Na Shaban Rajab

POLENI Clouds media, familia ya Ephrahim Kibonde na wana habari. Ikiwa ni siku chache tangu Kituo cha Utangazaji cha Clouds Media kuondokewa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa kituo hicho Ruge Mutahaba,

nyumba hiyo ya habari imepata pigo jingine Alfajiri ya Alhamisi Machi 7, 2019 kufuatia mtangazaji wake wa kipindi cha Jahazi katika Redio Clouds, Ephrahim Kibonde kufariki dunia.

Kibonde ambaye alikuwa muongoza shughuli (MC) kwenye msiba wa Ruge kule Bukoba, alikutwa na umauti wakati akipelekwa hospitalini Bugando Mwanza kwa ajili ya matibabu. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. Thomas Rutachunzibwa katika taarifa yake, alisema Kibonde alifariki akiwa njiani kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Mwanza akitokea Hospitali ya Uhuru. Taarifa inaeleza kwamba Machi 7 majira ya saa 11:30 Alfajiri, mwili wa Kibonde ulipokelewa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Bugando jijini Mwanza.

Ephraim Kibonde ameacha watoto watatu, Junior, Hilda na Illaria. Kwa mujibu wa meneja wa vipindi wa Clouds Sebastian Maganga, taratibu zinafanyika kupanga mipango ya msiba huo. Kupitia ukurasa wao wa Instagram, Clouds Media wameandika: “Ni pigo kubwa kwa familia ya Clouds Media Group, kwa familia ya Kibonde lakini kama tulivyoshikamana kwenye msiba wa Ruge, naomba tushikamane”.

“Tukiwa bado na majeraha mabichi ya msiba wa Mkurugenzi wetu wa Vipindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba, kwa masikitiko makubwa tunatangaza kifo cha Mtangazaji wetu Ephraim Kibonde kilichotokea alfajiri ya leo (Machi 7, 2019).

“Tunamtukuza Mungu kwa maisha ya Kibonde, na kumuomba yeye ampokee na kumpuzisha katika makao ya amani ya milele. Tutaendelea kuwapa taarifa zaidi kuhusiana na msiba huu. Bwana Ametoa, Bwana Ametwaa, Jina lake Lihimidiwe”. Imeelezwa katika mtandao huo.

Imeelezwa kuwa, Kibonde alifariki akiwa Mwanza na alianza kusumbuliwa na shinikizo la damu (BP) tangu akiwa Bukoba kwenye msiba wa Ruge. Siku moja kabla ya kufariki Kibonde, iliarifiwa katika mitandao ya kijamii kwamba timu ya Uzalishaji wa Vipindi ya kituo cha Clouds Media, ilipata ajali ya gari nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Timu hiyo ilikuwa ikitoka mazikoni Bukoba baada ya kukamilisha maziko ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba, ambapo mazishi yalifanyika Machi 3, 2019, nyumbani kwao katika kijiji cha Kiziru Kata ya Karabagaine Wilaya ya Bukoba.

Habari zilisema watu hao wamepata ajali wakiwa katika gari yao yenye namba za usajili T884 DNS iliyokuwa na watu sita na wote walitoka salama lakini baadhi wakiwa na majeraha madogo. Julai 10, 2018, Kibonde alipata pigo la kuondokewa na mkewe, Sara Kibonde, ambaye alifariki dunia usiku huo wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Hindu Mandal ya jijini Dar es Salaam.

An-Nuur tunachukua fursa hii kutoa pole kwa wafanyakazi wa Clouds Media na familia ya Kibonde kutokana na msiba huu. Tunamwomba Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.