Na Bakari Mwakangwale

Ahimiza Kilemile wakati wa dua ya mvua

NJIA muhimu ya kuepukana na ukame unaolikabili Taifa hivi sasa ni Umma wa Kiislamu kuzidisha Istighfar kwa wingi, kwani Allah (sw) anapenda waja wake wanapomrudia na kumtaka msamaha.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Hay’atul Ulamaa, Sheikh Suleiman Amran Kilemile, akizungumza na Waislamu mara baada ya swala ya kuomba mvua (Swalatul Al-Istisqaa), iliyoswaliwa Jumapili ya wiki iliyopita katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Swala hiyo ilijumuisha Waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, na kuswalishwa na Sheikh Suleimani Kilemile.

Swala iliandaliwa na Taasisi nne za Kiislamu ambazo ni Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Hay at Ulamaa, Basuta pamoja na Alhikima Foundation.

Akizungumza katika swala hiyo, Sheikh Kilemile, alisema kwa ujumla ili dunia inyooke, ni lazima waende sawa kwa kufuata yale anayo yataka Mwenyezi Mungu, na dawa ya kurahisisha mambo magumu na kufanya yawe mepesi ni kuzidisha Istighfar.

“Tukitaka tuepukane na tatizo la ukame kama huu uliopo sasa, ni lazima Waislamu tuzidishe Istigh’far na hata tukitaka Dunia inyooke na iepukane na mabalaa, muhimu ni kurudi kwa Mwenyezi Mungu, kwani Yeye anapenda waja wake warudi kwake na wamche.” Amesema Sheikh Kilemile.

Alisema, haya yanayotokea hivi sasa watu wa Qur’an wanapaswa kuyaelewa kwa sababu kitabu (Qur an) kimeshasema na kimeeleza ufumbuzi wake na wengine wasiyoyaelewa wawaache kwani hawana sababu wala njia ya kuyaelewa.

Sheikh Kilemile alisema tatizo lilipo ni kuwa umma wa Kiislamu ni kama vile umekwenda katika kufilisiwa maarifa na kukwanguliwa kiasi kwamba na wao wamekuwa kama vile wasioelewa, hali inayosababishwa na kuacha kufuata mwongozo wa Qur’an.

“Nawaeleza Waislamu ili tuzinduane, tumeteleza wapi kwa nini kuna ukame, lazima kuna ubovu katika imani na taq’wa, nadhani katika maeneo haya mawili kuna matatizo ndio maana yanatokea haya na hii si vinginevyo, ni katika kukadhibisha imaan na Taqwa.”

“Lakini haya yanayotupata ndani na nje ya Tanzania, ni matokeo ya matendo yetu kwani Dunia imezidi kuipiga teke Qur’an kwa kuifanya si lolote si chochote.” Amesema Sheikh Kilemile.

Sheikh Kilemile alisema, huu ni mpango wa siku nyingi katika juhudi za kuwafanya Waislamu wasifuate Mwongozo wa Qur’an, akaonyesha wasiwasi kama Waislamu wanaelewa wanayofanyiwa ili wasiwe na habari na Qur’an yao.

“Kwa hiyo ndugu zangu Waislamu, si ukame tu tulionao, hata vimbunga vinavyotokea kwa wenzetu, lakini pamoja na majanga hayo haijasikika kutokea Waislamu au watu kukusanyika na kumuomba Mwenyezi Mungu, wakati Qur’an imeshasema nini cha kufanya pindi ikitokea hali kama hizo.” Amesema Sheikh Kilemile.

Sheikh Kilemile, alizitaja aya za 65, 96 na 66 katika suratul Maida na aya ya 16 katika Suratul Jini, kuwa zimeeleza wazi sababu za kutokea matatizo na kwamba haiwezekani Allah (s w) aliye wasifu waja wake kwa rahma na mapenzi kisha yanawatokea matatizo, wakose ufumbuzi wa matatizo hayo.

“Ni kwamba Qur’an tunayo mkononi, lakini hatuisomi na wala hatutaki kuielewa kwani imetoa mwenendo mzima wa namna gani tukabiliane na matatizo yetu, Kitabu hiki kina dhamana ya kulindwa hakijabadilishwa hakijaongezwa wala hakijapunguzwa, halafu wafuasi wake ndio sisi lakini bado tunaandamwa na matatizo.” Amesema Sheikh Kilemile.

Kwa upande wake Sheikh Mohamamed Issa, alisema hakuna ubishi kuwa hali ni nzito kama ambavyo watu wa Idara ya Hali ya Hewa wanaeleza kuwa hali ya hewa imekuwa na utata mkubwa mwaka huu.

Alisema, kwa kawaida muda huu ni msimu wa mvua za masika kwa Mikoa ya Pwani, lakini mpaka sasa hakuna mvua hali iliyopelekea Waislamu kuamua kukutana na kumuomba Mwenyezi Mungu ajaalie mvua yenye manufaa kwa viumbe kwa ujumla.