Lakini hakuwahi kufika Mtwara…

Alikamatwa 2017 ameachiwa juzi

Na Bakari Mwakangwale

Ustadh Omari Salum Bambo amesema, amesota gerezani kwa miaka mine (4) akidaiwa kufanya ugaidi Mtwara, wakati huko Mtwara kwenyewe hakuwahi kufika kabla.

Alisema, yeye alitekwa baada ya kuitwa kwa simu na watekaji maeneo ya Tandika Jijini Dar es Salaam, na kupelekwa Kituo cha Polisi Tanzara, ambapo aliwekwa pale kwa muda wa wiki mbili.

Kisha alipelekwa kituo cha Polisi Ikwiriri, napo alikaa kwa muda wa wiki mbili na baada ya hapo alipelekwa Mtwara, na kufikishiwa Kituo Kikuu cha Polisi Mtwara, ambapo napo alikaa kwa muda wa wiki mbili.

“Katika vituo vyote hivyo tulihojiwa na wakajiridhisha kuwa hatuna tatizo, lakini cha ajabu Desemba 5, 2017, tulishangaa tunapelekwa Mahakamani na kusomewa mashitaka ya ugaidi, kwamba tumefanya ugaidi Manispaa ya Mtwara mjini.” Amesema Ustadhi Bambo.

Alisema, ilimstaajabisha kuelezwa kuwa amefanya vitendo vya kigaidi katika Manispaa ya Mtwara, wakati hajawahi kufika tokea kuzaliwa kwake na kwamba kwa mara ya kwanza Mtwara, amepelekwa na Polisi na kufikia Kituo cha Polisi Mtwara.

“Mimi kwa njia ya Kusini mwisho wangu ni Muhoro tu, lakini ghafla imeonekana nimefika Mtwara Mjini na kufanya vitendo vya kigaidi.” Amesema Ustadhi Bumbo.

Mhanga huyo wa ugaidi alitumia fursa hiyo kuwashukuru Waislamu kwa kuwaombea Dua huku wakiwataka Waislamu wazidi kuomba kwa ajili ya wenzao waliobaki Magerezani.

Wakati huo huo, Waislamu nchini wametakiwa kujiandaa kisaikolojia kwani hawana namna ya kuepuka misukosuko bila kujali umetenda kosa au hujatenda.

Hayo yameelezwa na muhanga mwingine wa tuhuma za ugaidi  Ustadhi Ramadhan Moshi Kakosa, akiongea na Waislamu mara baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Rahma, uliopo Buguruni, Jijini Dar es Salaam.

Ustadhi Kakosa, ni mmoja kati ya Waislamu walioachiwa hivi karibuni, ambaye alikuwa mahabusu tokea mwaka 2017, katika Gereza la Kanda ya Kusini, Lilungu Mtwara.

Ustadhi Kakosa, alisema Waislamu lazima wajifunze katika kadhia hii ya kukamatwa kwao na kupewa tuhuma za ugaidi, kisha kuachiwa kwa maelezo kuwa upande wa mashtaka hauna nia ya kuendelea na kesi hizo.

Ustadhi Kakosa, alisema wimbi hili la kukamatwa Waislamu na kupewa tuhuma za ugaidi, halina uhalisia na huenda lina agenda ambayo wenyewe wanaijua ndio maana hakuna ushahidi ambao umepatikana kulingana na tuhuma walizowapa.

Akijitolea mfano alisema, yeye amekamatwa na kupewa kesi ya ugaidi, lakini sehemu kubwa ya mawaidha na khotuba zake zilikuwa ni kukemea, kulaani na kupinga wanaofanya vitendo vya Kigaidi tokea mwaka 2000, tangu akiwa Mombasa (Kenya).

“Lakini mwaka 2017, nimejikuta nakamatwa na kupewa kesi hiyo hiyo ya ugaidi, jambo ambalo nilikuwa nalikemea na kulipinga kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kwa muda wa miaka 17, na baada ya kukamatwa nikaambiwa mimi najihusisha na vitendo vya Kigaidi.” Amesema Ustadhi Kakosa.

Pamoja na hali hiyo Ustadhi Kakosa, alisema wao kama umma wa Kiislamu wasiogope kusimamia haki na kukemea dhuluma kwa sababu ya hofu ya kukamatwa na kupelekwa magerezani, kuteswa na kuuwawa ikibidi, huo utakuwa si katika msimamo wa Kiislamu.

“Tusiingie hofu na kuacha kuisimamia haki, pia hatutojawa na jaziba kwa kulipa kisasi na kufanya uhalifu, muhimu tushikamane na Manhaj ya Mtume (s a w) ambayo ilikuwa ni ya mminyano, mbinyano wa kifikra mpaka akafikia malengo ya kusimamisha Uislamu Madina.” Amesema Ustadhi Kakosa.

 “Nakutanabaisha ewe Muislamu haswa vijana msiingie hofu na kuacha kufanya kazi ya Ukhalifa lakini pia msiingine jaziba mkatekwa na kujiunga na vikundi ambavyo hujui nani mpishi wake.” Amesema na kutahadharisha Ustadhi Kakosa.

 

Latest News

Most Read

  • Week

  • Month

  • All