Na Bakari Mwakangwale

JUMLA ya wafungwa na mahabusu 3,872, katika magereza 10, wamefikiwa na kupatiwa mahitaji muhimu katika Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani, kwa mwaka 2021.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa ‘Nyota ya Faraja’ Ustadhi Hussein Seif Mchomolo, katika taarifa yake kuhusu program ya kuwasaidia wafungwa na mahabusu, ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu wa 2021.

Ustadhi Mchomolo, amesema kupitia gazeti la An nuur, anapenda kuufahamisha Umma kuwa kupitia michango yao wamefanikiwa kukamilisha Program ya Ramadhani kwa mafanikio makubwa.

Alisema, awali kabla ya Mwezi wa Ramadhani walitoa taarifa ya kukusudia kuwafikia wafungwa na mahabusu Waislamu walio katika Magereza 11 kwa ajili ya kuwapatia huduma ya Futari na Daku katika Mwezi wa Ramadhani mwaka 2021.

Ustadhi Mchomolo, alisema wao (NYOTA YA FARAJA) wakiwa kama wasimamizi wamefarijika kwa uungwaji mkono unaofanywa na waumini na jamii kwa ujumla kwa lengo la kuwasaidia wenye uhitaji.

Ni kwa maana hiyo basi, kwa niaba ya timu yake Ustadhi Mchomolo, akaahidi kuzidi kujituma kwa uadilifu mkubwa ili waweze kuendelea kuwa daraja baina ya jamii na wenye uhitaji ili waweze kutatua changamoto zinazo wakabili.

Akianisha gharama zilizotumika katika kufanikisha zoezi hilo ndani ya Mwezi wa Ramadhani, Ustadhi Mchomolo, alisema jumla ya Shilingi 61,333,250/= zimetumika katika kufanikisha manunuzi ya mahitaji muhimu ya Daku na Futari.

Akitoa shukran, kwa waliofanikisha zoezi hilo alisema shukrani za dhati ziwafikie Waislamu (Members) wa Group la Whatsap la Tawheed Hajj Group, kwa kazi kubwa ya michango, mawazo na maelekezo muhimu.

Baraza Kuu la Wanawake wa Kiislamu Tanzania, chini ya Katibu wake Ukh't Fatma Mdidi, kwa kuhamasika kwa taarifa yao na kufanya juhudi ya kuhakikisha wanafanikisha kufuturisha Magereza Mawili.

Ustadhi Mchomolo, pia amewashukuru Maimamu na Waumini wa Misikiti ya Mtambani (Kinondoni) Masjid Haqqa (Buguruni) Msikiti wa Buguruni Sheli, Msikiti wa Makukula (Buguruni) nao kwa uzipo wake walikubali kuchukua jukumu zito la kuchangia mahitaji ya Futari na Daku kwa Waislamu Magerezani.

Lakini pia aliwashukuru Waislamu mmoja mmoja ambao hawakutaka kutajwa majina yao nao wamefanya kazi kubwa kwa kutoa michango ya hali na mali.

“Bila kuwasahau Mhariri na Mwandishi wa Gazeti la Annur, shukrani kwao kwa juhudi kubwa ya kuhabarisha wito kwa Umma kuhusu wito wa NYOTA YA FARAJA na jamii kuhamasika kujitolea, Allah alidumishe Gazeti letu hili muhimu”

“Pia tunamshukuru Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda kwa maelekezo, ushauri na kutupa uratibu wa baadhi ya mambo yaliyofanikisha kumaliza program hii muhimu kwa ufanisi mkubwa, kwa ujumla makundi yote hayo Allah awalipe kheri.” Amesema Ustadhi Mchomolo.  

 

 

Latest News

Most Read