Na Bakari Mwakangwale

MASHEIKH Maimamu na viongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu nchini wametakiwa kujifunza Teknolojia ya Mawasiliano (IT), itakayo wawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa Jumamosi ya wiki iliyopita na Amir wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Mussa Kundecha, katika mahafali ya nne ya kozi ya Kompyuta, ambapo Masheikh na Maimamu walikabidhiwa vyeti baada ya kuhitimu kozi hiyo.

Katika hafla hiyo iliyofanyika katika Shule na Chuo cha Al-haramain, kilichopo Jijini Dar es Salaam, na ndipo mafunzo hayo hutolewa pia, Sheikh Kundecha alisema ni vyema kutumia fursa za kielimu zinazopatika kwa viongozi. Mafunzo hayo ya IT, yanatolewa kwa hisani ya Ofisi ya Mufti Abubakar Zubeir, kwa maana hiyo Sheikh Kundecha, akawataka Maimamu na Masheikh kutumia fursa hiyo ili kujifunza elimu hiyo muhimu kwa wakati huu wa Sayansi na Teknolojia, ambayo kwa hali ilivyo sasa siyo hiyari tena kujifunza.

Sheikh Kundecha alisema Sheikh au Imamu asiyejua elimu ya Kompyuta na elimu zingine zinazoendana na masuala ya utandawazi, itamwia vigumu kuongoza jamii yake kwani kuna mambo mengi mapya ambayo atashindwa kuyatatua na hayapo katika Fik-hi za zamani.

“Kwa ujumla sio Masheikh tu na Maimamu, bali kila Muislamu anapaswa kuunga mkono juhudi za Mufti (Abubakar Zubeir) za kueneza ujuzi wa Teknolojia ya Mawasiliano kwani elimu hiyo ni muhimu kwa kila mmoja kulingana na hali ya dunia inavyokwenda.”

Amesema Amir Kundecha. Alhaj Khalid ambaye alimuwakilisha Mufti Abubakar Zubeir, akawataka wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kwani kuwa na elimu ya IT ni sawa na kuiweka Dunia kiganjani. Katika kuboresha na kuunga mkono mafunzo hayo yanayotolewa katika Chuo hicho cha Al-haramain, Alhaji Khalid aliahidi kutoa msaada wa Kompyuta Kumi ili kusaidia ufanisi wa mafunzo hayo kwa viongozi wa Kiislamu. Akawataka Waislamu kwa ujumla kuchangamkia fursa ya mafunzo hayo kwani ni sehemu ya kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Kwa upande wao, viongozi wa vikundi vya wanawake wa Kiislamu kutoka Majohe, Bunju, Buguruni, Mwananyamala, Uwanja wa Ndege, Kigogo na Manzese, Jijini Dar es Salaam,mambao walihudhuiria mahafali hayo walisema wapo tayari kujiunga na mafunzo hayo. Wamesema, watamuunga mkono Mufti Abubakar Zubeir kwani inaonyesha ana dhamira ya dhati ya kuwakwamua na kuwasaidia Waislamu nchini hivyo ni jukumu lao kutenga muda na kujiunga katika mafunzo hayo.

Latest News