Na Bakari Mwakangwale

MAUMBILE ya wanaadamu ni kupatia na kukosea, na mara nyingi huenda ikawa wanaadamu wanakosea zaidi kuliko kupatia. Hili ni kwa wote bila ya kujali kwamba mtu ni kiongozi au mfuasi.

Namna nzuri ya kuweza kuyakubali maumbile haya ya kibinaadamu ni kukubali kushauriwa na kukosolewa.

Watu wengi huweza kuona dosari za wengine zaidi kuliko mazuri wayafanyayo. Kwa kiongozi pale ambapo akikosolewa afanye haraka kukubali kosa hilo na apokee ushauri atakaopewa ikiwa ushauri huo utamsaidia kufikia malengo ya shughuli wanayoikusudia.

Mtume (s a w) ametuonesha kwa vitendo namna alivyokuwa mwepesi kupokea ushauri haraka pale ambapo anaona ushauri huo unapelekea kufikia malengo.

Tukio katika Badri.

Mtume wa Allah (s w) aliondoka mapema na jeshi lake ili awatangulie washirikina kwenye maji ya Badri na awazuie wasiweze kuyatawala. Wakati wa usiku alisogea karibu zaidi ya maji ya Badri, na hapo alisimama Khabbab Ibn Almundhir, mtaalam wa mambao ya kijeshi akasema:

“Ewe Mtume wa Allah hapatulipo weka kambi yetu, umechagua kwa Wahyi kutoka kwa Allah au ni rai yako katika mbinu za kivita? Hivi hatuna ruhusa ya kuyatangulia au kuwa nyuma yao?”

Mtume wa Allah akamjibu “Hii ni rai yangu katika mambo ya kivita,” Al mundhir, akasema kwa hakika mahali hapa sio mahala (salama) pa kuweka kambi, twende tukaweke kambi karibu na maji yaliyopo karibu na Makuraish, tutashukia hapo na kisha tutaviharibu visima vilivyo bakia baada ya sisi kujenga birika, tutalijaza maji kisha tutapigana nao huku sisi tunapata maji ya kunywa na wao hawayapati.”

Mtume wa Allah akaikubali rai ile (akasema) “Kwa hakika umetoa rai yenye kufaa kabisa.”

Mtume wa Allah akasimama na jeshi lake na akaenda mpaka kwenye maji yaliyo karibu kabisa na maadui, akateremka hapo katika nusu ya usiku, kisha wakayatengeneza mabirika na wakaviharibu visima vilivyo baki.

Kama Mtume wa Allah (s w) alikua na uwezo wa kuukataa ushauri wa Khabbaab Ibn Almundhir, kwa kua ushauri huo ulikua wenye manufaa aliupokea kwa mikono miwili na kuufanyia kazi. Sifa hii kila kiongozi anawajibika kujipamba nayo katika maisha yake yote.

Ijumaa Karim