerwa, kubaguliwa na kubugudhiwa na wakuu wa idara ya chuo hicho kutokana na uamuzi wake wa kuvaa Hijabu.

"Kwa mfano, Joyce Meadows, Mkurugenzi wa GCI, alianza kusisitiza kuwa Bi. McAvoy, avue Hijabu yake kwa kisingizio kuwa inakiuka taratibu za mavazi darasani," imesema barua ya Mawakili Waislamu.

Hata baada ya Bi. McAvoy kufafanua kuwa anavaa Hijabu kutokana na maamrisho ya Uislamu, Bi. Meadows, alisisitiza kuwa lazima avue Hijabu yake, licha ya kuwa taratibu za mavazi hazizuii mitandio ya kidini.

Bi. McAvoy amefukuzwa darasani mara kadhaa kutokana na uamuzi wake wa kuvaa Hijabu.

Meadows amesisitiza kuwa iwapo McAvoy anataka kuendelea na masomo, lazima avue Hijabu wakati akihudhuria darasa.

Nimra Azmi, wakili katika Jumuiya ya Mawakili Waislamu alisema ni muhimu kwa wanawake Waislamu kuvaa Hijabu na kupata elimu.

Aidha, aliongeza kuwa hakuna ushahidi wowote kuwa kuvaa Hijabu kunakiuka maadili ya kikazi.

Mawakili hao wanasema chuo cha GCI kinatekeleza ubaguzi ambao ni kinyume cha sheria na kwamba, McAvoy amebaguliwa kwa sababu tu ni Muislamu anayefungamana na misingi ya dini yake.

Sasa McAvoy anataka chuo kimrejeshee karo yake na pia kuwe na sheria maalumu inayoruhusu hijabu na pia wafanyakazi wa chuo hicho wapate mafundisho yatakayowawezesha kuacha sera zao za ubaguzi.

Kuna ongezeko kubwa la Wamarekani wanaosilimu na wengi wanakumbana na matatizo mengi maishani, hasa kutengwa katika familia na kubaguliwa katika vyuo vya elimu na sehemu za kazi. (IQNA

Most Read

  • Week

  • Month

  • All