Na Bakari Mwakangwale
JUMUIYA ya Wanataaluma wa Kiislamu Tanzania (TAMPRO), inatarajia kufanya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa viongozi wapya wa Kitaifa, sambamba na kutoa sura mpya ya kiutendaji.
Akiongea na Gazeti la An nuur, Septemba 13, 2021, Kaimu Amir wa Tampro, Mwalim Hussein Phili, amesema, Mkutano huo utafanyika Jumapili ya Oktoba 24, 2021, Jijini Dar es Salaam.
Mwalimu Phili, alisema katika Mkutano huo kitu kinachosubiriwa kwa hamu kubwa ni kujua nani ‘atavaa viatu’ vya aliyekuwa Amir wa Tampro, Marhum Mwalimu Hashim Saiboko, aliyefariki Machi 27, 2021.
Mwalimu Phili, aliye Kaimu Amir wa Tampro, alisema kwa niaba ya Marhum Amir wa Tampro, Mwalimu Hashim Saibiko, kabla ya uchaguzi atatoa taarifa/ripoti ya yaliyojiri katika Uongozi wa Amir Saiboko, na baada ya hapo Kamati ya uchaguzi itachukua nafasi ya kuendesha uchaguzi kwa mujibu wa Katiba ya Tampro.
Alipoulizwa kama mkutano huo ni wa kuziba nafasi ya Marhum Saiboko, alisema Mkutano huo ni wa kikatiba hata hivyo alisema, unafanyika nje ya wakati kwani kama Amir Saiboko, angelikuwa hai ungekuwa umeshafanyika miezi minne iliyopita.
“Marehem (Mwalimu Saiboko) alinitaka niitishe Mkutano Mkuu kwa ajili ya marekebisho ya Katiba na Uchaguzi Mkuu, wakati ananipa maagizo haya alikuwa amelazwa hospitali.”
“Nilipoiona hali yake nikasema siwezi kuitisha mkutano huo ilihali hali yake siyo nzuri, kwakweli toka siku ananiagiza zilipita kama siku nne tu na yeye akafariki Dunia.” Amefafanua Mwalimu Phili.
Hivyo, akasema malengo na utaratibu wa marekebisho ya Katiba ya Tampro na kufanya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi, zilikuwa zimesha anza, wakati Amir Saiboko, akiwa hai.
Mwalimu Phili, alisema katika Mkutano huo wanachama watachagua viongozi wao wa Kitaifa, ambao ni Amir, pia atachaguliwa Naibu Amir, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na majina wanachama kumi ambao wataunda Baraza la Tampro.
Mwalimu Phili, alisema Mkutano huo unatarajia pia kutoa sura mpya ya kiutendaji, tofauti na ilivyokuwa awali kwa maana sasa Tampro, watoke kuwa wamiliki na uendeshaji wa mambo mbalimbali.
“Kwa sura tunayotaka kwenda nayo kwa sasa tunataka Tampro iwe muwezeshaji zaidi kwenye Tasisi mbalimbali kwa maana, wanachama tutumie taaluma zetu kuziendea Tasisi zingine pamoja na jamii kwa ujumla kuwatengenezea mambo yao.”
“Kazi kubwa itakuwa ni kutawanya wataalamu wake kufanya kazi ya kutoa ushauri kwa Taasisi zingine tena bila malipo yoyote, ili zijiendeshe kiueledi, badala ya kuwa waendeshaji au washindani wa kazi zinazofanywa na Taasisi zingine.” Amefafanua Mwalimu Phili.
Mwalimu Phili, alisema Mkutano huo Mkuu wa Oktoba, 24, umetanguliwa na Mkutano Mkuu wa kurekebisha Katiba, ambao ulifanyika Agost 2021, na kufanya marekebisho baadhi ya maeno ya Katiba.
Alisema, marekebisho hayo yamefanyika kwa lengo la kuifanya Tampro kuwa imara zaidi kulingana na wakati ambapo mabli ya kuwa na kiongozi kwa nafasi ya Amir, sasa kutakuwa na kiongozi Mkuu atakaeitwa Mudir, ambaye atachaguliwa kwa mujibu wa Katiba inavyoelekeza.
Mwalimu Phili, alisema marekebisho ya Katiba yaliyofanyika, sasa yanaruhusu wanachama wote (wa Tampro) kuingia katika Mkutano Mkuu wa Tampro, badala ya kuwakilishwa na wajumbe wachache.