Inspekta, Ustadhi Masoud, aacha simanzi

Ni Amir, Kamati ya Kuendeleza Uislamu

Usomaji wake Qur an, wamvutia Afisa Magereza, asilimu

Na Bakari Mwakangwale

MKUU wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Ukerewe (OC CID), na Naibu Amir wa Kamati ya Kuendeleza Uislamu Wilaya ya Bunda, Inspekta Masoud Mohammed, amerejea kwa Mola wake.

Inspekta ‘Ustadhi’ Masoud (42), ameacha simanzi kutokana na kujitoa kwake katika kuutumikia Uislamu bila kujali wadhifa na cheo alichokuwa nacho katika Jeshi la Polisi, huku pia akiwa chachu kwa Askari Polisi Waislamu wengi, kushiriki katika masuala ya Dini yao kwa hali na mali.  

 

Aidha, katika masiku ya hivi karibuni, Inspekta Masoudi, alijizolea umaarufu kupitia mitandao ya kijamii akionekana akighani Qur an, kwa ufasaha mkubwa huku akiwa kavaa sare za Jeshi la Polisi, katika muonekano tofautitofauti kwa nyakati tofauti.

 

Sambamba na hilo lakini pia alionekana katika mitandao ya kijamii akisoma Qur an, akiwa katika majukumu yake ya kazi ama katika mikusanyiko ya Polisi na katika usafiri wa gari muda wote akisoma Qur an, hali iliyopelekea jamii ya Kiislamu kumpongeza na kumtakia kheir, kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mwenendo wake huo, Ustadhi Inspekta Masoud, baada ya kifo chake Waislamu wamemuelezea kuwa ni kijana wa Kiislamu aliyetumia wadhifa na cheo chake kufuta dhana kuwa Polisi au Afisa wa Polisi nchini hawezi kusimamia Imani yake ya Uislamu awapo katika kazi hiyo.

“Katika Waislamu walioutendea haki Uislamu kwa dhahiri pasi ya kujificha, basi ni huyu Jemedari Ustadhi, Inspekta Masoud, hakuhofu kuonyesha mapenzi ya Dini yake na Waislamu tulianza kumpenda kwa hilo kupitia mitandao ya kijamii.”

 “Katika athari chanya alioitoa ni pale nilipopata taarifa kuwa mmoja wa Afisa wa Jeshi la Magereza nchini Kenya, kasilimu baada ya kumuona katika mitandao akisoma Qur’an akiwa katika sare (Uniform) za Jeshi la Polisi Tanzania.” Kimeeleza moja ya chanzo chetu cha habari.

 Akimuelezea Inspekta Masoud, kwa njia ya simu Amiri wa Kamati ya Kuendeleza Uislamu Bunda, Ustadhi Said J. Kizigo, alisema  Marehemu alikuwa mstari wa mbele katika kuhuisha Uislamu akiwa kama Naibu Amiri wa Kamati ya Kuendeleza Uislamu Bunda.

 Ispekta Masoud ameweza kuwaunganisha Waislamu watumishi na wasio watumishi akiwahamasisha kujuwa wajibu wa kila Muislamu kushiriki kuupeleka mbele Uislamu na hasa kwa upande wa Askari Polisi wa Bunda, ambapo kwa juhudi zake aliweza kuwafanya nao kuwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Kuendeleza Uislamu Bunda.

“Inspekta pamoja na kuwa na majukumu mengi ya kiusalama, lakini alitenga muda wake kushiriki na ndugu zake Waislamu kivitendo pia alikuwa kiungo muhimu sana baina ya Waislamu wa Bunda na uongozi wa Serikali Wilayani Bunda.” Amesema Amir Kizigo.

 Alisema Inspekta, Amir Masoud, amerejea kwa Mola wake lakini licha ya kuwa mtumishi Serikalini, ameacha athari na fundisho kwa wengine kwa kujitoa kwa hali na mali katika masuala ya kuendeleza Uislamu.

 Amir Kizigo amesema, Marehem aliweza kudhamini shughuli za Uratibu wa Mitihani ya Elimu ya Dini ya Kiislamu (E.D.K) na ukarabati wa chumba cha darsa duara kwa vijana wa Kiislamu na wenye uhitaji maalum Wilayani Bunda, lakini pia alikuwa mstari wa mbele kushiriki na kuhamasisha wengine kushiriki katika ujenzi wa Misikiti midogo ya pembezoni ya Wilaya ya Bunda.

 Naye Ustadhi Kondo Bungo, alisema kifo cha Inspekta Masoud, kimemgusa kutokana na ugumu wa nafasi ya kazi yake katika kujitoa katika dini kama alivyokuwa anaweza yeye bila kujali cheo chake, kwani siku zote fakhari yake ilikuwa ni kudhihirisha imani yake ya Uislamu akiwa kazini au nje ya kazi.

 “Mwaka jana tulifanya mikutano ya dini pale Bunda, Inspekta Masoud, alishiriki nasi mwanzo mwisho katika viwanja vile bila ya kujali cheo na kazi yake, kama tuliovyozoea kuona kwa wengine wakiogopa hata kusogea sehemu ambayo wapo ndugu zao Waislamu katika masuala ya Dini yao.” Amesema Ust. Kondo.

Kwa upande wake Maalim Shoko, alisema Inspekta Masoud, ameacha funzo kwa vijana, hasa watumishi wa ummah, kwani amedhihirisha kwamba kuwa mtumishi kusikufanye ukajitenga kushiriki katika mambo ya imani yako, udhaifu ambao wengi ya Waislamu wanao.

 “Hakuona tabu watu wamtambue yeye ni nani katika imani yake na jamii imenufaika na mtaji wa imani yake kivitendo, pia funzo lingine ni kutohofia kukosa kazi au kushushwa cheo kwa kudhihirisha iman yako, kwani nyota tatu alizopata zinasadifu uhodari wake kwenye kazi yake.” Amesema Maalim Shoko.

 Naye Ukht Mwapwani Mohammed, alisema kifo cha Kamanda wa Polisi Masoud Mohamed, kimetawala mitandao ya kijamii, licha ya kuwa hakuwa IGP, hiyo ni kutokana na usomaji wake wa Qur’an, waziwazi haswa akiwa katika sare za Jeshi la Polisi, akasema hakika maneno ya Allah (s.w) na hayakumuangusha chini kabla na baada ya kifo chake.

 “Kifo chake kimenifunza kuwa si lazima kuishi miaka tisini ili kuacha athari njema hapa duniani, kumbe siku chache tu unaweza kuacha athari kubwa katika jamii.”

 “Kwani si muda mrefu Afande Masoud, alivuta hisia za Waislamu kwa kuitanguliza Qur’an mbele akiwa katika majukumu yake ya kikazi, Allah (s.w) amsamehe alipokosa, atujaalie na sisi mwisho mwema, Amiin yaa Raabil A’lamiin.” Amesema Ustadhi Gogo.

 Akizungumza katika msiba huo kabla ya kwenda kuustiri mwili wa marehemu, mmoja wa Masheikh aliyepata nafasi ya kumzungumzia Inspekata Masoud, alisema Afande Masoud, kaufanyia kazi Uislamu kwa vitendo kwani alipenda kujipambanua juu ya imani yake popote alipokuwa bila kujali cheo kikubwa alichokuwa nacho katika Jeshi la Polisi.

 Alisema, mara ya mwisho, ndani ya Ramadhani hii wakati anakwenda kuripoti kazini, alipita katika mji fulani kwa ajili ya kuswali kwa kuwa pale aliishi muda mrefu, aliingia Msikitini na aliadhini katika Msikiti ule.

 Alisema, kwa adhana ile Waislamu wa eneo lile walijua Afande Masoud, yupo na muda wa Sala ulipowadia Waumini walimuomba awaswalishe, baada ya hapo walimuomba awasomee Qur an.

 “Yote hayo aliyatekeleza na Waislamu wale walifurahi, lakini kwa upande wake na yeye aliwaomba Waislamu hao wamuombee Dua, baada ya kuwaeleza anakwenda kuanza kazi katika kituo kipya, Wilayani Ukerewe. Huyu ndio kijana wetu alipenda kuwa pamoja na ndugu zake Waislamu muda wote.” Amesema Sheikh huyo.

 Naye Bw. Arcado, alisema kwa Insekta Masoud, akiwa kijana wa Kiislamu anaamini kwamba kupitia cheo chake hakuna Muislamu anaejutia alivyokitumia ila wachache ambao ni katika udhaifu wa kibinadamu.

 “Huyu ndiye mtu pekee aliyenishawishi kurudisha akaunti yangu ya Instagram kutokana na kuona ubora wa jumbe zake anazoziposti, hata wewe jaribu kutembelea ukurasa wake wa Instagram ujifunze kitu ukuze iman yako.” Amesema Bw. Arcado.

 April 17, 2020, Inspekta Masoud, akizungumzia cheo alichopewa akichukulia cheo kama dhamna, aliandika haya:-

 “Namuomba Allah (s.w) anipe uwezo, hekima na uadilifu katika majukumu yangu ya cheo hiki kipya.”

 Na May 7, 2020, aliandika maneno haya, ambayo ndio post yake ya mwisho, kabla ya umauti kumfika, akim nukuu Mtume (s a w), “Muislamu safi ni yule ambaye watu hawapati madhara kutokana na mdomo wake na mikono yake.”….kisha akamalizia kwa kuandika “Allah atujaalie mwisho mwema tusiwe miongoni mwa watu wabaya.”

 Inspekta Masoud, amefikwa na umauti ghafla Ijumaa ya wiki iliyopita (Mei 8, 2020) akiwa Hotelini, Wilayani Ukerewe, alipokwenda kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi baada ya kupandishwa cheo kuwa Mkuu wa Upelelezi ngazi ya Wilaya, katika Wilaya ya Ukerewe, akitokea Wilayani Bunda.

 Inspekta Masoud, amezikwa Mei, 10, 2020, nyumbani kwao katika Makaburi ya Nyambele, Kata ya Itonjata, Manispaa ya Tabora, baada ya mwili wake kusafirishwa kutoka Ukerewe, Mkoni Mwanza.

Inspekta Masoud, ameacha mke mmoja na watoto wanne.  

 

 

 

 

Latest News

Most Read