Na Bakari Mwakangwale

JUMUIYA ya wanawake wa Kiislamu Mkoa wa Dodoma (JUWAKITA) imedhamiria kuwakwamua mabinti wa Kiislamu waliokwama kuendelea na masomo ya Sekondari.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa JUWAKITA Mkoa wa Dodoma Bi. Jasmin Awadhi, mwishoni mwa wiki iliyopita Mjini Dodoma, akizungumzia harakati za Jumuiya hiyo, mkoani humo kwa kuzingatia kauli mbiu ya ‘Jitambue, Badilika Acha mazoea.’

Alisema, JUWAKITA imekuwa chachu kwa kina mama wa Kiislamu mkoani humo na katika Wilaya zake kwani imekuwa mstari wa mbele kuwakusanya na kuwaunganisha wanawake kuwalingania kheri.

Amesema, tangu kuanzishwa kwa JUWAKITA, mkoani humo mpaka sasa wamekuwa na mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha darasa za kina mama kuelimishana maswala mbalimbali yahusiyo dini.

Katika maswala ya kiuchumi Bi. Jasmin, amesema wamekuwa wakifanya Sensa ya wanawake wa Kiislamu na kuwasaidia kubaini wanawake wa Kiislamu walio katika mazingira magumu.

Alisema, baada ya kufana Sensa, huwaendea wakina mama hao na kuwaunganisha na Jumuiya yao kwa lengo la kuwashirikisha na kuwasaidia kiuchumi, ambapo huwashawishi kujiingiza katika biashara kwa kuwawezesha.

Aidha, Bi. Jasmin alisema kwa upande mwingine JUWAKITA inajipanga kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Dodoma, kufungua kituo katika eneo la Chang’ombe, lenye vijana wengi wa kike ili kuwaunganisha na kuwapeleka SIDO, kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali.

Bi. Jasmin, alisema wamebaini kuwa vijana wengi haswa wa kike wapo mtaani ambao hawakuweza kuendelea na masomo ya Sekondari, hivyo kupitia mpango huo wataweza kuwakusanya na kuwapeleka SIDO, ili kupata mafunzo ya kusindika vyakula, kutengeneza Batiki, kushona na utengenezaji mapambo.