Na Bakari Mwakangwale

ZAIDI ya Waislamu elfu mbili wamejitokeza kuchangia Damu salama, katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke, Jijini Dar es Salaam.

Zoezi hilo limefanyika Jumamosi ya Machi 9, 2019 chini ya Taasisi ya Alhikma Foundation pamoja na JAI, na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji Mh. Angela Kairuki.

Kabla ya zoezi la kuchangia damu, Waislamu hao kwa pamoja walishiriki kufanya usafi wa nje ya maeneo ya Hospitali ya Temeke, kwa kufagia na kuokota takataka zilizokuwa zinazagaa.

Aidha, walishiriki kuwafanyia usafi baadhi ya wagonjwa katika hospitai hiyo.

Akizungumza katika zoezi hilo, Waziri Kairuki, alisema kuchangia damu ni katika kheri na Baraka kwa kuwa ni katika kutimiza ibada na ni moyo wa upendo kwa mtu kumjali mwenzie aliyekuwa katika matatizo na kuhitaji msaada.

Waziri Kairuki alisema, kilicho mvutia zaidi ni kuona vijana wengi wa Shule kufika na kuhiyari kutoa damu kwa ajili ya kuwasaidia wazazi wao na wadogo zao waliolazwa Hospitalini hapo kwa matatizo mbalimbali.

“Jambo la kuchangia damu ni jambo kubwa na ni lenye kheri kubwa na Baraka nyingi, kwani mmetimiza ibada lakini pia mmetoa sadaka, huu ni moyo wa upendo na kinachovutia zaidi ni kuona vijana wengi wa Shule wamejitokeza na kushiriki katika zoezi hili.”

“Kwa wanafunzi hawa, huu ndio umri wa kuwazoesha kufanya wema na kuoneana huruma na kujitoa kwa ajili ya watu wengine kwani wakiachwa bila kushirikishwa wakifikia umri mkubwa ndipo waanze kuelezwa kujitolea katika jamii ushiriki wao unakuwa mgumu.” Amesema Waziri Kairuki.

Kwa zoezi hili la kuwasaidia wagonjwa kwa kutoa damu na kufanya usafi, Waziri Kairuki, alisema anaamini kuwa wametimiza misingi ya Kiislamu katika kuwasaidia na kuwahudumia wenye kuhitaji.

Alisema, kwa walioitikia wito wa kutoa damu kwa ujumla wametambua kuwa huduma za afya na kutoa huduma kwa wagonjwa ni muhimu na zinahitajika zaidi kwani wapo ambao hawana ndugu na inakuwa ngumu hata kupata mahitaji ya malazi.

Kwa upande wake, Ustadhi Nurdin Mohammad, alisema wamejitolea kufika katika Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa ajali, watoto, wajawazito na wagonjwa mbalimbali kwa ujumla wanaohitaji msaada wa Damu.

Alisema, kabla ya zoezi la utoaji wa damu, walishiriki katika zoezi la kufanya usafi wa nguvu ndani na nje ya maeneo ya Hospitali ya Temeke, kwani akasema usafi pia ni sehemu ya afya na Uislamu umehimiza usafi.

Ustadhi Mohammad alisema, wamejaaliwa kukusanya maji ya kunywa na maziwa zaidi ya chupa elfu tatu, keki na biskuti kwa ajili ya kuwapatia wagonjwa sadaka kutoka kwa wadau mbalimbali waliounga mkono zoezi hilo la utoaji damu.

Kwa upande wake Amir Mkuu wa Jumuiya Waislamu ya JAI, Taifa Ustadhi Yahaya Ally Masao, kwa kuelewa umuhimu wa mahitaji ya damu katika sehemu mbalimbali nchini sasa wapo (JAI) katika mikoa 18 nchni nzima.

“Katika kujitanua kwa ajili ya kutoa msaada wa damu na wagionjwa mpaka sasa tumeshaingia Unguja na Pemba na tunakusudia kufika Micheweni, Chake Chake ili kuweza kuhamasisha umuhimu wa utoaji wa damu na kusaidia wagonjwa waliopo Hospitalini.

Kutokana na changamoto nyingi tunazo kutana nazo na matatizo waliyo nayo raia (wagonjwa) tumeona ipo haja kubwa ya kujitanua na kuwepo nchi nzima.” Amesema Amir Masao.

Alisema, kikubwa wanachoagalia JAI, ni ile rasilimali watu waliopo katika maeneo husika kwa kuwaelimisha na kushirikiana nao katika suala zima la kuhudumia wagonjwa na wasio jiweza waliopo mahospitalini.

 

Most Read

  • Week

  • Month

  • All