Waislamu wengi waliokamatwa ni tegemezi
Serikali ijifunze kupitia wahanga wa ugaidi
Na Bakari Mwakangwale
PAMOJA na uwepo wa faraja kufuatia baadhi ya Waislamu kufutiwa mashtaka ya ugaidi, yaliyowaweka mahabusu kwa zaidi ya miaka saba, ni wazi kwamba Umma wa Kiislamu umejeruhika.
Hayo yamebainishwa na Sheikh Mussa Kileo, akiwahutubia Waislamu katika Khotba ya Swala ya Ijumaa, katika Msikiti wa Rahma, Ijumaa ya wiki iliyopita Buguruni Jijini Dar es Salaam.
Sheikh Kileo, alisema ni jambo la kushukuru ndugu zao kuachiwa na kuwa huru huku wengi wao wakikaa mahabusu kwa miaka zaidi ya mitano, hali ambayo imepelekea kuyumba kiuchumi kwani wengi biashara zao tayari zimekufa.
Alisema, licha ya kutoka na wengine kuendelea kuwepo magerezani ni wazi kwamba hali hiyo imejeruhi umma wa Kiislamu kwa kiasi kikubwa kwani wengi iwe wametoka au waliobaki wameyumba kiuchumi.
“Hili wimbi la kuwakamata Waislamu na kuwaweka mahabusu zaidi ya miaka mitano, limewajeruhi Waislamu kwa kiasi kikubwa, ikiwa unamkamata mtu anayetegemewa na familia ya watu zaidi ya kumi ina maana hawa wote ni majeruhi.”
“Waislamu wenye tuhuma za ugaidi nchi nzima ni maelfu achiliambali wale ambao hawajulikani walipo mpaka sasa, je nyuma yao wana watu wangapi wanaowategemea, wote hao wamejeruhika katika elimu, uchumi, afya na dini yao kwa ujumla na wengine wamepoteza maisha kwa sababu ya ndugu zao kukamatwa.” Amesema Sheikh Kileo.
Alisema, hiyo ni dhuluma ya wazi, pamoja na hali hiyo inayowakabili akawataka Waislamu kuendelea kupaza sauti kupinga mwenendo huo kwani haupo katika utu kwa kumkamata na kumnyima dhamana kwa tuhuma tu ni sawa na kuwatesa watu wanaomtegemea nyuma yake.
Sheikh Kileo, alisema ni vyema kila anayedhulumu haraka aache dhuluma na arejee kwa Mola wake na afanye touba, akasema Waislamu ni watetezi wa haki na wakemeaji dhuluma, kwani mafundisho ya Dini yao yanawaambia ‘msaidie ndugu yako sawa kadhulumu au kadhulumiwa.’
“Uislamu haukubali dhuluma hata kidogo ndio maana Qur an ikasema katika aya ya 279, katika Suratul Baqara, kwamba msidhulumu wala msikubali kudhulumiwa.”
“Ndio maana Waislamu wamekuwa wakipaza sauti miaka yote wakisema haki, kwamba kama wana hatia wapeleke ushahidi kisha mahakama iamue na kama hakuna basi waachiwe.” Amesema Sheikh Kileo.
Alisema, kitendo cha kuwadhulumu watu hilo ni deni na ni gharama ambayo hakuna anaweza kuilipa isipokuwa ni Allah (s.w), na kwamba dhuluma mwisho wake ni majuto, kwani wapo waliodhulumu na hivi sasa wanajuta hapahapa duniani.
Alisema, kupitia kesi hizi na Sheria ya Ugaidi, Serikali ijifunze kitu, kwamba haifai kwani akasema miaka yote Waislamu wamekuwa wakipaza sauti kuwa sheria hii haifai na kwa mara ya kwanza walikutana Masjidi Tungi, na kusema wazi kuwa hii sheria ni hatarishi kwa raia.
“Mpaka sasa Waislamu tunasema hii sheria haifai kwa maana inakiuka ubinadamu utu, uhuru na haki.” Amesema sheikh Kileo.