Akutana na Mwalimu Kidege, yupo imara kiiman

Awageukia Mahabusu kuwafundisha E.D.K

Apunguza hali ya utovu wa nidhamu gerezani

Na Bakari Mwakangwale

AFYA ya Amir wa Baraza la Vijana wa Kiislamu Tanzania, Mwalimu Ahmed Kidege, ipo imara akiwa katika Gereza Kuu la Maweni Jijini Tanga, huku akiendelea na kazi yake ya Ualimu gerezani humo.

Akiongea na Gazeti la An nuur, Jumatatu ya wiki hii, Sheikh Ponda Issa Ponda, amesema amefanya ziara ya kuwatembelea Waislamu wenye tuhuma za ugaidi katika Gereza la Maweni Jijini Tanga.

Sheikh Ponda, amesema katika gereza hilo amebahatika kuongea na Mwalimu Kidege, kwa niaba ya wenzake ambapo kuna Waislamu wapatao Sabini wanaokabiliwa na kesi za ugaidi, miongoni mwao wapo mahabusu kwa mwaka wa saba sasa.

Ahmad Kidege, ni Mwalimu wa somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu (E.D.K) katika Shule mbalimbali Jijini Tanga, alikamtwa na Jeshi la Polisi Oktoba 13, 2019, akiwa na Waalimu wenzake wawili na kufunguliwa mashtaka saba ya ugaidi.

“Hali ya afya ya Mwalimu Kidege ni salama na kiimani pia yupo imara zaidi kwa sababu ukizingatia mazungumzo yake anaonyesha kuwa ni mtu mwenye matumaini ya kukabilina na kadhia iliyomfika.” Amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda, amesema Mwalimu Kidege, anaendelea na Da’awa, akiwalingania mahabusu, lakini pia anafanya kazi ya kuwaunganisha mahabusu wenye tabia tofautitofauti za kimaadili na amekuwa msuluhishi mzuri wa migogoro ya wafungwa pindi inapotokea baina yao.

Akasema, kwa wale mahabusu Waislamu, Mwalimu Kidege, ameweza kuwafanya wawe ni wenye kufanya ibada kutokana na darsa za Maarifa ya Uislamu ambazo amekuwa akiziendesha humo Gerezani.

“Askari Magereza wanamfurahia kwa kuweza kuwarejesha mahabusu katika hali ya utu na maadili mazuri wanasema tokea ameingia humo gerezani kazi anayoifanya ya kuwapa elimu ya kiimani mahabusu, hali ya utovu wa nidhamu imepungua.” Amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda amesema, mwenendo wa Mwalimu Kidege, akiwa gerezani umedhihirisha kivitendo kuwa yeye kweli ni Mwalimu wa somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu, somo ambalo humjenga mwanafunzi katika maadili na mwenendo mwema.

Akizungumzia mwenendo wa kesi ya Mwalimu Kidege na wenzake Sheikh Ponda, alisema shauri la Ustadh Kidege na wenzake linaendelea kwa njia ya TEHAMA, halipelekwi Mahakamani kwa maana linaendeshewa ndani ya gerezani yaani kesi inaendeshwa nje na wao wanafatilia wakiwa humo gerezani.

Aidha, Sheikh Ponda, alisema kwa ujumla katika kesi za ugaidi zinazowakabili Waislamu nchini kuna tatizo la upungufu wa Mawakili.

 Watuhumiwa wengi hawana Mawakili kutokana na wingi wa kesi hizo katika mikoa mbalimbali nchini.

 “Huu mfumo wa Serikali kuwakamata watu na kuwaweka Mahabusu kisha ndio waanze kutafuta ushahidi una athari kubwa sana kwa watuhumiwa kwani unakiuka haki za kibinadamu.”

“Ni bora Serikali inapomshuku mtu kwanza ifanye uchunguzi kabla ya kumkamata ikishajirizdhsha ndio imkamate mtuhumiwa na kumfikisha Mahakamani, kisha wakati huo huo watoe ushahidi wa tuhuma walizo mkamatia.” Amesema Sheikh Ponda.

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All