Saidieni Madrasa-Kundecha

 

Na Bakari Mwakangwale

WAFADHILI wa masuala ya michezo wametakiwa kusaidia vituo vya Dini kama Madrasa, Twariqa na Zawia hususan katika kipindi hiki cha kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covic 19-Corona.

Wito huo umetolewa na Amir Mkuu wa Baraza Kuu la Jumiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Yusuph Kundecha, akiongea na Waandishi wa Habari, Katika Msikiti wa T.I.C, Kichangani Mago meni Jijini Dar es Salaam.

Amiri Kundecha amesema kwa sasa Madrasa zimefunguliwa kwa kuthamini na kutambua agizo la Serikali juu ya kuendelea kujikinga na gonjwa la Covic 19 (Korona) wanahimiza viongozi wa Madrasa za watoto kuzingatia kanuni za Afya katika kujinga kwa kuweka katika Madrasa ndoo za maji tiririka, Sabuni, Sanitaiza na uvaazi wa Barakao.

Hata hivyo Amir Kundecha, alisema kwa kuzingatia kuwa Madrasa na vyuo vya Dini kwa kiasi kikubwa huendeshwa kwa misingi ya kujitolea, upo uwezekano mkubwa wa kuweza kukosekana vifaa hivyo kwa watoto hao wanapokuwa katika Madrasa na hivyo sadaka zinahitajika.

Akifafanua Amiri Kundecha, alisema kusaidia vituo vya elimu ya kiimani ni jambo muhimu kwani msaada huo unakuwa umeambatana na Baraka za Mwenyezi Mungu tofauti na kusaidia katika maeneo mengine kama ya urembo na mpira.

Alisema, wao kama viongozi wa Kiimani, hawafurahi kutumia fursa hiyo badala ya kuendelea kutoa pongezi na kusahau kuyasemea maeneo yenye mapungufu na baadae yakaanza majuto tena, akasema Baraza Kuu la Jumuiya, wapo tayari kupokea misaada na kuwafikishia walengwa.

“Hivyo, pamoja na hali walizo nazo tunatoa wito kwa Masheikh, Maimamu, Walimu, Wamiliki wa Madrasa, Zawiya na Twariqa pamoja na Vyuo vya Dini kuendelea kuzingatia kanuni za Afya katika kujikinga na maambukizi, sambamba na kumuomba Allah atunusuru.” Amesema Amiri Kundecha.

Alisema, wahisani hao wafahamu kwamba sehemu kubwa ya vituo vya Elimu ya Dini hufanya kazi kwa kujitolea hivyo huwa ni ngumu kwao kuwa na gharama za ziada kwa mambo ya dharura yanapo jitokeza au kukidhi mahitaji ya wale wanaowa hudumia.

Aidha, Amir Kundecha, alisema njia za kufikisha misaada hiyo zipo nyingi moja wapo ni kupitia Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, kwani moja ya kazi ya Baraza ni kufanya kazi na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu.

“Katika Jumiya na Taasisi za Kiislamu zimo Twariqa, Zawiya na Madrasa, ikiwa Wahisani watapata tabu ya namna ya kuwafikia, Baraza Kuu lipo tayari kupokea na kusimamia zoezi la kuwafikia.

Lakini hii haina maana hakuna njia nyingine zipo njia nyingi za kuweza kuwafikia walengwa kama kuna msamalia anaweza kuwafikia bila ya tatizo ni vizuri afikishe kwani haja ni kuwafikia sio nani anafikisha.” Amesema Amiri Kundecha.

Kwa upande mwingine alivitaka vituo hivyo kuwa na kamati za Afya zinazoelekezwa na Wizara mara kwa mara au kualika wataalamu wa Afya ili kutoa somo na maelekezo yatakayo faa kusaidia kuepuka maam bukizi katika vituo hivyo.

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All