Colors: Purple Color

 Kesi kurejeshwa Mahakama Kuu Z’bar?

Mahakama ya Rufaa, kutengua kitendawili

Na Bakari Mwakangwale

HATIMAE Mahakama ya Rufani Jijini Dar es Salaam, imesikiliza rufaa ya Jamhuri iliyokata kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu kuwafutia mashitaka 14, Masheikh wa Uamsho.

Katika rufaa hiyo iliyosikilizwa Mei 7, 2021, ilitawaliwa na  malumbano mazito ya kisheria yakiwahusisha Mawakili 20,  wakiwa Mawakili 9 wa upande wa utetezi na 11 wa upande wa Jamhuri, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP).

Chanzo chetu cha habari kimelipasha Gazeti la An nuur, kwamba kwa sasa  shauri hilo limekamilika baada ya kusikilizwa na Majaji watatu wa Rufani, ambao ni  Mheshimiwa Stella Mugasha (J. A), Mheshimiwa Shaaban Lila (J. A), na Mheshimiwa Korsso (J. A).

“Leo (Ijumaa iliyopita) katika Mahakama ya Rufani, shauri la kusikiliza rufaa ya Jamhuri dhidi ya Masheikh, limekamilika  na sasa tunasubiri kuitwa tena hapo Mahakamini kwa Tarehe itakayopangwa na Mahakama ya Rufani, kusikiliza uamuzi.” Kimesema chanzo hicho cha habari.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa katika shauri hilo Mawakili wa pande mbili walitoana jasho katika hoja za mahusiano na mgongano wa kisheria katika mambo ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hoja zilizochukua muda mrefu kujadiliwa.

Katika shauri hilo, chanzo hicho kimedai kuwa Mawakili wanaowatetea Masheikh wametoa hoja za kuonyesha uhalali wa hukumu iliyoyafuta mashitaka 14, mbele ya Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa.

“Mawakili wa Masheikh wameonyesha nguvu na uwezo wa kisheria wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, kusikiliza shauri hilo la Masheikh kuliko Mahakama Kuu ya Tanzania Bara.” Kimeeleza chanzo hicho.

Chanzo hicho kimeeleza kuwa kesi ya Masheikh imekuwa na mvutano mkubwa wa kisheria tokea kukamatwa kwao jambo ambalo linazidi kuiweka kesi hii katika sintofahamu kubwa kwa wananchi.

Kikaeleza chanzo hicho kuwa kwa sasa kinachosubiriwa kwa hamu ni kujua je, hukumu ya Mahakama ya Rufaa italirudisha shauri hilo Mahakama Kuu kuendelea chini ya hati yenye mashtaka 25, ya awali?

Au itakubaliana na hoja za kisheria za Mawakili wa Masheikh na kesi iendelee na hati mpya yenye mashtaka 11 kama ilivyoamuliwa awali na Mahakama Kuu.?  

“Hicho ni kitendawili ambacho jibu lake tunalisubiri kutoka kwa Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa.” Kimeeleza chanzo hicho cha habari.