WAKATI Wakristo wakisherehekea uzawa wa Nabii Isa AS (Yesu) katika siku ya Krisimasi na pia mwaka mpya Miladia, Taasisi ya Dar al-Ifta ya Misri imesema inajuzu au ni sawa kwa Waislamu kuwapongeza wasiokuwa Waislamu kwa munasaba wa sikukuu zao na kwamba, hilo ni kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya IQNA, Tovuti ya Al Ahram imeripoti kuwa, Dar al-Ifta ya Misri, inayoshughulikia masuala ya fat’wa za Kiislamu, imetangaza kuwa Mafundisho ya dini ya Kiislamu yanawahimiza Waislamu kutoa salamu za pongezi kwa wasiokuwa Waislamu katika Id na minasaba yao ya kidini na hili ni kwa mujibu wa ubora wa tabia njema ambazo alikuja nazo Mtume (SAW).

Dar al-Ifta ya Misri imeambatanisha taarifa hiyo na ujumbe wa video kuhusu kuwapatia wafuasi wa dini nyingine salamu za pongezi kwa munasaba wa kumbukumbu za kuzaliwa manabii wao.

Dar al-Ifta iliongeza kuwa Uislamu ni dini inayowahimiza watu kuishi pamoja kwa maelewano na kwamba, hakuna kosa kuwapa wasiokuwa Waislamu zawadi na kupokea zawadi zao kwa minasaba hiyo.

Taasisi hiyo imesema kuwa kumbukumbu za uzawa wa Manabii wa Mwenyezi Mungu ni kheri na amani kwa wanadamu wote na Uislamu ni dini ya amani, rehema, ubora na watu kutembeleana na kujuliana hali.

Aidha ujumbe huo umeashiria Aya ya 107 ya Suratul Anbiyaa isemayo:

"Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote."

Katika ujumbe wake wa video, Dar al-Ifta ya Misri imetoa wito kwa Waislamu kufuatia Sira ya Mtume Muhammad (SAW) na kuwataka wasitumbukie katika mitego ya makundi ya wenye misimamo mikali ya kufurutu ada ambao wanawakufurisha wale wote wasioafiki fikra zao finyu.

Na katika tukio jingine, washiriki wa warsha iliyofanyika hivi karibuni nchini Pakistan wamesema Uislamu ni dini pekee ambayo imeangazia kila kipengee cha maisha sambamba na kulinda haki za binadamu.

Katika warsha iliyofanyika mapema wiki iliyopita, mjini Mingora nchini Pakistan chini ya anuani ya "Mtazamo wa Haki za Binadamu katika Uislamu na Magharibi", Lutfullah Saqib, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Chuo Kikuu cha Swat, alizungumza kuhusu nafasi ya Uislamu katika haki za binadamu na kulinganisha na ulimwengu wa Magharibi.

Alisema, nchi za Magharibi bado ziko mbali sana hadi kufikia kiwango bora cha haki za binadamu katika nyuga mbalimbali.

"Uislamu ni dini bora zaidi na kwa mara ya kwanza katika historia ya mwanadamu, dini hii ilibainishwa wazi kuhusu haki za binadamu katika sekta zote za maisha. Mtume Muhammad (SAW) katika hotuba yake ya mwisho alibainisha wazi kigezo cha haki za binadamu." Alisema Lutfullah Saqib (IQNA).

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All