Rais Hussein Ali Mwinyi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi baada ya kushauriana na chama cha ACT Wazalendo, alimchagua Othman Masoud, kuwa Makamu Mpya wa Kwanza wa Rais wa serikali ya Zanzibar.

Mh. Othman ameapisha rasmi Machi 2, 2021 katika ukumbi wa Ikulu ya Zanzibar, ikiwa ni wiki mbili kamili tangu kufariki kwa Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alizitawala siasa za Zanzibar kwa takribani miaka 40.

Mh. Othman Masoud Othman, maarufu kwa jina la Ochu, ni mmojawapo ya Wazanzibari mahiri na wa kutajika katika masuala ya sheria na mikakati. Uteuzi wake haukuja tu kimiujiza au kama bahati, bali sifa za usomi, uwezo na weledi, misimamo yenye maslahi na umma, uzalendo na uchapakazi ndizo silaha alizobarikiwa na mwenyezi Mungu zilizomfikisha hapo alipo.

Kazaliwa kijiji cha Pandani Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba mwanzoni mwa miaka ya sitini. Baba yake mzazi Sheikh Masoud Bin Othman, alikuwa mmoja wa walimu mahiri wa dini akifundisha darsa Misikitini, madrasa na hususan katika Skuli ya Pandani, ambako alifundisha Qur’an.

Mh. Othman alianza masomo yake ya msingi katika Skuli ya Pandani ambapo alionyesha umahiri mkubwa darasani, akishika nafasi ya kwanza katika miaka yake yote na kuwaacha wanafunzi wenzake kwa mbali sana kiwastani. Kama ilivyokuwa matarajio ya wengi, Othman mwenyewe, alipasi vizuri mitihani yake ya michepuo na kupata nafasi ya kuendelea na masomo katika Skuli ya Fidel Castro, Chake Chake, Kusini Pemba.

Akaendeleza ukipanga na kufaulu kwa daraja la kwanza (Division One) na kufanikiwa kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa shahada ya kwanza katika Sheria (LL.B). Akiwa UDSM, Othman Masouid alikuwa mwanafunzi mahiri kwenye Kitivo cha Sheria akiwa na uwezo mzuri darasani na kujenga hoja kwenye mijadala. Alihitimu masomo yake chuoni hapo kwa kupata digrii ya kwanza ya Sheria yenye heshima (Cum Laude/With Honors).

Baada ya mahafali UDSM alirejea Zanzibar na kuajiriwa na SMZ katika Wizara ya Katiba na Sheria kama Wakili wa Serikali. Alifanya kazi vizuri serikalini na baadaye SMZ ikampa ufadhili kwenda Chuo Kikuu cha London kuongeza ujuzi kwa kuchukua Shahada ya Pili ya Sheria (LL.M). Alipohitimu alirejea Zanzibar na baada ya muda mfupi akateuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Utawala Bora na Sheria katika kipindi uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Dk. Salmin Amour.

Alikuwa msomi aliyejiamini kazini na kutimiza majukumu yake bila ajizi, hivyo aliaminiwa sana na mfumo wa uongozi wa nchi.

Rais Amani Abeid Karume alipoingia madarakani alimteua kuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Mashtaka Zanzibar, kazi ambayo nyaraka zinaonyesha aliifanya vizuri japo yalikuwepo malalamiko kuwa alitumia nafasi yake kulazimisha kuajiriwa watu wa asili ya Pemba zaidi katika ofisi hiyo.

Novemba 2010 Dk. Ali Mohamed Shein, alichaguliwa kuwa Rais wa saba wa Zanzibar na katika moja ya teuzi alizofanya katika kuunda serikali yake, ilikuwa kumteua Othman kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Moja ya kazi yake kubwa katika cheo hicho kipya ilikuwa mapitio ya sheria mbalimbali za Zanzibar na Muungano. Katika mchakato wa majadiliano ya mabadiliko ya katiba ya Tanzania, Othman alikuwa nyota iliyotoa mwanga, hasa kwenye mijadala migumu na tata iliyohusu mambo mbalimbali.

Wakati wa mchakato huo wa mabadiliko ya Katiba, mabalaa yalianza kumuandama Mh. Othman, hasa kutokana na misimamo yake kwenye utetezi wa mambo yahusuyo Zanzibar, uumini wa Serikali tatu na kupunguzwa mambo ya muungano.

Moja ya nadharia yake mashuhuri ilikuwa ni ile ya kusema kila jambo moja la muungano ni kama liko katika kontena, na ndani ya kontena hilo yako makontena mengine elfu. Katika sekeseke hilo la Katiba na misimamo yake, Othman alitimuliwa katika Bunge la Katiba chini ya ulinzi wa vyombo ya usalama na kisha kurejeshwa Zanzibar, ambako alivuliwa nafasi yake kama Mwanasheria Mkuu wa SMZ.

 

Baada ya mitihani hiyo Othman akaamua kuingia kwenye siasa, akiamini ni njia nyengine ya kusimamia yale anayoyaamini. Akajiunga na Chama cha Wananchi (CUF) na kuteuliwa kuwa Mshauri Mkuu wa Chama na Mshauri Maalum wa aliyekuwa Katibu Mkuu CUF, Marehem Maalim Seif Shariff Hamad.

Mbali na misukosuko aliyokuwa akiipata, ubongo wa Othman bado ulikuwa inachemka na aliamua kurudi tena darasani. Safari hii akajiunga na Chuo Kikuu cha Turin nchini Italia kusoma Shahada namba mbili ya Uzamili (Master) katika Sheria (LL.M) na kuhitimu vizuri.

Alipokuwa nje ya SMZ na ndani ya siasa za upinzani, popote alipokwenda ndani na nje ya Zanzibar, bado alitoa na kusimamia mawazo yake yale yale kuhusu haki za Zanzibar, akiamini kwenye serikali tatu na mamlaka kamili. Hata hivyo dhoruba ilipoipiga CUF na kuamua kugawana mbao, Marehemu Maalim na kundi lake wakitimkia ACT Wazalendo, akiwemo Othman Masoud.

Mbali na siasa, Othman alikuwa anamiliki kampuni yake binafsi ya masuala ya sheria iliyopo eneo la Mombasa mjini Zanzibar, kwenye jengo la Bopar Enterprise. Wateja wake wakiwa ni watu binafsi na makampuni, lakini pia hutoa huduma kama mshauri mwelekezi katika mashirika mbalimbali ya kimataifa nje ya nchi.

Bila shaka Othman ni msomi, mtumishi mahiri wa umma na kaiweka Zanzibar moyoni, lakini mbali na hayo kama alivyo binadamu yeyote yule, anaweza akawa na mapungufu yake, lakini uchache wa mapungufu haukuweza kumuondoa katika fikra za viongozi wake waliomwamini, wakaona anaweza kuvaa koti la Marehem Maalim Seif Shariff Hamad.

Othman ni mtu anayetegemewa sana na chama chake cha ACT Wazalendo katika siasa za Zanzibar kutokana uelewa wake wa eneo hili. Alikuwa karibu sana na viongozi wakuu wa chama hicho hasa Marehem Seif Shariff Hamad, Jussa na Mazrui.

Othman alionekana pia kuwa ndiye mpanga mikakati mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, anayetoa mwongozo wa vipi chama hicho kinaweza kushinda katika uchaguzi mkuu ulioofanyika baadaye mwaka huu.

Huyo ndiye Othman Masoud Othman, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar. zanzibardaily.com

Latest News

Most Read