"TUNAFANYAJE Ustadh kuhakikisha akina mama wa Kiislamu wanauishi Uislamu?"

"Ustadh tunafanyaje ili mabinti zetu wawe salama kiimani..."?

Hili ndilo jambo la mwanzo ambalo Ukhty Nadhira angekuuliza punde ukikutana nae. Innaa lillaahi wa innaa ilayhi raajiuun. Amerejea kwa Mola wake, Alhamdulillaah! Ametekeleza wajibu wake na amefikisha ujumbe.

Kwa mara ya kwanza nakutana nae akiwa ni mwanafunzi wa program ya kuwaandaa Walimu wa EDK kwa Madrasa na Shule za Msingi mwaka 2006 wakati huo tayari ni mama wa watoto watatu. Mpaka wakati huo Ukhty Nadhira alikuwa mzoefu kwenye harakati za kuelimisha akina mama na mabinti wa Kiislamu, lakini kila aposikia panasomeshwa, basi alikuwa tayari kuwa mwanafunzi; kwa takriban wiki 30 hivi tulikuwa nae kama mwanafunzi. Hakuishia kuwa mwanafunzi bali alihamasisha wenzake kuwa wanafunzi na akawa mwalimu wao.

Kwa kuthanini program ile, Ukhty Nadhira aliianzisha katika Madrasa Rahman Kinyerezi mahali ambapo palikuwa ndio Kituo cha cha harakati, wakikutana akina mama na kujifunza Uislamu na kulea mabinti zao kiakili na kiroho. 

Ukhty Nadhira mbunifu wa program za kimalezi, muanzilishi na msimamizi, amewalea vijana wengi wa kike na wa kiume kupitia Daarul Uluumi Kariakoo ambapo palikuwa pakiendeshwa semina mbali mbali za kimalezi kwa vijana na wanafunzi wa Kiislamu kidato cha kwanza hadi cha sita na wanufaika wa program ile waliendelea kuhudhuria hata walipokuwa vyuoni!

Ukhty Nadhira alihamasisha, kusimamia na kushiriki makongamano ya akina mama wa Kiislamu kimkoa, kikanda na kitaifa akishirikiana na akina mama wengine wa Kiislamu. Tija ya makongamano haya ni pamoja na uwepo wa madrasa hai za akina mama na mabinti wa Kiislamu, uwepo wa shule za awali katika madrasa nyingi na kutoa ajira kwa vijana waliosomea ualimu.

Huwezi kumtaja Ukhty Nadhira kwamba alikuwa tajiri kuweza kuyafanya yote haya, lakini alijaaliwa uwezo wa ku-mobilize rasilimali na kuzielekeza zinapostahiki hivyo kujenga Imani ya kuaminiwa na kukabidhiwa amana bila tone la shaka.

Tunamuadhimishaje Ukhty Nadhira? 

Ukhty Nadhira alikuwa mpole sana kwa watu lakini mkali inapokuja jambo la Uislamu na Waislamu. Alikuwa mwenye msimamo akisimamia kile anachokiamini. Hakuwa mtu rahisi wa kukata au kukatishwa tamaa. Akipanga jambo lake muda wa kuwa anaamini yupo sahihi na lina tija kwa Uislamu na Waislamu, hachelei kubakia na watu wachache.

Alikuwa hodari mno wa kuwatia watu moyo na kuwapa bishara njema. Mwepesi kusaidia mwenye sikio makini na moyo laini. Aghalabu shida za watu wengine alizifanya zake.

Ameacha alama katika maisha ya akina mama na vijana wa kike na wakiume na kwa kila Imam na mwalimu wa madrasa aliyeshirikiana naye. Ni wajibu wetu kuendeleza pale alipoishia na kuongeza hima zaidi katika yale aliyoyafanya.

 “Hao ni watu waliokwisha pita. Wao watapata waliyo yachuma, na nyinyi mtapata mliyo yachuma, wala hamtaulizwa nyinyi yale waliyo kuwa wakifanya wao.” (2:141)

Allah Ampe Kauli thabiti. Amrehemu na Amsamehe makosa yake.

 

Abu Sumayyah Salah

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All