Nguvu Moja kwa Pamoja wasonga mbele

Ni miradi ya kujitolea nguvu na mali zao

Na Bakari Mwakangwale

HARAKATI za ujenzi wa vituo vya Afya kwa nguvu za Waislamu Mkoani Kagera, zinazidi kushika kasi kwa kushambulia kwa pamoja shughuli za ujenzi wa vituo hivyo.

Hali hiyo imejidhihirisha katika miradi ya vituo vya Afya vilivyoanza kujengwa katika Wilaya za Mkoa wa Kagera, ikiwa ni katika utekelezaji mpango Mkakati wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2019-2023), chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Kagera.

Akitoa majumuisho ya harakati za ujenzi wa vituo hivyo, Mratibu wa Miradi hiyo Bw. Msabilla Raphael, amesema, baada ya kuzindua Mpango Mkakati, Julai 20, 2019, Wilayani Muleba, na uwekaji wa mawe ya uzinduzi, sasa Waislamu wanajitokeza katika Wilaya zao katika utekelezaji kivitendo kwa pamoja na kwa nguvu moja.

Akianisha shughuli zinavyoendelea katika Wilaya hizo Bw. Msabilla, alisema Wilaya ya Karagwe, katika eneo la mradi la Omugakorongo, jiwe liliwekwa Septemba 14, 2019, na ujenzi utaanza muda si mrefu, kinachosubiriwa ni vibali tu.

Alisema, Bukoba Vijijini Jiwe limewekwa Machi 25, 2020, na tayari Waislamu wameanza kushambulia shughuli za ujenzi wa jengo la OPD, kwani msingi umekamilika na upandishaji wa kuta utaanza muda si mrefu.

Ama katika Wilaya ya Misenyi, jiwe la msingi limewekwa Juni 21, 2020, na sasa Waislamu wanaendelea kushambulia uchimbaji na ujenzi wa misingi mitatu na inaelekea kukamilika.

Wilayani Muleba Waislamu wanashambulia uchimbaji wa msingi wa jengo la OPD, wakati uwekaji wa jiwe la msingi umefanyika Julai 11, 2020, na inakuwa ni Wilaya ya nne kufanikisha kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha Afya.

“Kwa sasa Waislamu wanatekeleza Azimio la Muleba, tusirudishwe nyuma bado hatujachejelewa, wasemaji wote katika kuuendea mpango huu wanahimiza Umoja na Mshikamano kuwa ndiyo nyezo kubwa ya Ushindi.” Amesema Bw. Msabilla.

Bw. Msabilla, alisema Sheikh wa Mkoa wa Bukoba, Sheikh Haruna Abdallah Kichwabuta, alitoa historia ya huzuni kubwa ya magomvi ya nyuma, akawaonya wale wote watakao rudisha majonzi kwa kuwatonesha vidonda vya mgonvi.

Sheikh Kichwabuta alieleza siri ya mafanikio ya kuiendea miradi hiyo kwa mafanikio kuwa ni utekelezaji wa kauli mbiu ya Mheshimiwa Mufti Abubakar Zubeir ya Jitambue, Badilika, Acha Mazoea.

Bw. Msabilla, alisema Sheikh wa Mkoa wa Kagera aliamua kufasiri kimatendo kauli mbiu hiyo kwa kutumia timu ya washauri na watalaam ambao kwa pamoja waliibuka na kuandaa mpango mkakati wa maendeleo wa miaka mitano (2019-2023).

“Maono ya Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Sheikh Haruna Abdallah Kichwabuta, yanaleta matunda kwa umm wa Kiislamu Mkoa wa Kagera, alivutiwa na kauli Mbiu ya Mheshimiwa Mufti na kuamua kuvunja ukuta wa kujifungia ndani.”

“Kwani alikiri wazi kuwa kwa muda mrefu ilikuwa inakwamisha harakati ndani ya Baraza na kwa sasa anapata kuona mwanga mkubwa baada ya kuwashirikisha wataalamu wa Kiislamu bila kujali itikadi zao katika Mpango Mkakati, na umenza kutekelezeka kwa kasi katika ujenzi wa vituo vya Afya.” Amesema Bw. Msabilla.

Akasema, kwa upande wa Sheikh wa Wilaya Bakwata, yeye amekuwa Mwanadiplomasia mzuri kwa kuzileta pamoja Taasisi  za Kiislamu zaidi ya nne kushiriki katika ujenzi wa kituo cha Afya.

Ambapo, alisema mmoja wao ni Sheikh Haruna wa Taasisi ya Imaam Shafii (Ijumaa na Adhuhuri) ambaye alitoa wito kwa umma kumalizia hasira zao katika kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo unaka milika kwa wakati.

“Ili kuleta tija katika utekelezaji wa mradi huu nguvu ya pamoja ya wadau ilionekana inahitajika na hivyo Bakwata ngazi ya Mkoa wa Kagera, ikaja na kauli mbiu ya kimkoa ya ‘Nguvu Moja kwa Pamoja’ ndani ya Kagera.”

“Sasa miradi inatekelezwa kwa ushikikiano wa Taasisi zote za Kiislamu zilizopo Kagera, kuna mapokeo makubwa ya muungano wa Taasisi hizi kujua kuwa maendeleo haya ya jamii hayana ngome maalumu ya kujifungia, Waisilamu kwa asilimia kubwa wamefahamu kuwa umoja ni nguvu.” Amesema Bw. Msabilla.

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All