Na Mwandishi Wetu

WAISLAM wa kitongoji cha Ng’ambo ya Msingi, Kilosa mjini mkoani Morogoro, Ijumaa iliyopita ya Machi 29, 2019, walifanikiwa kuzindua Msikiti wao wa kisasa walioujenga kwa miaka mitatu.

Msikiti huo ulipewa jina la Masjid Rahman ulizinduliwa na Sheikh wa Wilaya ya Kilosa Nassor Rajab Mirambo baada ya swala ya Ijumaa, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mwidimgoi, ambaye ndiye aliyepangwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Msikiti huo umejengwa na Waislamu wa mjini Kilosa wakiongozwa na Sheikh Suleiman Mdumbwa na Marehemu Mkamba Waziri Ponda, kwa kushirikiana na wahisani.

Bw. Tanga Makoye Sued, ambaye alikuwa mmoja wa waliohudhuria hafla ya uzinduzi huo, alisema kukamilika kwa Msikiti huo ni faraja kwa Waislamu wa Kilosa, kwa kuwa sasa wana nyumba bora ya kufanyia ibada na ofisi ya kupanga mambo ya maendeleo ya Waislamu na kijamii kwa ujumla mjini Kilosa.

Sheikh Suleiman Mdumbwa, mmoja wa viongozi wa Msikiti huo alisema baada ya kukamilika ujenzi wa Msikiti, Waislam mjini humo wana mpango wa kujenga shule, kituo cha afya na chumba cha kuhifadhia maiti wilayani humo.

Sheikh Mdumbwa amewaomba Waislamu wa maeneo mbalimbali nchini kuchangia harakati hizo za kimaendeleo zinazofanywa na Waislamu wenzao wa Kilosa, kwa kuchangia chochote watakachojaaliwa.

Kwa mawasiliano zaidi:0714 072 911.