Sheikh Alhad, Bi. Aisha Sururu waandaa dua kuliombea Taifa

Bint Ally Ahmed

Sheikh wa Mkoa Dar es Salaam, Sheikh Alhad Musa Salum, akishirikiana naTaasisi ya Bi. Aisha Sururu Foundation, wameandaa dua maalumu ya kuliombea Taifa itakayofanyika katika ukumbi wa P.T.A viwanja vya Sabasaba Jumapili tarehe 26, Julai 2020.

Dua hiyo inafanyika wakati huu ambapo Watanzania wanajiandaa na Uchaguzi Mkuu mwaka huu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Bi. Aisha Sururu amesema kuwa Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber Bin Ally Mbwana, atakuwepo katika dua hiyo ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. George Simbachawene na kuwaalika Waislamu kuhudhuria kwa wingi.

Alisema dua hiyo muhimu inatarajiwa kuanza saa 2:00 hadi saa 8:00 mchana.

Akiongea na An nuur siku ya Jumanne wiki hii jijini Dar es Salaam, Sheikh Alhad Mussa ametoa nasaha kwa wagombea wanaotarajia kuingia kuwania nafasi mbalimbali za uongozi nchini katika Uchaguzi Mkuu ujao kwamba, wazingatie na kujali utu, ubinadamu na heshima. Kwamba ni vizuri pia wakaheshimiane wenyewe kwa wenyewe.

Sheikh Alhad amewaasa wagombea kuacha lugha za matusi, kashfa, kejeli na kutajiana aibu zao, kwani amedai kuwa hakuna mtu asiye na aibu yake.

Aidha Sheikh Alhad alisema kuwa wagombea wanapaswa kufahamu kwamba watagombea wengi miongoni mwao na kwamba, yule atakaepata nafasi, ni yule aliyeandikiwa na Mwenyezi Mungu apate nafasi hiyo.

Lakini pia akasisitiza suala la uzalendo, utu na heshima kwa wagombea na kuwakumbusha watambue kwamba, Mwenyezi Mungu ndio anayewapa vyeo au kuvichukua pia hivyo vyeo.

Alisema kufanya juhudi ni muhimu ili kupata nafasi lakini si kwa namna isiyofaa.

Na ndipo hapo aliwataka wagombea wajiepushe na rushwa, kwani rushwa ni jambo baya.

Alinukuu maneno ya Mtume (saw) kwamba, “mwenye kutoa na kupokea rushwa amelaaniwa na Allah”.

Kwa upande wa Bi. Aisha Sururu, alisema kuwa taasisi yake na ofisi ya Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani  Sheikh Alhad Mussa Salum, wameandaa dua hiyo maalumu ya kuliombea taifa kuelekea uchaguzi mkuu, ikiwa ni maalum kuikabidhi nchi kwa Mwenyezi Mungu, kwani wameona matukio makubwa aliyoyafanya Allah (SW), likiwemo la kuidhoofisha corona nchini.

“Tulisimama kwa kumtegemea Mungu, watu waliomba dua na kujielekeza kwa Mola wao kwa dhati ya mioyo yao mpaka Mungu ameepusha na gonjwa hilo hatari lililotikisa dunia hadi leo na baadhi ya nchi bado wanahaha na Korona”. Alisema Bi. Sururu.

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All