Waongoza Waislamu katika Dua ya Kunuti

Mmoja akhutubu Mtambani, mwingine Masjid Jumaa

Na Bakari Mwakangwale

VIONGOZI wa Jumuiya ya Uamsho, Sheikh Msellem Ally na Farid Had, wamehutubia Waislamu Jijini Dar es Salaam, sambamba na kuongoza Dua ya Kunuti.

Viongozi hao walikuwa Jijini Dar es Salaam, kwa mwaliko wa Shura ya Maimamu, ili kushiriki katika Dua maalum ya Kunuti, kwa ajili ya kuwaombea Waislamu walio katika magereza, mbalimbali nchini wakituhumiwa kwa Ugaidi.

Dua hiyo, imesomwa Ijumaa ya wiki iliyopita Novemba 5, 2021,  katika Misikiti mbalimbali Jijini Dar es Salaam, huku Sheikh Msellem, akiongoza Dua hiyo katika Msikiti wa Ijumaa uliopo Gongo la Mboto, wakati Sheikh Farid, yeye akimeongeza Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, wote walihutubu na kuswalisha.

Akihutubia Waislamu katika Msikiti wa Ijumaa Gongo la Mboto, Sheikh Msellem, alisema wanadamu wanaishi katika maisha ya uadui kwa maana wao wenyewe kwa wenyewe ni maadui na hili si ngeni katika nafsi zao na  kila mmoja anafahamu.

“Kimsingi tufahamu kuwa tupo hapa Duniani ijapokuwa tunafanana sura na maumbo kwa maana sote ni binadamu lakini, tunatofautiana kwenye imani na matendo, wasifu wa maisha yetu ndio upo hivyo.” Amesema Sheikh Msellem.

Sheikh Msellem, alisema katika mchanganyiko wa maisha ya hali hiyo Allah (s.w) anaangalia na anaona yale au kile ambacho kila  mahali katika Dunia ya sasa kinafanyika.

Alisema, mtu atakapo amua kuyaendea maasia, Allah hatumii nguvu kumzuia bali inatosha tangazo lake kwa maandiko aliyoyatuma, pale aliposema watakao ufuata muongozi wake ndio watakao fanikiwa na hawatakuwa na hofu wala huzuni.  

“Wewe unasoma maandiko au unayasikia yakisomwa unawaona wanao yaheshimu sasa utakapoamua kuchukua na kutumia madaraka yako mikononi ufanye utakavyo, elewa hakuna nguvu utakayoina inakuzuia, wefanya utakavyo.”

“Lakini hivyo unavyofanya usidhani umeridhiwa, ndio maana Allah akasema, anaangalia mnachofanya ila ipo siku aliyo iandaa ya kutoa matokeo ya mlicho fanya hapa ardhini.” Amesema Sheikh Msellem.

Akisherehesha aya ya 67-71 za Qur an, Sura ya 9, Sheikh Msellem, alisema aya hizo zinawapa wasifu wa maisha yote ya Duniani.

 

Akifafanua Sheikh Msellem, alisema mtu anaeitwa mnafiki ni Muislam aliyetamka Shahada mbili na anapojisikia kuswali anaswali na anaonekana anafanya khairat mbalimbali lakini Muislamu akiwa  na sifa hii, Uislamu wake unakuwa ni sawa na ukafiri.

Kwani Sheikh Msellem, alisema inakuwa hivyo kwa sababu anachokidhihirisha si kilicho moyoni mwake na lolote la kheir unaloliona anafanya linakuwa nyuma au mbele yake anakuwa kakusudia latija ya kidunia.

“Huyu hataki radhi ya Allah na anapoacha kufanya ubaya haina maana anamuogopa Allah na anapofanya jambo jema la kheri si kwamba anahitaji thawabu, bali kipaumbele chake ni maslahi yake ya Dunia.”

“Huyu ndio mnafiki hata kama anaitwa jina zuri Abdallah, Abdulmanan, Abdulrahmaan, lakini kama muamala wake na Mola wake sio mzuri, afahamu yule anayepima imani za waja anamtoa katika hesabu ya watu waliomkubali.” Amefafanua Sheikh Msellem.

Aidha Sheiklh Msellem, alisema ukiona mji kwa asilimia zaidi ya themanini ni Waislamu, lakini maovu yameshika kasi na hayana wakemeaji, hii ni alama moja wapo ya kukujuza kuwa, Waislamu wa hapo si Waislamu wazuri.

Sheikh Mselem, alisema hiyo ni alama mbaya kwa jamii ya Waislamu, wanakuwa ni Waislamu kama wanavyojitangaza lakini kwa vigezo vya kiimani Allah (s.w) anasema hawa wana magonjwa ya kinafiki sio wakweli kwa wanachokitangaza.

Alisema, kwa upande mwingine jamii hiyo ya Waislamu wa hivyo akitokea Muislamu mwenye mapenzi na watu wake akakemea maovu yanayofanyika, mkemeaji huyo ndio anakuwa mkosa.

“Atachukuliwa hatua na wanaomchukulia hatua ni Waislamu wenzake, hali hiyo inatoa picha kwamba hao ni Waislamu lakini si Waislamu wazuri wenye kuupenda Uislamu wao.”

“Bali wanajitangaza midomoni tu lakini nyoyoni mwao sio Waislamu kwa sababu yale mema anayoyatangazia Allah thahwabu wao ndio wanayadhibiti na kuyakaza.” Amesema Sheikh Mselem.

Naye Sheikh Farid Had, akiwahutubia Waislamu katika Khutuba yake Masjid Mtambani, alisema Mtume (s.a.w) amesema Muislamu anapaswa kumthamini Muislamu  mwenzie asimdhulumu, asimdhalilishe, asimuache akidhulumika huku yeye anaendelea na yake.

“Tambueni Muislamu kwa Muislamu mwezie mambo hayo ni kharamu msifanyiane, usiguse damu ya mwezio, usihatarishe maisha ya Muislamu mwezio na mali yake Muislamu usiichukue bila ya ridhaa yake na heshima yake usiichezee.” Amesema Sheikh Farid.

Sheikh Farid, alisema Allah anasema, wasiotubia kwa haya na mfano wake watambue kuwa wao ni madhalimu na ukifa katika hali hiyo, huna muombezi atakaesikilizwa ili usamehewe.

Sheikh Farid alisema, ifahamike kwamba mwanadamu ni bora kufa hali yakuwa ni mdhulumiwa utasalimika mbele ya Allah (s.w) kuliko kufa ukiwa wewe ni dhwalimu.

 

 

Latest News

Most Read