Tunahitaji Maridhiano kwa Amani ya nchi yetu

Oktoba mwaka huu Watanzania wataelekea vituoni kuwachagua viongozi kwa miaka mitano ijayo.

Ni muhimu tukakumbushana kwamba Tanzania imepitia mifumo mitatu ya vyama vya siasa katika historia yake hadi sasa. Kabla na hata kipindi kifupi baada ya uhuru wa iliyokuwa Tanganyika hapo mwaka 1961 na Mapinduzi ya Januari 1964 visiwani Zanzibar, pande hizi mbili Zanzibar na Tanganyika ambazo zilikuja kuungana baadaye kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilikuwa na mifumo ya vyama vingi vya kisiasa vilivyoshiriki kupigania uhuru kutoka kwa Muingereza.

Kwa hiyo kwa uzoefu tuliokuwa nao wa kushiriki katika uchaguzi mkuu zilizohusisha vyama vingi, hatudhani kama tunapaswa kuingia Oktoba 2020 tukiwa na hofu au shaka kuhusu kuwepo Uchaguzi Mkuu wenye heri, wa haki na uhuru kamili, katika mazingira ya amani na utulivu, Tanzania Bara na Tanzania visiwani.

Tunapaswa kujiandaa vizuri kufikia lengo hilo lenye maslahi makubwa kwa kila raia mwema.

Tunakumbuka siku za nyuma, kila unapofikia wakati wa uchaguzi, kada mbalimbali za Watanzania hujaribu kutoa yao ya moyoni kuelekea uchaguzi huo. Zilikuwepo asasi za kiraia ambazo wakati wa maandalizi ya uchaguzi, zilikuwa zikifanya semina mbalimbali na kuendesha elimu ya uraia kuhusiana na uchaguzi.

Maneno kama uhuru wa kushiriki, uwazi, haki za binadamu, mwafaka, utawala wa sheria, ukweli, utamaduni wa kuvumiliana, elimu ya mpiga kura, uadilifu, nafasi sawa nk. Yalitawala katika semina hizo. Alimradi kila asasi ikijitahidi kutoa elimu ili kuwashawishi watu wajitokeze, washiriki kupiga kura kwa maslahi na kwa mustakabali mzuri wa Taifa lao.

Lengo kubwa la asasi za kiraia na zisizo za kiserikali kutoa elimu ya uchaguzi, ni kuwafanya watu kushiriki uchaguzi wakiwa na ufahamu wa kutosha juu ya kwanini wanafanya uchaguzi, wanachagua kwa maslahi ya nani, waamchagua nani kwa maslahi ya umma.

Aidha tumezoea kuona katika chaguzi zilizopita, unapokaribia uchaguzi mkuu wanasiasa nao hutumia muda mwingi kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi, kwa kupitia majukwaa ya kisiasa, vyombo vya habari nk hutoa hamasa kwa wananchi tangu kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura. Huhamasisha watu juu ya umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi. Lakini lengo kubwa kwao likiwa ni kuweka mazingira ya kupata kura zaidi kwa wagombea wa vyama vyao, na kushinda na hatimaye kutwaa madaraka, tofauti kidogo na malengo ya watu wa asasi za kiraia.

Lakini tumeshuhudia hata taasisi za kidini, nao wamekuwa wakitoa nyaraka mbalimbali za kuelekea uchaguzi mkuu, wakieleza shida zao, kero zao na wakati mwingine kutoa mwongozo, maoni na ushauri kwa waumini wao juu ya kushiriki uchaguzi.

Viongozi wa dini wamekuwa wakifanya hivyo, ili kuwakumbusha wanasiasa kuwa wao wakiwa wanadini, nao wanaona kuna haja ya kuboreshwa mambo kadhaa yasiyokaa vizuri kiimani na jamii.

La muhimu kwa Watanzania wa leo ni sote tubakie ndugu. Udugu wetu ndio unatufanya tujione sisi sote ni binadamu sawa, wenye utu sawa, haki sawa na mahitaji ya msingi sawa.

Tumezoea utaratibu wa kuwapata viongozi wetu kwa kuchaguliwa na watu. Tuelekee kwenye uchaguzi mkuu wa nchi yetu, huku kukiwa na maridhiano baina ya watu au makundi ya watu katika jamii yetu.

Tuelekee katika uchaguzi tukiwa na fahamu kwamba ni vizuri watu wakaishi kwa upendo na umoja na kukabili matukio yoyote ndani ya Taifa letu kwa pamoja, tukijua sote ni wadau kamili wa hatma ya nchi yetu.

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All