Hatuoni dalili ya Hija mwaka huu

Tujiandae kwa mwakani Insha Allah

Kwa zaidi ya miezi mitatu sasa virusi vya corona vimetutengenisha na utakalezaji wa baadhi ya ibada muhimu katika imani.

Ni kutokana na kuenea kwa kasi kwa virusi vya corona, watu katika maeneo mbalimbali duniani, wengi wamebadili utamaduni, utaratibu na mwenendo wao wa kufanya baadhi ya ibada na mambo mengine ya kimaisha.

Baadhi ya watu wameahirisha mipango yao ya kusafiri na kujizuia kufika katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu.

Tumeona wengi wameacha kusalimiana kwa kushikana mikono na kukumbatiana, huku wengine wakibuni namna mpya ya kusalimiana kwa kugonga miguu.

Tumeshuhudia hata taratibu za kwenye nyumba za ibada pia zimebadilika, zote hayo ilikuwa ni jitihada za kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Tunafahamu wengi wanajiuliza, Je, ni rahisi kiasi gani kuendelea kubaki katika hali hiyo na kuwafanya watu waendelee kubadili namna yao ya kuabudu?

Lakini wakati huu, yaani hivi sasa wakati tupo katika mwezi wa Shawwal, ikiwa umebakia mwezi mmoja tu kuingia mwezi wa Dhul Hija, Je, kuna uwezekano kwa Waislamu kuweza kutekeleza ibada ya Hija ambayo ni moja ya nguzo katika Uislamu?

Kama tunavyofahamu Msikiti mkubwa wa Makka umefungwa kwa muda sasa tangu kutangazwa kuzuka kwa viruzi vya corona. Hadi sasa haijatangazwa unafunguliwa lini rasmi.

Kuna sheria mpya za kuabudu katika eneo hilo kama vile, katazo la watu kuzungukia 'kaaba' ambayo iko katika ya Msikiti na kuzuia watu kupashika. Katazo hilo limetolewa kwa mahujaji wote wageni na wenyeji wa Mecca na Medina.

Tunafahamu waumini wengi kutoka maeneo mbalimbali duniani mara nyingi wamekuwa wanatembelea katika eneo hilo la Hija hata kama sio wakati wa hija. Tumeona hata ibada za Umra hazijafanyika.

Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa watu wana huzuni. Mamlaka ya Saudia inasema kuwa hatua waliyochukua ni ya muda mfupi na haiashirii kuwa wanapanga kufanya hivyo hata wakati wa Hija.

 

Baadhi ya taratibu za kuswali ambazo zinaweza kusababisha maambukizi bado zinaendelea.

Tushauri tu kwamba kwa wale ambao walishafanya taratibu za awali za malipo ya Hija, tunawaomba kuwa na subra na tunamuomba Mwenyezi Mungu awaweke hai na wenye afya, hadi pale watakapotimiza nia zao hizo adhimu.

Lakini pia tunachukua fursa hii kuziomba taasisi, kampuni na mashirika yanayosimamia malipo na maandalizi ya Mahujaji wetu watarajiwa, kuhakikisha wanatunza amana za mahujaji hao salama hadi pale muda utakapotimu au pale ambapo Hija na Umra zitaruhusiwa rasmi.

Hatutarajii kusikia kuna taasisi au kampuni hata moja inayoshughulika na masuala ya Hija, kwamba imeghafilika na kutumia fursa hii ya kuahirishwa ibada ya Hija, kutokomea na amana za Mahujaji walioanza kufanya maandandalizi ya safari zao mapema kupitia makampini na mashirika hayo.