Na Mohammed Said

 

NIMESOMA makala ambayo imezunguka sana katika mitandao ya kijamii kuhusu Mark Bomani, katika kinyang’anyiro cha Urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM mwaka wa 1995.

Makala hiyo kila nikiisoma inanirudisha nyuma miaka 25, iliyopita wakati wa uchaguzi Mkuu wa kwanza wa vyama vingi, baada ya kurejeshwa mwaka wa 1992 na kwa hakika huishia kwa kucheka ninapomkumbuka Prof. Kigoma Malima. Kwani ni kama vile namuona anavyonihadithia kwa staili yake ya hata jambo likiwa zito kiasi gani yeye atakuhadithia katika njia ya kukufanya wewe ucheke na nyie wasikilizaji wake mcheke pia.

Siku moja katika mazungumzo yetu alinihadithia jinsi siasa za Tanzania, zinavyochezwa kwa ustadi wa hali ya juu kiasi ni watu wajanja sana ndiyo wanaweza kutambua na kutegua kitendawili pindi kinapo mkabili.

Prof. Malima, akanipa mfano wa Jaji Mark Bomani, pamoja na yeye wa wanachama wengine wa CCM walipoomba uteuzi kuwa wagombea wa nafasi ya Urais na majina yao yafikishwe Halmashauri Kuu ya CCM ili waingizwe kwenye mchakato.

Prof. Malima, anasema yeye aliomba uteuzi ule kwa kughadhibishwa na gazeti moja lililoandika mbele kwa wino mweusi wa kukoza, ‘’Waislam Waiogopa Ikulu.’’

“Hivi hawa jamaa wanatudharau sana sisi,” Prof. Malima, alisema huku anacheka, lakini gazeti lile lilikuwa limeandika ukweli hapakuwa na Muislamu yeyote aliyechukua fomu kuutaka urais.

Prof. Malima anasema, “Pale pale nikamwambia dereva wangu akaiangalie gari ajaze mafuta kwa ajili ya safari ya Dodoma kwenda kuomba nafasi ya kugombea urais.’’

Prof. Malima, mwenyewe alikuwa na historia ya kutukuka katika kupigania Uhuru wa Tanganyika, kwani akiwa kijana mdogo na bingwa wa hesabu aliacha Shule Mzumbe mwaka wa 1957, kurudi kijijini kwao Kisarawe kujiunga na TANU, kupigania Uhuru wa Tanganyika, chini ya uongozi wa Julius Nyerere.

Sasa ikiwa Malima, hakuiogopa Government House ya Governor Edward Francis Twining na Special Branch yake vipi atishike na Ikulu ambayo anaijua ndani nje?

Wakati ule lile gazeti lilipotoka na maneno yale ya kuwabeza Waislamu katika ukurasa wake wa mbele, hapakuwa na hata Muislamu mmoja aliyeomba nafasi ya kutaka achaguliwe kugombea Urais. Prof. Malima akaendelea kusema, “Mimi nikijua fika siwezi kuchaguliwa, lakini nilitaka nitoe jibu kwa lile gazeti kuwa Waislamu hatuiogopi Ikulu.’’

Ndani ya Bunge la Tanzania, kulikuwa na kikundi cha Wabunge wamejichagua na kutengeneza genge ambalo kazi lililojipa ilikuwa ni kumzomea Prof. Malima, ndani ya Bunge kwa kila atakalofanya.

Pamoja na Wabunge hawa, walikuwapo pia na Wahariri wa magazeti ambao wao kazi yao kuu ilikuwa ni kumuandika Prof. Malima kwa ubaya. Katika hali hii Prof. Malima, alikuwa anaijua hali vizuri sana. 

Sasa tuje kwa Jaji Mark Bomani. Baadhi ya wananchi na marafiki wa Mark Bomani, walimwendea na kumuomba agombee urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na inasemekama walimshinikiza sana aombe nafasi hiyo na yeye hakutaka kuwavunja moyo akiamini kuwa anaweza akatoa mchango katika ujenzi wa taifa la Tanzania akawakubalia. Jaji Bomani, hakuwa anafahamika sana katika duru za siasa lakini aliongoza kwa idadi ya wadhamini kwa nafasi ile akifuatiwa na John Malecela.

Prof. Malima,akawa anasema, “Wengi katika sisi tuliokwenda Dodoma, kufanyiwa usaili ukinitoa mimi. wakidhani kuwa zoezi lile lilikuwa linaendeshwa kwa umakini mkubwa na kuwa wagombea watakuwa na nafasi ya kujieleza na yule ambae ataonekana ana sifa zinazohitajika ndiyo atakuwa mshindi.’’

Baada ya kuingia Prof. Malima katika kinya ng’anyiro kile cha Urais akaongezeka Muislamu mwingine, Jakaya Mrisho Kikwete. Kikwete katika maziko ya Benjamin Mkapa, alisema alisukumwa kuingia kwenye kinyang’anyiro kile na iko siku ataeleza kisa hicho. Leo baada ya zaidi ya miaka 25 ndiyo nami nimejifunza vipi siasa za Tanzania zinavyoendeshwa.

Prof. Malima amekuwa ndani ya chama kile toka enzi za TANU na nikisoma kumbukumbu zake na kufanya rejea katika mazungumzo yetu natembea katikati ya mistari ya maneno yake kwa hakika nimejifunza mengi. Nimeona pia Prof. Malima, na yeye kama binadamu amefunzwa mengi ndani ya CCM, nimeweza kubaini kuwa kuna sifa za ziada mtu anatakiwa awenazo ndipo achaguliwe kuwa Rais wa Tanzania.

Ikiwa mimi nimezitambua sifa hizi zisizoonekana kwa macho, Prof. Malima, yeye bila shaka alikuwa anazijua vizuri na alikuwa na uwezo wa kuziona kwa macho yake mawili, kuwa Jaji au Profesa si moja ya sifa za Urais. Prof. Malima, anasema alipofika chumba cha mapumziko kabla ya kuingia ndani kuhojiwa na ‘Central Committee’ alimkuta Jaji Mark Bomani, keshafika zamani na mkononi ana makaratasi mengi anatwalii.

Mkononi Jaji ana kalamu anapiga mstari hapa na pale anahangaika kuweka kila jambo mahali pake. Wasukuma na Wazaramo ni watani, Prof. Malima, akamuuliza Jaji, katika njia ya utani, “Jaji hiyo nini?’’ Jaji Bomani akamjibu, “Hii hotuba yangu mbele ya Kamati.”

Prof. Malima, akacheka sana, akamwambia Jaji, kuwa hawana muda wa kusikiliza hotuba yake na atakuwa na bahati kubwa ikiwa atapewa dakika tatu. Jaji Bomani alishtuka na Prof. Malima, alimuona kwa hakika kabisa Jaji Bomani, alikuwa kashtuka kwani hakulitegemea hilo. Iweje jambo muhimu na kubwa kama hili Kamati iwe haina muda wa kuwa sikiliza.?

Prof. Malima hakuwa na la zaidi la kuongeza alitulia tuli anamwangalia Jaji Bomani, lakini ndani ya nafsi yake akimuhurumia sana na huruma yake ilitokana na kuwa atavunjika moyo atakapotambua kuwa yeye hakuwa anajua siasa za Tanzania. Ngoma zinaporindima ni mtindo upi wa ngoma wachezaji hucheza.

Prof. Malima alikuwa anajua fika kuwa si yeye wala Mark Bomani, watapitishwa, alikuwa anajua kuwa palitakiwa wawepo watu mfano wa wao ili ngoma inoge. Prof. Malima, aliingia kuhojiwa na kutoka muda mfupi, hapa kwenye mahojiano machozi yalinitoka kwa kucheka. Prof. Malima, alijaaliwa kipaji cha kuchekesha, hakukaa akiwa wima alimuaga mtani wake Jaji Bomani, nae akamuuliza “Profesa husubiri matokeo.?’’

Prof. Malima, aliniambia alipigwa na mshangao mkubwa, pale ambapo Central Committee iliwapitisha Jakaya Mrisho Kikwete, Benjamin Mkapa na Msuya, kuwa majina yatakayokwenda mbele kwa uchaguzi wa jina moja la mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM. Taarifa zinasema Jaji Mark Bomani, aliumia sana kwa kukatwa jina lake.

Prof. Malima, yeye njia nzima wakati anarudi Dar es Salaam, alikuwa kila akikumbuka aliyoyaona Dodoma, yeye ilikuwa ni kucheka tu kwani yale yalimkumbusha yaliyomfika Chimwaga mwaka wa 1992, pale alipofanyiwa njama asichaguliwe NEC, iliyokuwa na viti 20.

Huwezi kuchoka kumsikiliza Prof. Malima, kwani alikuwa anajua mengi sana na akiyaeleza kwa namna ambayo ingawa mengi ni ya kusikitisha atakuacha taaban kwa kucheka.