Waachiwa wakamatwa tena
Washtakiwa upya, warudishwa gerezani
Wamwaga machozi, wamekaa miaka 8 Mahabusu
Na Bakari Mwakangwale
WATUHUMIWA wa kesi za ugaidi, katika gereza la Mahabusu Morogoro, wamejikuta katika wakati mgumu baada ya Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, kuwaachia huru kisha kukamatwa tena na kushtakiwa upya.
Tukio hilo limewakumba Waislamu 21, Februari 22, 2022, wakiwa katika makundi mawili ya kesi za ugaidi zenye Namba P.I.16 na P.I.17, kwa kukusudia kufanya vitendo vya kigaidi, tuhuma zilizowaweka gerezani kwa takribani miaka minane.
Waislamu hao waliachiwa huru Februariy 22, 2022, katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, baada ya kufutiwa mashtaka yote ya ugaidi, kwa maelezo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendelea na kesi hizo.
Akiongelea tukio hilo kwa njia ya simu kutoka Mjini Morogoro, Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa Mkoa wa Morogoro, Sheikh Juma Kitunga, alisema baada ya kufutiwa kesi, na kuanza kutoka nje walikutana na Askari wenye silaha na kuwaambia kuwa wote wapo chini ya ulinzi.
Sheikh Kitunga, alisema amri ile iliwafanya wapigwe na butwaa na wakiwa katika mshangao huo, palepale waliamriwa warudi Mahakamani, ambapo walimkuta Hakimu yuleyule aliyewafutia mashtaka dakika chache zilizopita.
Alisema, Hakimu huyo aliwasomea mashtaka mapya yenye Namba P.I.9/2022, huku tuhuma (makosa) waliyosomewa yanafanana na yaleyale ya kesi P.I 16 na P.I. 17, waliyofutwa muda mchache uliopita, katika Mahakama hiyo.
“Hali hiyo iliwashangaza watuhumiwa hao kwamba wamekaa gerezani kwa miaka minane, wakituhumiwa kwa makosa ya kula njama kwa pamoja kutaka kutenda vitendo vya ugaidi, ambayo wamefutiwa kisha tena wanakamatwa na kupewa tuhuma zilezile.” Amesema Sheikh Kitunga.
Akifafanua Sheikh Kitunga, alisema kesi hiyo mpya inaonyesha mashtaka ni kama yaleyale na sehemu wanazotuhumiwa kutaka kutenda vitendo vya ugaidi ni zilezile.
Alisema tofauti ni kwamba sasa wamejumuishwa katika kesi moja iliyopewa Namba, P.I.9 ya mwaka 2022, yenye watuhimiwa 21, ambapo awali zilikuwa ni kesi mbili tofauti.
Alisema, baada ya kusomewa mashtaka yao, kesi hiyo iliahirishwa mpaka Machi 8, 2022, na watuhumiwa wote walirudishwa katika gereza la Mahabusu Morogoro Mjini, kwa kuanza kusubiria mwenendo wa kesi hiyo mpya.
Sheikh Kitunga, alisema kufuatia hali hiyo, Jumamosi ya wiki iliyopita, alilazimika kwenda gerezani na kuongea nao akitaka kujua nini kinachoendelea kwa Waislamu hao.
“Nilipofika niliwakuta katika hali ya huzuni tofauti na miaka yote waliyokaa gerezani wakisubiri hatima yao, na baada ya kuniona walilia sana, kibinadamu na mimi ilinibidi nilie, kwakweli ni jambo la kusikitisha wanatia huzuni sana.”
“Ndani ya majonzi yao waliniambia wameumia sana na wamefanyiwa dhuluma kubwa ni bora wangewaacha katika hali ileile ya awali, kitendo cha kuwaachia na kuwakamata tena ni jambo ambalo limewaumiza sana.” Amesema Sheikh Kitunga, akirejea maongezi yake na mahabusu hao.
Alisema, baada ya kutoka gerezani, kama kiongozi, aliitisha kikao cha Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Morogoro, inayoshughulikia Waislamu wenyeye tuhuma za ugaid, ambapo kikao hicho kilifanyika Februari 27,2022.
“Kikao hicho tulikubaliana kwamba tuandike barua kwa DPP, na nakala kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hatuwezi kukaa kimya katika tukio hili kwa sababu tunaona dhuluma imetengenezwa waziwazi.”
“Japo hatupaswi kusema sana kwa kuwa kesi ipo Mahakamani, lakini unajiuliza hawa watu walikuwa gerezani kwa miaka minane leo unawakamata na kuwapa mashtaka kama yaleyale ambayo ushahidi wake umeshindikana kupatikana kwa miaka minane.” Amesema Sheikh Kitunga.
Hata hivyo Sheikh Kitunga, alisema baada ya tukio hilo alimpigia DPP, lakini hakupokea simu, tofauti na awali wakati wanafuatilia suala hili, alikuwa mwepesi wa kupokea simu yake na wakati mwingine DPP, alikuwa akimpigia na kumpa maelezo ya mwenendo wa kesi za Ugaidi.
Sheikh Kitunga, alisema awali wakati wanafuatilia hatma ya ndugu zao hao katika kesi ya awali iliyofutwa, Januari 31, 2022, DPP alimpigia simu na kumtaka aende Ofisini kwake Jijini Dodoma.
Alisema, akiwa Dodoma, DPP, alimweleza kwamba Wanasheria wa Serikali, wapo wanapitia mafaili yote ya watuhumiwa wa ugaidi nchini, hivyo wampe muda mpaka Februari 15, 2022, ajiandae kwenda Mahakamani, kuwachukua vijana wake.
“Aliniambia kama itaonekana kuna mwenye asilimia themanini ya makosa kwa sababu wamekaa jela miaka mingi (miaka nane) watatolewa kwa dhamana sasa hiki kilichotokea hapa Morogoro kwakweli sielewi kinamaanisha nini.” Amesema Sheikh Kitunga.
Wakati hali ikiwa ni ya huzuni kwa Waislamu hao Mkoani Morogoro, hali imekuwa kinyume katika Magereza mengine mikoani, kwani Mahakama zimeendelea kuwaachia huru Waislamu kati ya mamia ya Waislamu wenye tuhuma za ugaidi walioko katika magereza mbalimbali nchini na kupeleka vicheke na furaha kwa ndugu na jamaa zao.
Hatua hiyo kwa watuhumiwa hao wote walioachiwa imetokana na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kutoona hatia yoyote kwao.
Jijini Dar es Salaa, Jumla ya Waislamu 15, wenye tuhuma za ugaidi wamefutiwa mashtaka, wakati taarifa kutoka Musoma, zinaeleza kuwa Mahakama ya Wilaya ya Musoma, imewaachia kwa dhamana Waislamu 17, na Jijini Mwanza takriban Waislamu hamsini nao wameachiwa.
Kutoka Mkoa wa Pwani, Mahakama ya Mkao wa Pwani (Kibaha) imewaachia Waislamu 40, ambao walikamatwa na kuwekwa gerezani kwa miaka saba iliyopita.
Mkoani Shinyanga, Mahakama ya Mjini Shinyanga, imewaachia huru Waislamu wanne wakiwemo wanawake wawili waliokuwa wanatuhumiwa kwa kesi za ugaidi, wanawake hao ni Bi. Mariam Hajji na Bi. Jasmini Abubakari, ambao walikuwa gerezani kwa muda wa miaka saba.
Kutoka katika Gereza la Maweni Jijini Tanga, taarifa zinasema, Waislamu watatu wameachiwa huru akiwemo Mwalimu maarufu wa somo la Maarifa ya Uislamu, Mjini Tanga, Ustadhi Ahmad Kidege.
Hata hivyo, wakati Waislamu hao wakiachiwa huru kuna mamia ya wengine waliokamatwa tangu 2013, bado wanashikiliwa katika magereza mbalimbali kwa madai ya upande wa Jamhuri kutafuta ushahidi.
Gazeti la An nuur, lilivyowasiliana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Sylvester Anthony Mwakitalu, ili kujua kadhia ya watuhumiwa wa Morogoro na hatma ya Waislamu wengine ambao bado wapo Mahabusu kwa tuhuma za ugaidi, simu yake iliita, bila kupokelewa.