Na Bint Ally Ahmed

Bi. Saada Juma Ahmad, ameibuka mshindi katika fainali ya mashindano ya 11 ya kuhifadhi Qur’an tukufu kwa wanawake watu wazima mkoa wa Dar es salaam na kukabidhiwa zawadi zake.

Mshindi huyo wa jumla wa Juzuu 15 amekabidhiwa zawadi ya jokofu, cherehani, dera, cheti cha ushindi na pesa taslim shilingi 80,000 za kitanzania, huku mshindi wa pili Juzuu 15, Maryam Yunusu Ibrahim, alijipatia jokofu, dera, cheti na shilingi elfu 70,000. Halima Khamisi Mjaja alishika nafasi ya tatu Juzuu 15 na kujipatia jiko kubwa la gesi, dera, cheti na shilingi 60,000.

Mashindano hayo yalioandaliwa na Aisha Sururu Foundation, yalifanyika Jumapili Octoba 18, 2020 katika ukumbi wa City Garden, Kariakoo jijini Dar es salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Bi. Aisha Sururu, ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Aisha Sururu Foundation, taasisi iliyoandaa mashindano hayo.

Baada ya kutangazwa mshindi wa kwanza, Bi. Saada Juma Ahmad, amewashauri akina mama kuisoma Qur’an na kuitumia katika uhai wao wote, kwani kufanya hivyo ni kujiandaa kuishi maisha ya kumpendeza Allah (SW) kwa kuwa Qur’an ndio mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu.

 

“Qur’an haijaacha kitu, kuanzia unapoamka mpaka unapolala imekueleza kila kitu, imetufundisha kila jambo liwe kubwa au dogo, malezi au maisha ya ndoa, hakuna jambo lililoachwa kwenye kitabu cha Allah, kufungamana nacho ni kuwa katika mafanikio makubwa” Alisema Ukht. Saada.

Alisema siri ya ushindi wake ni kuweka juhudi katika kuhifadhi kitabu cha Mwenyezi Mungu, kumtanguliza Mungu, bidii, na kutokata tamaa katika kusoma.

Kwa upande wake mshindi wa kwanza wa Juzuu 10 Ukht. Tima Othmani Ally, alisema ana furaha kubwa kwani huwa anashiriki mashindano hayo kila mwaka, lakini hajawahi kushinda. Hata hivyo hakukata taama na leo amefanikiwa kuwa mshindi wa kwanza wa Juzuu 10.

 

Aliwaasa wanawake kujitahidi kuisoma Qur’an, kwani mtu anapokuwa ameihifadhi kifuani mwake, ni sawa na kujiwekea kinga katika mwili wake kutokana na kufanya mambo maovu. Alisema Qur’an ni kinga na ni mwangaza katika maisha.

 

Katika mashindano hayo, washindi wa Juzuu ya kwanza hadi Juzuu ya 10 nao walikabidhiwa zawadi mbalimbali, zikiwamo jokofu mitungi ya majiko ya gesi, madera, cherehani, blender na fedha taslimu.

 

Kwa upande wa Juzuu 1 mshindi wa kwanza Amina Athumani Mkotya, alipata vyombo vya Hotpot, jiko la gesi, dera, cheti na shilingi 25,000. Mshindi wa pili Juzuu ya kwanza Ukht. Maimuna Abdallah Ally, alipata hotpot dera, cheti na shilingi 20,000 huku mshindi wa tatu wa Juzuu ya kwanza Ukht. Aisha Abduljabar Haruna, akijinyakulia hotpot dera, cheti na shilingi 15,000.

 

Mshindi wa kwanza Juzuu ya tatu Ukht. Wahida Sharif Aziz, alijipatia jiko la gesi, sufuria tatu, dera, cheti na pesa taslimu 40,000 huku mshndi wa pili Juzuu ya tatu Ukht. Mwanaharusi Ally Mikoma, akijipatia jiko la gesi, sufuria tatu, dera, cheti na pesa shilingi 30,000 na mshindi wa tatu Ukht. Wasila Masoud Jongo, alijipatia jiko la gesi, sufuria tatu, dera cheti na pesa elfu 20,000.

 

Mshindi wa kwanza Juzuu tano Ukht Salama Amani Saidi, alijishindia cherehani, dera, cheti na elfu 50,000. Mshindi wa pili Juzuu tano Ukht Subira Othmani Ally, alijipatia cherehani, dera, cheti na shilingi elfu 30,000, Ukht Aisha Hamad Darous akijipatia shilingi 20,000

Juzuu ya saba mshindi wa kwanza alikuwa ni Ukht. Mariyam Musa Ally, aliyezawadiwa cherehani, dera, cheti na shilingi 60,000. Mshindi wa pili Juzuu saba ni Time Ally Abdallah, aliyepata cherehani, dera, cheti na shilingi 50,000 na mshindi wa tatu Juzuu 7 alikuwa Ukht Faudhia Suleimani, aliyepata cherehani, dera, cheti na shilimgi 40,000.

Mshindi wa kwanza Juzuu 10 Tima Othmani Ally alijipatia cherehani, blender, dera, cheti na 70,000 na mshindi wa pili Salma Kombo Kasim alijipatia cherehani, rice cooker, dera, cheti na 60,000 huku mshindi wa tatu Juzuu ya 10 Husna Ally Rashid, alijinyakulia cherahani, dera, cheti na shilingi 50,000.

Mwenyekiti wa mashindano hayo Bi. Amina Njechele, amesema kuwa mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi ikilinganishwa na ya mwaka jana, lakini pia yameshirikisha washindi wa Juzuu 1,2,3,5,7,10,15 na kushirikisha washiriki wa mkoa wa Dar es salaam.

Lakini pia walishiriki wapatao 100 walifanyiwa michujo minne na kupatikana washindi 50, ambao ndio walioshiriki mashindano ya mwaka huu.Alisema dhumuni la kufanya mashindano hayo ni kuwainua wanawake kiuchumi, lakini pia kuwavutia waipende kuisoma Qur’an kwani ndio muongozo wa Waislamu.

Bi. Aisha Sururu, Mwenyekiti wa taasisi hiyo alisema kuwa mashindano ya mwaka huu ni ya aina yake ambapo wameshiriki kina mama wa umri mkubwa wa miaka kati ya 60 na 70, hivyo kina mama na wanawake kwa ujumla wanatakiwa kuishi Qur’an kwani mtu akishikamana na Qur’an hawezi kuwa katika mambo maovu na ya kumchukiza Allah (s.w).

 

 

Latest News

Most Read